Unknown Unknown Author
Title: MAHABA: UMESHAGUNDUA ANACHOHITAJI MWENZI WAKO?
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
INAHITAJI kufikiri tu ili uweze kuwa katika uhusiano bora. Ukiacha ubongo wako nafasi ya kujifunza vitu vipya, hakika hakuna kitakacho-kusum...

INAHITAJI kufikiri tu ili uweze kuwa katika uhusiano bora. Ukiacha ubongo wako nafasi ya kujifunza vitu vipya, hakika hakuna kitakacho-kusumbua katika mapenzi.clip_image001Hata hivyo, ukiwa mwenye kujijali mwenyewe, hasira, chuki na mgomvi wakati wote, hutajenga uhusiano imara. Mapenzi ni furaha, hata siku moja, ubabe haujawahi kutengeneza ladha iliyo sawasawa kwenye mapenzi.

Hapa katika All About Love ni sehemu yako sahihi kukuza ufahamu wako. Jambo kubwa na la msingi kutambua ni kwamba, makala ninazoandika hapa huwa ni baada ya kufanya uchunguzi usio rasmi kutoka katika jamii inayotuzunguka.

Wenye lugha wanasema; akili za kuambiwa, unachanganya na zako. Una uhuru wa kuchukua yale unayoyaona yanafaa kutoka kwa Shaluwa na kuacha yale ambayo kwako hayana mashiko ili kuboresha uhusiano wako.

Umeshawahi kuchunguza anachohitaji mpenzi wako au huwa unakwenda tu bora liende? Hapo ndipo kwenye mzizi hasa wa mada hii. Rafiki zangu, wakati ukijifikiria wewe katika ulimwengu wa mapenzi, unatakiwa pia kumfikiria mpenzi wako!
Kwa bahati mbaya, katika eneo hili, wanaume wengi huwa hawafikirii sana namna ya kuwafurahisha wenzi wao. Wanahisi ni suala linalowahusu wanawake pekee. Ni kosa.

Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua. Vipengele vinavyofuata hapa chini vinachambua vizuri mambo ambayo wanawake wengi wanapenda kufanyiwa na wanaume wao. Twende tukaone.

USAFI
Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya nyumba au ua la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.

Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia sebeleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele. Rafiki yangu, kama uko mbali na usafi, ujue kuwa itakuwa vigumu kupata mdada wa ukweli – yule wa ndoto zako.

MWANAUME KUJIAMINI
Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini – mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika. Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia manukato mapya!
Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa maamuzi yasiyoyumba.

Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!  Usiyebadilika kama kinyonga!

UWE FITI!
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni kwenye upande wa kujitetea zaidi – lazima uwe fiti! Wakati unapodai haki yako mbele ya mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.

Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi na ambaye yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au watu wabaya wenye lengo la kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye fiti ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.

ANAYEJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume wanaowajali. Wanaowaona wao ni kila kitu na wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
Wanaume wengi ni wavivu, si tu kuwatumia hata SMS za “mambo dia?” wapenzi wao lakini hata kujibu tu, “nipo poa mama, siku yangu ni nzuri na nafurahi kunikumbuka...” wanaona shida!

Si hulka ya wanaume kutumatuma SMS – inajulikana, lakini angalau ukiweza kulifanya hili hata kidogo tu, utakuwa unajiongezea pointi kwa mwenzi wako.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top