Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 25
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 25 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA......!!!! Kila mmoja alikuwa akitetemeka, wakahisi nyoka mmoj...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 25
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 25
ILIPOISHIA......!!!!
Kila mmoja alikuwa akitetemeka, wakahisi nyoka mmoja akija na kuanza kuzunguka miguuni mwa Kareem, alivumilia, hakutingishika lakini nyoka huyo alipoanza kutembea chini ya Saida, akashtuka na kuanza kupiga kelele, hakutaka kusimama, akaanza kukimbia kusonga mbele, Kareem alipomfuata tu, sehemu ile ikadidimia na kuanza kuingia ndani. Wote wakaanza kuporomoka kuelekea chini huku wakipiga kelele za kuomba msaada.

“Puuu...puuu...” wakatua chini kwa nguvu, sehemu iliyokuwa na mawe mengi. Hapohapo wakatulia kama walivyokuwa, wakapoteza fahamu na hawakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

ENDELEA NAYO SASA.....
Wote walikuwa kimya, walipoteza fahamu na hawakujua kitu gani kiliendelea baada ya wao kuanguka chini. Walikuwa kimya kabisa, walionekana kama tayari walikwishakufa kwani hawakutingishika, ni damu tu ndizo zilizokuwa zikiwatoka vichwani mwao.

Walikuwa kimya kwa zaidi ya saa mbili ndipo Kareem akarudiwa na fahamu. Kitu cha kwanza alishangaa, hakukumbuka alikuwa wapi, akainuka na kukaa kitako, sehemu aliyokuwa ilikuwa na mwanga hafifu ambayo haikumfanya hata kuona hatua kumi mbele.

Chini, kulikuwa na mawe mengi kitu kilichomfanya kuogopa. Baada ya kukaa kwa sekunde kadhaa, akakumbuka kila kitu kilichotokea na alipoangalia pembeni, akamuona Saida akiwa amelala.

Aliogopa, kwa jinsi alivyokuwa akionekana msichana huyo, alikuwa kama mtu ambaye tayari alikufa. Akaanza kumsogelea kwa magoti, alipomfikia, akamshika na kuanza kumuita huku akimtaka kuamka.

“Saida mpenzi...Saida mpenzi amka,” alisema Kareem huku akiendelea kumwamsha mwanamke huyo.
Saida hakuamka, kitu alichohisi Kareem ni kwamba Saida alikuwa amekufa, alilia sana, aliumia moyoni mwake, akalipeleka sikio lake katika upande wa kushoto kifuani mwa Saida na kuanza kusikiliza mapigo ya moyo.

Yalikuwa yakidunda kwa mbali sana, alikuwa na hofu kwamba mpenzi wake alikuwa akielekea kufa kitu kilichoibua huzuni kubwa moyoni mwake. Alichokifanya ni kumnyanyua na kuanza kuondoka naye mahali hapo.

Hakuwa na nguvu za kutosha, kichwa chake kilitapakaa damu lakini hakutaka kujali, alipokuwa akielekea ilikuwa ni sehemu ambayo aliamini kwamba ni salama, hakujua huko mbele kulikuwa na nini, ila alichokifanya ni kusonga mbele kwa kuamini kwamba ilikuwa njia ya kuelekea sehemu salama.

Chini kulikuwa na mawe mengi, hakujua palikuwa sehemu gani, hakujua alikuwa akielekea wapi, alisogea mbele huku mwili wa mpenzi wake ukiwa shingoni mwake, alipofika sehemu fulani, kwa mbele akaona mwanga mkubwa ukiwa unaingia mpaka kule walipokuwa.

Akakazana, alipofika karibu na mwanga huo ambapo kulionekana kuwa kama mlango fulani, akaanza kusikia sauti kubwa ya maji yaliyokuwa yakimwagika sehemu. Akahisi kwamba ilikuwa sehemu salama, alipiga hatua mpaka kuufikia mlango ule, kitu alichokiona kilikuwa ni maji, alitokea katika Bahari ya Mediterania.

“Hatimaye tupo baharini,” alijisemea huku akianza kuonyesha tabasamu pana.

Mbele yake kulikuwa na bahari kubwa, hakukuwa na mtumbwi wala kitu chochote kile ambacho kingewafanya kuvuka mahali hapo. Alikuwa akiangalia huku na kule kuona kama angeweza kuona mtu yeyote yule ili amuombe msaada wa kuja kuwachukua.

Hakukuwa na mtu yeyote yule. Mpenzi wake, Saida alikuwa akitoka damu kichwani, kipindi walichokuwa wameanguka walivipigiza vichwa vyao katika mawe yaliyokuwa mule na ndiyo maana walijikuta wakipoteza fahamu.

“Tutatokaje?” alijiuliza huku akimwangalia Saida na kuangalia bahari ile.

Wakati akiwa hajui ni kitu gani walitakiwa kufanya, mara Saida akaanza kuyafumbua macho yake. Akamuona mpenzi wake na kumuita kwa sauti ya chini. Kareem akayapeleka macho yake kwa Saida, alikuwa hai na uso wake ulikuwa na tabasamu pana.

“Mpenzi wangu...” aliita Kareem huku akimuweka chini vizuri.
“Tupo wapi? Nini kilitokea?” aliuliza Saida huku akimwangalia mpenzi wake machoni.
“Tulidondoka kule pangoni. Nilizinduka na kukubeba kukuleta huku,” alijibu Kareem huku akimwangalia mwanamke huyo.

Hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kutoka hapo walipokuwa. Walibaki wakiwa wamekaa chini. Hiyo ilikuwa majira ya saa mbili asubuhi, hawakuona mtu yeyote yule.

