KITENDO cha baadhi ya akina mama wajawazito kujenga mazoea ya kujifungulia majumbani,badala ya kwenye vituo na kupima afya zao, kimetajwa kuchangia maambukizi ya VVU kwa watoto wachanga hapa nchini.
Hayo yamebainika katika taarifa iliyowasilishwa na wizara ya afya kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari,yaliyofanyika wilaya ya Bagamoyo,mkoani Pwani.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliandaliwa na kuendeshwa na wakufunzi kutoka Asasi ya Elizabert Graser Pediatric Aids Foundation (Egpaf) wakisaidiwa na mkufunzi kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam,Charles kayoka.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,iliyowasilishwa katika mafunzo hayo, na Afisa mipango kitengo cha kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Grace Denis, imesema baadhi ya akina mama wanaojifungulia majumbani, wanakosa nafasi ya kupima zao afya na kupatiwa dawa za kupunguza makali (ARV) kwa waathirika na huduma za uzazi salama.
Taarifa hiyo imeeleza ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa watoto wachanga, wizara kwa kuwatumia wataalamu wake washauri na wadau, imeandaa mpango mkakati wa kitaifa wa miaka mitano kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji wa masuala yanayohusu ukimwi.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa lengo la mkakati huo ni kutaka kuongeza ushawishi, hamasa na kukubalika kwa huduma za PMTCT katika kupunguza kwa asilimia 90% ya maambukizi mapya kwa watoto na MTCT hadi kufikia kiwango cha pungufu ya asilimia 5% ifikapo mwaka kesho.
"Kwa mujibu wa ripoti ya PMTCT ya mwaka 2013, inaonyesha kiwango cha maambukizi kwa watoto ni chini ya asilimia 15.7%" imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema ili kuweza kutokomeza maambukizi mapya kwa watoto, jamii haina budi ikachukuwa taadhali kwa kuacha kushiriki ngono zembe, kubeba mimba zisizotarajiwa na kutumia huduma za afya ya uzazi.
Aidha, taarifa hiyo, imeeleza ili kutokomeza VVU kwa watoto ifikapo mwaka kesho, waandishi kupitia vyombo vyao vya habari hawana budi kutumia karamu zao kuandika na kuzitangaza ili kuwafikishia taarifa wananchi waliowengi, waweze kuzifahamu huduma za kutokomeza maambukizi ya VVU.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo, wameshauri watendaji wakiwemo wa kitengo cha kutoa taarifa, kuacha tabia ya kukwepa kuzungumza na vyombo vya habari, pamoja na kukanusha taarifa wanazozitoa ili kuondoa manung'uniko kwa waandishi.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.