Unknown Unknown Author
Title: WAALIMU WA SHULE ZA MSINGI WILAYA YA NANYUMBU WALALAMIKIA MANYANYASO NA VITISHO KUTOKANA NA KUDAI STAHIKI ZAO
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Na. Abdulaziz Ahmeid Baadhi ya walimu wa shule za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wanalalamika kunyanyasw...
Nanyumbu
Na. Abdulaziz Ahmeid
Baadhi ya walimu wa shule za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wanalalamika kunyanyaswa na kutishwa kutokana na kudai stahiki zao.

Wakizungumza na Lindiyetu.com kwa nyakati na maeneo tofauti, huku baadhi yao wakikataa majina yao kuandikwa mtandaoni, Walisema sababu ya kunyanyaswa na kutishwa ni kukataa kuhama katika vituo vyao vya kazi vya awali na kuhamia kwenye vituo vingine kabla kulipwa stahiki zao ikiwamo malipo ya usumbufu. 

Mwalimu Leornad Bara wa shule ya msingi Msinyasi, alisema yeye ni miongoni mwa walimu waliopewa barua ya uhamisho na alikwenda kuripoti kwenye kituo kipya hata hivyo tangu apewe barua ya uhamisho mwezi januari mwaka huu, hajapelekewa usafiri na hajahakikishiwa kama atalipwa stahiki zake iwapo atapelekewa usafiri kwani wapo walimu wenzake wanalazimishwa kuhama bila kulipwa fedha za usumbufu na zakujikimu, na wanapata vitisho. Alisema tangu apewe barua ya ya uhamisho hafanyi kazi kwani yeye ameshahama katika kituo cha awali na hajafika katika kituo kipya.

Mwalimu Abdul Rashid wa shule ya Michiga, alisema tangu apewe barua ya uhamisho mwezi Oktoba mwaka jana hafanyi kazi kwani alishakwenda kuripoti kwenye shule aliyotakiwa ahamie hata hivyo hajapelekewa usafiri, Alisema hatakama angepelekewa usafiri asingekwenda bila kuanza kulipwa stahiki zake ingawa baadhi ya walimu wenzake ambao wamekataa kuhama bila kulipwa wanalazimishwa na kutishwa kukatwa mishahara na kufukuzwa kazi. "mwenyewe niliuliza kuhusu malipo kabla ya kuletewa usafiri nikaambiwa niende nikaripoti kwanza, nikawaambia sina nauli mkuu wangu wa elimu kule wilayani akaniambia atanikopesha shilingi 50,000/= nanatakiwa kurejesha mwezi huu kutoka kwenye mshahara wangu, sasa hivi nipo mtaani sifanyi kazi kwasababu uhamisho wangu haujatenguliwa na nilisharipoti katika shule nyingine na bila kulipwa stahiki. zangu sitakubali kuondoka," alisema Abdul.

Hamis Lubanga wa shule ya Michiga alisema, yeye kuwa ni miongoni mwa walimu waliopata uhamisho, hata hivyo tangu muda ambao alipewa barua ya uhamisho na alipokwenda kuripoti katika kituo kipya hajui hatima yake mpaka sasa na hafanyikazi kwani hajapelekewa usafiri na pia anaungamkono kitendo cha waalimu wenzake ambao walipelekewa usafiri wakakataa kuhama kabla ya kulipwa malipo ya usumbufu kwani sheria ndivyo inavyosema ingawa wakubwa wao wanataka sheria ipindishwe na wanawatisha.

Mmoja wa walimu ambaye hakutaka jina lake liandikwe mtandaaoni  aliyejitambulisha kuwa ni mhanga wa mpango huo kutokana na vitisho anavyopata kutoka kwa wakuu wake wa kazi baada ya kukataa kuhama kabla ya kulipwa. Alisema takribani waalimu 30 katika halmashauri hiyo wanalipwa mishahara bila ya kufanya kazi na wengi wao wamegoma kuhama kabla ya kulipwa, japokuwa wameripoti kwenye vituo vipya. 

Alisema yeye alipelekewa gari ili ahame baada ya kuripoti lakini alikataa kuhama bila kulipwa. "mimi na mwenzangu baada ya kukataa kuhamishwa bila kulipwa tumelazimishwa tujisafirishe wenyewe, nibaada ya kuitwa wilayani nakuwekwa kitimoto takribani mara mbili na kupewa vitisho na tuliambiwa hadi tarehe 16 mwezi machi mwaka huu tuwe tumehamia katika vituo vipya kwa gharama zetu vinginevyo tutafukuzwa kazi kwani sisi ni vinara wa mgomo," alisema.

Mwalimu huyo alisema kinachoendelea katika halmashauri hiyo ni vitisho licha yakuwa hata uhamisho unaofanyika nikama unalengo la kukomoa. Kwani wapo walimu wanatarajia kustahafu ndani miezi miwili ijayo lakini wamepewa barua za uhamisho, na wengine ndani ya miezi 10 wamehamishwa mara tatu. "kinachoendelea huku Nanyumbu ni udikteta unaosababisha serikali kupata hasara ya kulipa mishahara ya bure na kwa mtindo huu Matokeo Makubwa Sasa itakuwa ni ndoto kufikiwa".

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Sulpis Likanda alikiri kuwa takribani walimu 30 wamepewa barua za uhamisho kutoka katika vituo vya awali, lakini katika vipindi tofauti na hawajalipwa malipo ya usumbufu. "habari uliyoniuliza nimefuatilia nimegundua ina ukweli kiasi, nikweli takribani walimu 30 wamepata barua za uhamisho hawajalipwa, kati yao 20 wameshahamia katika vituo vyao vipya lakini baadhi ya walimu wamekataa kuhama walipelekewa usafiri, wanasema hawakubali kuhama bila kuanza kulipwa", alisema Likanda. 

Alisema uhamisho huo umefanywa kwa lengo la kuinua kiwango cha taaluma katika shule nyingi zenye upungufu wa walimu, hasa walimu wakuu. "Tumewahamisha kwa kuzingatia kiwango cha bajeti tuliyonayo mwaka huu, hata hivyo nimeambiwa na afisa elimu kwamba fedha hizo hazijaletwa," alisema. 

Alisema walimu hao kuanza kulipwa ni suala la kisheria hata hivyo siyowalimu peke yao wanaodai, hata watumishi wengine wanadai lakini wanaendelea kufanyakazi. Kuhusu walimu waliokataa kuhama na wanatishwa, alikiri kuwa ni kosa. Hata hivyo aliahidi kufuatilia ili athibitishe madai hayo na mengine ambayo hakuyatolea majibu. Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa walimu wengi ambao wamepata barua za uhamisho hawajahamia kwenye vituo vipya huku wakiendelea kubaki katika vituo vya awali bila kufanyakazi.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top