Unknown Unknown Author
Title: WASTARA: NITAKUFA KWA AJALI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MASKINI! Staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma amezungumzia jinsi jinamizi la ajali linavyoweza kumsababishia kifo kwani ana msurur...

MASKINI! Staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma amezungumzia jinsi jinamizi la ajali linavyoweza kumsababishia kifo kwani ana msururu mrefu wa matukio hayo, Amani lina mzigo kamili.

Wastara jumaStaa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili yaliyodumu kwa takriban saa mbili kwenye Ofisi za Global Publishers zilizopo Bamaga-Mwenge jijini Dar hivi karibuni, Wastara alisema tayari ameshapata ajali kumi tangu kuzaliwa kwake, mbili zikimtokea jirani na nyumbani kwake Tabata-Bima, Dar.

AJALI YA KWANZA
Wastara ambaye ni mjane wa aliyekuwa mwigizaji wa filamu za Kibongo, marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’, alisema ajali ya kwanza aliipata mwaka 1987 akiwa na miaka minne.
Alisema ajali hiyo ilimtokea mkoani Morogoro, aligongwa na pikipiki. Mguu wa kulia ulisagika, akakaa miezi kumi nyumbani akiwa hawezi kutembea.
“Nilipopona sawasawa nilianza kutembea kwa kujifunza kama mtoto anavyofanya,” alisema Wastara.

AJALI YA PILI
Nyota huyo alizidi kuweka wazi kwamba, mwaka huohuo alipata ajali ya pili akiwa mkoani humo ambapo aligongwa na baiskeli kisha kuvunjika mkono wa kulia, akafungwa plasta ngumu au hogo (P.O.P).

AJALI YA TATU
Wastara ambaye alitamba na Filamu ya Mboni Yangu alisema mwaka mmoja na nusu baadaye, yaani 1990 alipata ajali ya tatu akiwa na pacha wake aitwaye, Issa Juma.
“Nakumbuka ilikuwa Ramadhan ya kwanza, wakati huo tulikuwa tunaishi Mlandizi (Bagamoyo, Pwani).

“Siku hiyo kuna mzee mmoja alitupa shilingi mia, tukagawana hamsini-hamsini. Mimi nilinunulia maembe. Mwenzangu akakataa kutumia fedha yake, nikamwambia mimi natumia ya kwangu kwa sababu tunaweza kugongwa kabla hatujatumia fedha yetu.

“Kweli haikuchukua muda. Wakati tunavuka barabara pale Mlandizi mbele yetu kuna mtu alikuwa na baiskeli, tukashika nyuma, ile anavuka na sisi tukafuata, ghafla gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Chalinze kuelekea Dar likatokea na kutugonga mimi na kaka yangu.

“Kwenye ile ajali mimi nilipasuka fuvu (akionesha kovu kichwani), kaka yeye alivunjika mguu wa kushoto,” alisema Wastara na kuongeza:
“Tulipelekwa Hospitali ya Tumbi, Kibaha. Sikumbuki tulikaa kwa muda gani lakini ulikuwa muda mrefu.”
AJALI YA NNE
Kama hiyo haitoshi, staa huyo aliongeza kuwa akiwa na umri wa miaka 15 alianguka kwenye ngazi nyumbani kwao mkoani Morogoro, akavunjika mkono.
AJALI YA TANO
“Mwaka 2008, nilipata tena ajali ya pikipiki. Ilikuwa maeneo ya Mwananyamala Sokoni (Dar).
“Dalali niliyekuwa naye alikuwa na pikipiki, nilipanda nyuma akaingia chini ya Toyota Coaster ya Mbagala-Mwenge.

Niliumia magoti na mguu wa kushoto, damu zikatoka. Lakini ajali hii nayo niliishaiona mapema.
“Nasema niliona mapema kwa sababu siku hiyo wakati naondoka nyumbani nilivaa suruali nyeupe lakini nikasema huenda ikachafuka, nikabeba nyingine nyeusi kwenye mkoba jambo ambalo siyo kawaida yangu.

“Baada ya ajali, nilipelekwa hospitali moja maeneo ya Kijitonyama, siikumbuki jina. Nilikuwa nimechafuka kwa matope, ukichanganya na damu ndiyo kabisa ikawa balaa.
“Daktari alipomaliza kunihudumia ndiyo nikakumbuka ni kwa nini niliibeba suruali nyeusi, nikabadili,” alisema staa huyo.
AJALI YA SITA
“Hii ndiyo ile kubwa. Ndiyo  iliyonivunja mguu na baadaye ukakatwa. Ilikuwa siku tatu mbele baada ya ajali ya Mwananyamala.

