Unknown Unknown Author
Title: HUU NDIO USAJILI ULIOFANYWA KWA AKILI NA TIMU ZA TANZANIA BARA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Pichani ni Mchezaji wa Yanga Andrey Coutinho akliwa mazoezi  KLABU kongwe na tajiri katika Ligi Kuu Bara za Azam FC, Simba na Yanga kab...
Andrey Coutinho
Pichani ni Mchezaji wa Yanga Andrey Coutinho akliwa mazoezi 

KLABU kongwe na tajiri katika Ligi Kuu Bara za Azam FC, Simba na Yanga kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa 2014-2015, zilitikisa kwenye usajili ambao kila mmoja akiamini amelamba dume.

Lakini baada ya wachezaji hao kuingia mzigoni, wapo wachezaji ambao unaweza kusema klabu hizo zililamba dume zilipokuwa zinasajili kutokana na namna waliosajiliwa walivyowasaidia na wanavyonogesha ushindi wa timu au uchezaji wake. Wachezaji wafuatao wamefanya kazi ya maana mpaka sasa;

Frank Domayo
Anaendesha gari aina ya Alteza. Ni kiungo wa Azam FC, alisajiliwa akitokea Yanga mwanzoni mwa msimu huu, lakini hakufanikiwa kucheza mechi zote za awali kwa sababu ya majeraha ambayo alifanyiwa upasuaji wa nyama za paja la mguu wa kushoto.

Lakini baada ya kupona na kurudi uwanjani, Domayo amekuwa mtamu kwa Azam kwa sababu ubora wake, umeongezeka maradufu.

Sasa ni mfungaji mzuri, analijua goli vizuri sana na sehemu ya mabao yake, yameitoa Azam kimasomaso. Kocha wake, Mcameroon Joseph Omog anajivunia uwepo wa Domayo kikosini hapo kuwa ni mhimili na ameifanya safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho, kuimarika.

Hassan Ramadhani ‘Kessy’
Ni beki wa kulia wa Simba, yeye amesajiliwa katika dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar. Tangu atue kikosini hapo, Kessy amekuwa tegemeo kutokana na namna anavyofanya vizuri.

Ubora wake umedhihirisha hata anapokosekana ni pengo kikosini humo.

Umbo lake ni dogo lakini jamaa ni mtu wa kazi, ana kasi, nguvu na akili ya mpira, anaijua vizuri kuicheza beki ya kulia katika kupandisha mashambulizi na kukaba.

Simba haiwezi kujuta na sasa inajisifu kuwa imelamba dume.

Andrey Coutinho
Ni kiungo Mbrazil wa Yanga ambaye kwenye kikosi hicho anacheza winga ya kushoto. Yanga wana kila sababu ya kujivunia uwepo wake kikosini hapo kwa sababu amekuwa ni chachu ya mafanikio kikosini hapo.

Staili yake ya uchezaji uwanjani ni kama hayupo, lakini ana uwezo wa kufunga na kuchezesha timu hadi Yanga kufikia mafanikio hayo.

Didier Kavumbagu
Awali Kavumbagu alipoondoka Yanga, haikuwashtua sana mabosi wa Jangwani kwa sababu akili zao zilifikiri haraka kuwa, wapo wachezaji wengi wa aina hiyo.

Lakini ukweli wa mambo kwa sasa wanajuta na kila wanapomwona anaifungia Azam mabao, roho huwa zinawauma sana.

Azam imelamba dume ilipomsajili Kavumbagu mwanzoni mwa msimu na sasa amekuwa chachu ya ushindi ya timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Analijua goli, ameshawafungia idadi kubwa ya mabao na kati ya hayo, manane yamemweka kileleni kwa Ligi Kuu na moja la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Juuko Murshid
Sahau kuhusu Straika, Danny Serrunkuma ambaye alitamba sana kwenye ligi ya Kenya msimu kama mitatu mfululizo kabla hajatua Simba. Kuna mtu anaitwa Juuko, ni beki wa kati wa Simba, amesajiliwa kwenye dirisha dogo akitokea Victoria University ya Uganda. Tangu atue kikosini hapo, Juuko ameng’ang’ania kwenye kikosi cha kwanza baada ya kombinesheni yake na Hassan Isihaka kwenda sawa.

Juuko amewafanya Simba wamsahu Mkenya Donald Mosoti ambaye awali alikuwa midomoni mwa mashabiki wa klabu hiyo ilipokuwa inafanya vibaya.

Pascal Wawa
Bonge la mtu halafu anajua. Yanga na Simba zinamtamani lakini hazimuwezi, hazina fedha ya kummudu kuanzia usajili mpaka mshahara. Ni kama mtu anayemiliki Bajaji halafu ghafla anatamani kumiliki Hummer halafu mfukoni ana buku (10,000) za kuweka wese lake la mawazo. Ni raha kwa Azam kumnasa beki wa kati aina ya Wawa. Azam imemsajili beki huyo mwenye mwili mkubwa, nguvu, kasi na akili ya mpira kutoka El Merreihk ya Sudan.

Ni msaada kwa Azam na ameonyesha hayo katika mechi za ligi pamoja na ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya El Merreihk hadi wakashinda 2-0. Ananyambulika, ana uwezo kwenye kuzuia pia katika kupandisha mashambulizi mbele.

Amissi Tambwe
Anajua nini kazi ya straika na kwa nini akakabidhiwa jezi ya Yanga. Walimsajili Tambwe baada ya kuachwa na timu yake ya zamani ya Simba katika usajili wa dirisha dogo.

Mabao yake mawili aliyofunga kwenye mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya BDF ya Botswana ni zawadi tosha kwa Yanga ingawa bado anahitaji juhudi zaidi.

Hana kasi lakini ni mviziaji mzuri, ukimsahau kidogo lazima atakuliza.

Brian Majwega
Mguu wake la kushoto ndiyo unaoirahisisha kazi yake uwanjani. Mara nyingi anachezeshwa winga wa kushoto kwa sababu ya ubora wake, ni mara chache kuona ameharibu mpira.

Ana kasi na staili yake ya uchezaji ni kupambana, anamudu mazingira ya mpira wa aina yote, uwe wa fujo au kasi. Ni tegemeo la Azam kwa sasa.

Emmanuel Okwi
Wanaomjua wanadhani kwamba angeongeza kiwango kidogo tu na kutulia mazoezini angekuwa matata zaidi ingawa hata sasa yuko vizuri.Wengi walidhani atashindwa kucheza mpira kutokana na vurugu zilizojitokeza katika usajili wake akitokea Yanga kujiunga na Simba.

Lakini wakati wapo wanaomwombea dua baya, yeye ameendelea kufanya vizuri na kuwa tegemeo kwenye kikosi cha Simba. Ubora wake upo wazi kwani hata anapokosekana, pengo lake litaonekana tu. Anajua kufunga na kuchezesha timu.

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’
Ni beki wa kushoto wa Simba aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar mwanzoni mwa msimu.

Uwezo wa kufikiri, kasi na nguvu ndiyo vimemfanya kuwa lulu ya mafanikio kwenye kikosi cha Simba. Pamoja na udogo wa umri wake na umbile lake, amekuwa mwiba kwa wakongwe.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top