Wafanyabiashara wa manispaa ya Lindi wakiwa katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Double “M” tarehe 04/11/2013, ambapo walikusanyika na kufanya mkutano wa pamoja wa kuzungumzia tozo mbalimbali za manispaa na TRA
Ndg: Ismail Khaify akichangia jambo katika mkutano huo wa wafanyabiashara uliofanyika Jana tarehe 04/11/2013 katika ukumbi wa Double “M”
Uongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara Manispaa ya Lindi ukisikiliza kwa makini maoni ya wajumbe wa mkutano huo ambao ulitoa hoja mbalimbali nazo ni kama inavyoseomeka hapa chini kwenye taarifa yao walioitoa kwa Vyombo vya Habari.
*****************************
MKUTANO WA WAFANYABIASHARA ULIOFANYIKA UKUMBI WA
DOUBLE ‘M’LINDI MJINI TAREHE 04/11/2013
HOJA ZILIZOAINISHWA KUTOKA KWA WAFANYABIASHARA MBALIMBALI
1. Kurejesha Leseni kwa wafanyabiashara bila ya taarifa na kwa viwango vikubwa.
- Wafanyabiashara kutoshirikishwa katika urejeshaji wa leseni za namabadiliko ya viwango stahili kulingana na biashara wanazofanya
- Viwango vilivyotumia kwa baadhi ya biashara ni vikubwa ikilinganishwa na biashara zinazofanywa.
- Pamoja na kulipia leseni hizo baadhi ya wafanyabiashara hadi sasa hawajapatiwa Leseni.
2. Ushuru wa Service Levy
- Manispaa imewakabidhi mawakala kutoza ushuru wa service Levy na ambao hutozwa bila ya taratibu zilizoanishwa, viwango stahili na mfumo wa ukusavyaji ushuru huo.
- Mawakala wamekuwa wakiwalenga baadhi ya wafanya biashara kwa kuwapelekea madai makubwa yasiyoambatana na taarifa zozote za makadirio ya ushuru husika.
- Mawakala huwatishia wafanyabiashara kwa kuwapatia summons za kuitwa mahakamani kwa madai ya ushuri wa service levy na baadae kuwataka wamaliziane nje ya mahakama kwa kulipa kiasi nje ya utaratibu bila ya mwanasheria wa Manispaa kufahamu na yeye ni msimsmizi wa kesi na mashauri yote ya madai kwa Manispaa.
3. Fire Extinguisher
- Watumishi wa Idara ya zimamoto wamekuwa wakipita kwenye maduka na kuwataka walipe ushuru wa fire extinguisher kiwango cha laki moja kila mlango wa biashara na pia kuwataka wanunue kifaa hicho kwa gharama zao na kuwapa siku 14 wawe wametekeleza. Baadhi yao ambao hawajatekeleza agizo hili huwalipisha faini si chini ya Laki mbili na huwajazia fomu za malipo ya ushuru pamoja na faini na kuwatakaa waingize pesa hizo kwenye akaunti ya NMB nambari wanayoitoa.
- Uelewa wetu ni kuwa makusanyo yote ya serikali yana maeneo maalum na yanatoa stakabadhi ya mapokezi ya pesa, na tunashangazwa na utaratibu huu unaotumiwa na watumishi hawa wa kutokuwa na ofisi maalum ya ukusanyaji ila NMB.
4. Mabango ya Biashara.
- Mawakala wa Manispaa wamekuwa wakipita kwenye maduka na kutoza shs elfu kumi 10,000/= ikiwa ni ada kwa mfanya biashara kulipia bango ama maandishi yaliyopo kwenye ukuta wa biashara.
- Kwa ufahamu wetu tozo hili linahusu maeneo yote ya manispaa kama barabarani maeneo ya wazi ukuta wa uwanja wa ilulu na mengineyo yasiyohusu viwanja vya watu ndio yanayostahili kwani ni matakwa ya mfanya biashara kutangaza biashara yake katika maoneo hayo.
- Ukuta wa nyuma ni miliki ya mtu na haistahili kuingiliwa utaratibu wa nyumba yake ama bango lililopo kwenye eneo la ndani ya mipaka yake.
5. Bei kubwa kwa Mashine za kutolea stakabadhi TRA
- Utaratibu wa kuwataka wafanyabiashara kununua mashine za kutolea risiti umekuwa tatizo kutokana na bei za machine, na gharama za matengenezo jukumu analobebeshwa mfanyabiashara. TRA walitakiwa kutumia busara kwa machine hizi kuagiza wao wenyewe na kugawa kwa wafanyabiashara kwa kutumia mawakala kunawagandamiza wafanyabiashara kwa kuwatoza bei kubwa.
