Twiga Stars imepoteza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) baada ya leo kufungwa mabao 2-1 na Zambia (Shepolopolo) kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa suluhu.
Wenyeji ndiyo walianza kupata bao lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya 75. Mfungaji huyo aliyeingia kipindi cha pili nchini alimalizia wavuni pira uliotemwa na kipa Fatuma Omari.
Dakika nne baadaye Zambia ambao walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na washabiki wao baada ya kufunga la kwanza, walipata bao la pili ambalo nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili alijifunga mwenyewe.
Mwasikili alikuwa akijaribu kutoa nje mpira uliopigwa na nahodha wa Shepolopolo, Mupopo Kabange ambapo ulipishana na kipa Fatuma Omari kabla ya kujaa wavuni.
Bao la Twiga Stars lilifungwa na Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa kushoto ambaye pia ni mchezaji wa Tanzanite alipanda mbele kuongeza mashambulizi ambapo akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti lililomshinda kipa Hazel Nali.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema amebaini upungufu katika kikosi chake ambao ataufanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano ili timu yake iweze kusonga mbele.
“Kwa matokeo haya bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano nyumbani na kusonga mbele,” alisema Kaijage.
Twiga Stars iliwakilishwa na Fatuma Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel, Fatuma Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa Mtumwa/Amina Ali, Asha Rashid, Etoe Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.
Timu hiyo inarejea nyumbani kesho kwa ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.