Mtoto mchanga aliyetelekezwa na mama yake
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni ACP, Camillius Wambura, amethibitisha kutokea kwa tukio hiloa ambapo amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kumtafuta mama mzazi wa mtoto huo.
Tukio hilo limetokea Aprili 16, mwaka huu, ambapo wasamaria wema walifanikiwa kumuokoa mtoto huyo kisha kumpeleka katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo Bunju A, na baadaye alihamishiwa katika kituo cha Polisi cha Wazo, ambapo pia ilikutwa barua aliyoiandika mama wa mtoto huyo ikiwa karibu na mtoto huo.
Aidha aliandika barua yenye maelezo mafupi yanayoelezea maisha yake, huku akielekeza lawama kwa mzazi mwenzake ambaye hakumtaja jina kuwa amemtelekeza muda mrefu bila kumpatia mahitaji muhimu kabla ya mtoto huyo kuzaliwa, hali iliyomlazimu kuchukua uamuzi wa kumtelekeza mtoto huyo.
Aidha barua hiyo ambayo FikraPevu imeipata, inasema kuwa mama mzazi wa mtoto huyo alitaka kujiua kwa kunywa sumu, ingawa hakufanya hivyo.
“Sijamuacha kwa ubaya ninampenda mwanangu sana ila kutokana na maisha yangu kuwa magumu, nimeamua kumtelekeza hapa ili apate msaada kwa wasamaria wema, mzazi mwenzangu kanikataa kuanzia kwenye mimba nimejaribu hata kutoa ila imeshindikana” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Kwa mujibu wa barua hiyo inaeleza kuwa mtoto huyo alizaliwa Machi 17, mwaka huu, katika eneo la Mistuni kufukuzwa kila mahali, ambapo mtoto huyo hajawahi kupata chanjo ya aina yeyote, ambayo inatakiwa kutolewa kwa mtoto mchanga ili aweze kupata kinga ya kumkinga na maradhi mbalimbali.
Barua iliyoachwa na mama wa mtoto huyo
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na Visiwani umebaini kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo huku matukio 996 ya udhalilishaji yaliripotiwa kutokea katika wilaya sita za Zanzibar.
Kati ya matukio hayo, 242 yalihusu ubakaji, vipigo vilikuwa 388, ndoa za utotoni 42, kutelekezwa 96, mimba za utotoni 228, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara ukionyesha kuwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara inaongoza ikiwa na matukio 132.
Ripoti ya Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Tanzania, iliyotolewa na serikali pamoja na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) mwaka 2011, ilidhihirisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba nchini Tanzania hukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
>> FikraPevu
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.