“Siku hiyo nililala kwa Sajuki.Wakati naondoka asubuhi alifika rafiki wa Sajuki anaitwa Hamis. Nilitakiwa kuwahi pale Njia Panda ya Tabata-Bima ili nipande gari kwenda dukani ambako nilikuwa nauza.
“Sajuki aliazima pikipiki ya Hamis lakini kabla ya kuondoka nilimwambia sitaki anipeleke yeye, maana ataniua, kwa utani na yeye alisema ‘we panda nikakuue’.

“Baada ya mvutano wa kukataa, mwisho nilikubali, lakini nilirudi ndani kwanza na kujiangalia kwenye kioo, nikasema moyoni mbona miguu yangu haijakaa vizuri?

“Kweli, tulipofika Njia Panda, Tabata-Bima kulitokea (Toyota) Corolla, ikasimama kuturuhusu kupita, lakini ghafla nikasikia bung! Halafu nikajikuta nipo mtaroni.
“Nilitaka kuinuka, watu wakawa wanapiga kelele nisisimame nitakufa, nikaendelea kulala. Nilijiuliza hivi kweli nipo salama au?

“Madereva teksi wakanunua mfuko wa rambo, wakautia mguu wangu na kuufunga ili damu ivujie humo na kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili.
“Hali ya mguu ilipozidi kuwa mbaya, nilipelekwa kwa Dk. Baki, Tumbi-Kibaha na baadaye mguu ukakatwa.
AJALI YA SABA

“Mwaka 2009 nilikuwa mkoani Njombe eneo la stendi ya mabasi, nikiwa tayari nina mguu wa bandia, mguu huo ulichomoka ghafla. Nilikuwa sijauzoea vizuri. Nilianguka vibaya mno mbele za watu. Niliumia mkono,” alisema Wastara.
AJALI YA NANE
“Siku hiyohiyo niliingia chooni kwenye hoteli niliyofikia, cha ajabu nikajipigiza kichwa kwenye sinki, niliumia sana kichwani. Kishindo cha kujipigiza watu wote kwenye hoteli walishtuka na kuja kutaka kujua nini kilitokea,” alisema.
AJALI YA TISA
Wastara aliendelea kusimulia: “Baada ya Njombe, nilipata ajali tena maeneo ya Popobawa-Tandale (Dar). Nilikuwa na gari langu dogo, Toyota Vitz. Niliingia chini ya Toyota Coaster, sikuumia ila gari iliumia kidogo. Hapo Sajuki alikuwa ameshafariki dunia.”
AJALI YA KUMI
“Hii ndiyo mbichi, ilinitokea Februari 13, mwaka huu palepale Tabata-Bima nilipopotezea mguu wangu. Siku hiyo nilikuwa nakwenda kutoa fedha ATM nikanunue umeme.

“Ile naingia tu barabarani lilitokea lori likanigonga na kunirushia mtaroni na gari langu la Vitz.
“Niliumia tena kichwani, gari lilivunjika vioo na taa,” alisema Wastara jinsi ambavyo msururu wa ajali zilivyokosa kuutoa uhai wake huku akijitabiria kifo cha ajali kwa kusema:

“Yaani ajali ajali kila mara. Nadhani nitakufa kwa ajali. Lakini Mungu ndiyo anajua mimi nitakufaje.”
MAMA AMWEKEA NADHIRI
Wastara mwenye umri wa miaka 31 sasa ambaye aliolewa ndoa ya kwanza akiwa na miaka 15, alisema akiwa mdogo, mama yake alimwekea nadhiri kwamba kutokana na kuandamwa na jinamizi la ajali akifikisha miaka 15 salama angemfanyia Maulidi jambo ambalo alilifanya.
KUNA MKONO WA MTU?
“Ni kweli nahisi kwamba kifo changu kitatokana na ajali lakini siamini kama ni mkono wa mtu. Naamini kila kitu ni mpango wa Mungu. Mimi si mtu wa imani nyingine tofauti na kumtegemea Mungu. Najua ana mipango yake juu ya maisha yangu,” alimaliza Wastara.

Wastara alimpoteza mumewe Sajuki mapema Januari 2, 2013 baada ya kuumwa kwa muda mrefu huku akiachiwa mtoto mmoja.

>>GPL

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top