- Watumishi wa TRA wamekuwa wakipita maeneo ya wafanya biashara na kuwabainishia makosa na kuwalipisha faini. Hata hivyo huwataka watu hao kwenda katika ofisi za TRA na kujadiliana kuhusu malipo cha jambo ambalo linatia mashaka kwa uhakika wa makosa na taratibu zinazotumika kama ndio sahihi.
- Suala la Wafanyabiashara kukosa uelewa wa mambo mengi yanayohusu kodi na ushuru mbalimbali inahisiwa kutumiwa vibaya na baadhi ya watendaji wa taasisi hizo kwa wafanyabiashara.
- Wafanyabiashara kutakiwa kuwasilisha hesabu kwa ajili ya makadirio linahitajika kuangaliwa ukubwa wa biashara, na uzalishaji wa faida kwenye biashara husika, kwani mtayarishaji wa hesabu mara nyingi hudai kiwango kikubwa kupita kazi hiyo hata kodi utayokadiriwa huenda ikawa ndogo kuliko malipo hayo, jambo ambalo linachangia kupunguza uwezo wa kufanya biashara
6. Kupanda kwa gharama za Idara ya vipimo.
Upo utaratibu unaofahamika wa kaguzi za mizani wa kila mwaka unofanywa na watendaji wa idara ya vipimo.Utaratibu huu hauna mashaka unakubalika isipokuwa kwa yafuatayo.
- Bei zimepanda kufikia sh 18,000/= kwa mizani ndogo na 65,000/= kwa mizani kubwa. Upo utaratibu unautumika wa kuwalipisha wafanya biashara gharama za usafiri wanaotumia iwapo watatumia usafiri binafsi kumtaka mfanya biashara husika alipe.
- Katika utendaji wao upo utaratibu wa mkaguzi tofauti na mrekebishaji na gharama za kugonga mawe ni tofauti kwa kila jiwe la mizani.
7. Kodi ya majengo kwa wafanyabiashara
- Manispaa imekuwa imegeuzwa kodi ya majengo Property tax Badala ya kuwa kodi ya jengo inakuwa kodi ya mlango wa biashara.
- Kodi hiyo badala ya kumlenga mmiliki wa jengo sasa inageuka kuwa ya mfanya biashara kwani mmiliki wa jengo hudai haimuhusu kwa vile isingetokea bali ni kwa ajili ya biashara.
8. Wafanyabiashara/jamii kulazimishwa kusafisha mifereji ya Halmashauri
- Kumekuwa na utaratibu wa kulazimishwa kuzisafisha mfereji uliopo mbele yako hata kama biashara hiyo haizalishi taka.
- Baadhi ya Watendaji wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakishirikiana na mabwana afya kuwalazimisha wale wanaopakana na mifereji kusafisha kwa lazima na wasipofanya huwachukulia hatua. Kwa uelewa wa watu ni kuwa mipaka ya mmiliki wa jengo ni eneo lake la kiwanja na mfereji ni sehemu ya Halmashauri isipokuwa kama kuna mfereji uliopita chini ya jengo. Manispaa imeweka utaratibu wa vikundi vya kufanya usafi mitaani na kutoza kiwango cha shs 1000 hadi shs 2000 kwa mwezi kwa kila eneo la biashara ama nyumba. Utaratibu huu ni mzuri ila watendaji wanaamua kuacha kufanya kazi hiyo kwa vile wanalazimishwa kiwango wanachokusanya wanatakiwa wakiwakilishe manispaa na baadae walipwe wao.
9. Tozo kubwa kwenye bidhaa za maliasili
- Idara ya maliasili imepandisha ushuru wa bidha za mbao kwa kiwango kikubwa hali iliyopelekea mafundi seremala kukosa kazi za kufanya
Mfano : Tozo la kusajili kutumia mazao ya misitu imepanda kutoka shs 305,000/= hadi 389,000/=
- Ushuru wa kusafirisha samani umepanda kwa viwango vifuatavyo
a) Top ya mlango kutoka shs 6,500 hadi shs 101,000/=
b) Frem ya dirisha kutoka shs 4,300/= hadi shs 55,000/=
c) Kitanda kutoka shs 10,000/= hadi shs 131,000/=
10. Ushuru kwa huduma za TFDA
- Watumishi wa TFDA wamekuwa na utaratibu wa kawaida ya ukaguzi wa maeneo ya biashara za vyakula. Katika ukaguzi wao hupatikana mambo yafuatayo.
a) Hutoza malipo ya ukaguzi shs 46,000/=
b) Iwapo watapata bidhaa zisizostahili kutumika utalipa posho ya shs 30,000/= kwa kila mtumishi aliyopo.
c) Utalipia gharama za usfiri wa kuharibu vifaa hivyo
d) Utalipia gharama za mafuta ya taa kwa ajili ya kuchoma bidhaa hiyo
Iwapo msafara huo ni wa watumishi iweje ugharimie posho na kama watapita maeneo 20 kwa kutwa moja watakuwa na kiasi gani wanachopata.