Mfanyakazi wa ndani, Joseph Matonya (26) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mwanagati mwenye umri wa miaka 14.
Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu John Msafiri alisema kuwa mshitakiwa huyo atatumikia adhabu ya viboko ambavyo atachapwa sita akiingia na sita akitoka.
Pia alisema Matonya atatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni moja baada ya kumaliza kifungo hicho.
Hakimu Msafiri alisema mshtakiwa alitiwa hatiani baada ya upande wa mashitaka kuthibitisha mashitaka yake bila ya kuacha shaka kwa kuwa na mashahidi wanne na PF3 iliyothibitisha kubakwa kwa mwanafunzi huyo.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda alidai kwamba mshtakiwa apewe adhabu kali iwe fundisho kwa wengine.
Kabla ya hukumu, mshitakiwa huyo alidai kuwa yeye ni mgeni wa Mahakama na kwamba familia yake inamtegemea na kudai kuwa hakumbaka mtoto huyo.
Pia alidai kuwa adhabu hiyo imemuathiri kisaikolojia na kimwili na kwamba hatasahau maishani mwake.
Ilidaiwa kati ya Novemba na Desemba, 2013, maeneo ya Kitunda Mwanagati, wilayani Ilala, Matonya alimbaka mtoto wa miaka 14 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mwanagati.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.