Tukio hilo limetokea ndani ya ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem na kuweka historia kwa Wema kuwa staa wa kwanza ‘kumwaga’ fedha wakati wa uzinduzi wa bendi ya Yamoto.
MAMBO YALIVYOANZA
Awali, wakati bendi ya Yamoto ilipokuwa ikitumbuiza, ulifika wakati kiongozi wa bendi hiyo, Said Fella alitambulisha uwepo wa Wema kwa kudai amemuwakilisha bebi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond’ hivyo apande jukwaani na kusema chochote lakini mrembo huyo akasema kilichompeleka ukumbini hapo ni uzinduzi wa Yamoto Band.
AMWAGA FEDHA
Mrembo huyo asiyechuja tangu alipotwaa taji la u-miss Tanzania (2006), akiwa na wapambe wake, baada ya kuimba kidogo, alichukua pochi yake na kuanza kummwagia fedha mfululizo Dogo Aslay huku akiwa anamzunguka kwa kucheza.
ASLAY APAGAWA
Kwa fedha hizo zilizokadiriwa kuzidi milioni moja alizotunzwa Aslay, ilifika wakati dogo huyo akawa anaziangalia tu kama bubu na kupigwa butwaa huku akiishia kuzitazama bila kuimba chochote.
Katika hali iliyowashangaza wengi, baunsa mmoja aliyekuwa akimlinda Wema alimzuia staa huyo kuendelea kutoa fedha zaidi akidai zimetosha ndipo akaacha na kushuka jukwaani.
KWA NINI ASLAY TU?
Wakati zoezi hilo likiendelea, kuna baadhi ya mashabiki waliibua minong’ono wakihoji kwa nini atunzwe Aslay peke yake wakati bendi hiyo ina wakali wengine watatu, Malomboso, Enock na Beka?
“Mbona kama anampendelea Aslay tu wengine hawatunzi ona hela zote ameshikilia yeye tu kweli, inaonekana anamzimia sana Aslay, si bure, haikatazwi lakini,” alihoji shabiki mmoja aliyekuwa akifuatilia shoo hiyo.
Wema ameonekana kuja juu kwa sasa kifedha, wiki iliyopita alifanya tukio kama hilo katika Ukumbi wa Thai Village Masaki kwa kumtunza ‘pesa ndefu’ mwanamuziki wa Bendi ya Skylight, Sam Mapenzi huku ikidaiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kumziba mdomo aliyekuwa shosti wake, Kajala Masanja ambaye inadaiwa kwa sasa yuko ‘vizuri’ kifedha.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.