Baada ya kucheza michezo mitano ya ligi kuu ya vodacom bila ya kupata ushindi wakiambulia sare tatu na kupoteza michezo miwili leo Simba SC wamepata ushindi wa goli 3-2 mbele ya Ruvu shooting waliotokea kwenye kichapo cha goli 7 toka kwa Yanga.
Katika mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Simba SC walienda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 2-0, magoli yote yakifungwa na Hamisi Tambwe.
Hamisi Tambwe aliandika goli la kwanza katika mchezo wa leo katika dakika ya 23 akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Ruvu shooting kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Said Ndemla na kuipa Simba goli la uongozi.Tambwe alifunga goli lake la 19 msimu huu likiwa la pili katika mchezo wa leo katika dakika ya 32 akimalizia pasi ya Haruna Chanongo na kuipeleka Simba mapumziko wakiwa mbele kwa goli 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu shooting kusaka magoli ya kusawazisha na mnamo dakika ya 72 Saidi Dilunga aliandikia Ruvu shooting goli la kwanza kwa kichwa akiunga kona ya Michael Idan.
Wakati Ruvu shooting wakihaha kupata goli la pili na la kusawazisha walijikuta wanaruhusu goli la tatu lililo tiwa kimiani na Haruna Chanongo katika dikaka ya 77.
Ruvu shooting walifanikiwa kupata goli la pili kwa mkwaju wa penat katika dakika ya 82 baada ya Joseph Owino kuushika mpira na kupeleka mchezo kumalizika kwa simba kuibuka na ushindi wa goli 3-2 mbele ya ruvu shooting ya Pwani.
Picha kwa hisani ya BINZUBERY