Hawakuweza kuondoka, waliendelea kubaki mahali hapo. Njaa ikaanza kuwauma, hawakujua wangekula nini, hawakujua ni kwa jinsi gani wangepata chakula. Kitu walichoingiza mdomoni mwao kilikuwa ni maji ya bahari hayo ambayo hayakuwa na chumvi nyingi kama bahari nyingine.

Walikaa na njaa, walivumilia mpaka ilipofika saa tisa alasiri ambapo kwa mbali waliweza kuuona mtumbwi mmoja uliokuwa na watu wanne, Kareem akaanza kuwaita watu hao.

Sauti yake haikutoka vizuri lakini hakutaka kunyamaza, aliamini kwamba wangemsikia na hivyo kuja kuwasaidia. Hiyo ilionekana kuwasaidia kwani watu hao waliwaona na kuanza kuwafuata kule walipokuwa.

Walionekana kuwa na hofu, waliwaangalia Kareem na Saida, wakawaambia waingie kwenye mtumbwi na waondoke eneo hilo haraka iwezekanavyo.

“Nyie mlikuwa pale?” aliuliza mzee mmoja huku akionekana kutokuamini.
“Ndiyo! Kuna nini?”
“Aisee! Hivi hamjui kama ile sehemu iina miujiza na watu huwa hawatoki pale salama. Mliingia kwenye lile pango?” aliuliza mzee huyo, kila alipokuwa akiwaangalia, hakuamini kama alikuwa akizungumza na watu hao.
“Ndiyo!”
“Sasa imekuwaje kuwa salama?” aliingilia mzee mwingine, kama alivyokuwa yule wa kwanza, hata naye alikuwa akishangaa.
“Ni habari ndefu!”
“Hivi mnajua kwamba hapa Misri sehemu ile ndiyo inaongoza kuwa na mamba wengi? Mnajua kwamba sehemu ile ndiyo inaongoza kuwa na mauzauza mengi na kila mtu akayesimama katika mlango wa pango lile lazima afe? Sasa nyie imekuwaje kuwa hai?” aliuuliza mzee yule wa kwanza.
“Hata sijui!”
“Au siku hizi hakuna mauzauza?” aliuliza mwingine.
“Yapo sana. Siku hizi tatu zilizopita Wazungu wanne waliingia mule, hawakutoka. Waliliwa na mamba na wengine kuchukuliwa na majini,” alijibu mzee mwingine.
“Basi kweli Mungu yupo na hawa watu,” alisema mzee mwingine.

Walionekana kuwa na bahati mno, katika pango walilokuwepo lilijulikana kama pango la kifo lakini pamoja na hatari yote iliyokuwa mule bado walinusurika na kuwa wazima wa afya.

Waliwashangaa, wakati mwingine waliona kama watu hao walikuwa malaika kwani haikuwa rahisi kwa mtu kunusurika ndani ya pango lile au katika mlango wa kuingilia katika pango lile ambapo hapohapo ndipo Kareem alipokuwa amekaa na Saida.

Safari iliendelea mpaka walipofika katika Mji wa Alexandria ambapo wakateremka na kuondoka. Walikuwa hoi, japokuwa walinawa vichwa vyao lakini bado damu zilikuwa zikiendelea kuwatoka vichwani mwao.

“Ni lazima uondoke kuelekea Tanzania, huku si salama tena,” alisema Kareem, alikuwa akimwambia mpenzi wake, Saida.
“Nitafurahi sana!”

Wakaanza kuulizia mahali ulipokuwa ubalozi wa Tanzania, hawakupata tabu, wakaelekezwa sehemu ulipokuwa na kitu kilichowafurahisha ni kwamba haukuwa Cairo kipindi hicho, ofisi zake zilikuwa Alexandria hivyo walitumia muda mfupi mpaka kufika huko.

“Wewe ndiye Saida?” aliuliza balozi Christopher Makame, hakuwa akiamini kama msichana aliyekuwa akimwangalia alikuwa Saida.
“Ndiyo!” alijibu Saida.
“Yule wa kule Oman?”
“Ndiyo!”
“Aliyetoroshwa wakati alipotakiwa kupigwa mawe?”
“Ndiyo!”

Balozi hakuamini, mtu huyo bado aliendelea kuwa gumzo kila kona, Watanzania waliokuwa Oman walijitahidi kumtafuta katika kila pembe ya nchi hiyo lakini hawakufanikiwa kumpata na hata waliposikia kwamba alikuwa Iran, pia walimtafuta lakini hawakumpata kitu kilichomfanya kila mmoja kujua kwamba alikufa.

Akawachukua wote wawili na kuwapeleka kwake, kwanza wakala na kuwataka walale mahali hapo kabla ya kuanza safari ya kwenda Tanzania. Hapo ndipo Kareem alipogundua kwamba baba yake alikuwa amekufa katika ndege iliyokuwa imepotea.

Alihuzunika mno lakini kila alipokuwa akimwangalia Saida, moyo wake ulikuwa na amani tele kwani mwanamke huyo alikuwa kila kitu katika maisha yake.

“Saida, ninakupenda sana mpenzi wangu,” alisema Kareem huku akimsogelea mwanamke huyo.
“Ninakupenda pia. Ahsante kwa kila kitu ulichokifanya kwa ajili yangu! Ulihatarisha maisha yako kwa ajili yangu! Nashukuru sana mpenzi,” alisema Saida huku akilia, kwake, Kareem alionekana kama malaika aliyeletwa duniani kwa ajili yake, yaani walikutana Facebook lakini mwisho wa siku mwanaume huyo alimuonyeshea mapenzi mazito ambayo hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angeweza kumuonyeshea.

Je, nini kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Mwisho ya Simulizi Hii


++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top