Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA KUMI NA TATU
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SITAISAHAU facebook MTUNZI: Emmy John P. MAWASILIANO: 0654 960040 SEHEMU YA KUMI NA TATU Nililitazama tumbo langu dogo kisha nikafumba macho...

clip_image002SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI NA TATU
Nililitazama tumbo langu dogo kisha nikafumba macho na kujenga picha jinsi litakavyokuwa siku za usoni. Tumbo kubwa kabisa na kila mmoja ataliona. Aibu kubwa! Halafu pia nitachekesha kiasi fulani, nilivyokuwa cha ufupi halafu na tumbo kubwa?? Fedheha.
Kama hiyo haitoshi itafikia kipindi nitaugulia uchungu na hatimaye nitajifungua. Mtoto wa nani huyu? Nilijiuliza bila kupata jawabu sahihi. Sikutaka kujipatia jibu la gogo.
Mawazo yakaniumiza kichwa nikameza dawa za kutuliza maumivu. Nikasinzia!
Asubuhi nikashtuka kutoka usingizini. Tatizo lilelile haikuwa ndoto, nilikuwa na mimba. Nikawaza na kuwazua bado hapakupatikana jibu sahihi. Nikajaribu kupuuzia lakini suala hili liliniumiza kichwa.
Sasa nikakumbuka kuwa nilikuwa na pesa za kutosha katika akaunti yangu. Sasa kwa nini niendelee kuhangaika kiasi hiki. Ina maana pesa haiwezi kutatua tatizo hili.
Nikafikiria kugawana pesa zangu na mganga mwingine wa jadi. Lakini huyu sikutaka awe anatokea hapa Tanzania. Nilihitaji mganga
mwingine kabisa kutoka nje ya nchi.
Sikumshirikisha Maria, maana angegundua kuwa nina mimba. Hili nililiepuka sana.
Kimya kimya nikampata mganga. Alijitambulisha kuwa anatokea Naijeria. Huyu alikuwa ananifaa.
Nikamfungia safari! Alikuwa amejiundia ofisi yake nje kidogo ya jiji la Mwanza, maeneo ya Shamaliwa kata ya Igoma.
Nyumba yake ilikuwa nzuri sana, tofauti na wale waganga waliotangulia ambao walikuwa wakiishi katika vibanda vya nyasi huku wakiwa mabingwa wa kuomba kuku na mbuzi kama njia ya kutibu tatizo.
Huyu alikuwa katika nyumba nzuri sana. Huenda na tiba yake ilikuwa nzuri.
Nilipokelewa vyema na kuandikisha jina langu getini. Nikafikishwa ofisini kwake. Na penyewe palivutia sana.
Alikuwa anaye mkarimani wa kumsaidia kuweza kuwasiliana na wateja wasiojua kiingereza. Mimi sikuhitaji mfasiri nilikuwa najua kiingereza hivyo tulizungumza moja kwa moja.
Alinisikiliza kwa makini, miwani yake machoni. Kisha akaanza naye kunipa maelekezo.
Alitoa maelekezo mengi. Mwisho akaniambia nirejee usiku wa saa mbili aweze kunipatia tiba. Wakati huo ilikuwa saa kumi na moja jioni.
Saa mbili nilikuwa kwa mganga tena. Sasa alinipeleka mahali anapotolea tiba.
“Una mimba ya jini..jini la hatari..na ukilitoa kwa njia ya kuzaa.UTAKUFA! hakika UTAKUFA!” Alizungumza kwa msisitizo. Nikatetemeka kusikia suala la kufa.
“Hongera umewahi sana..bado halijakomaa. Sasa unatakiwa ulitoe sasa hivi. Linatakiwa kutoka.”
“Nitoe!.” Nilijikuta najibu huku ninatetemeka. Akacheka.
“Vua nguo zako zote.” Alitoa maelekezo.
Nikasita, akacheka tena. Kisha akanitazama.
“Toa nguo zako!!.” Aliamuru kwa kiingereza chake chenye lafudhi ya Afrika magharibi. Alikuwa mweusi tii.
Nikasalimu amri, mtaalamu huyu ndiye aliyekuwa ameshika mpini nami mikono yangu kwenye makali. Yeye mshindi.
Nikasaula moja baada ya nyingine. Nikaacha chupi. Akakoroma huku akitetemeka. Nikaiondoa na hiyo iliyobaki. Sasa nijizibe wapi? Juu ama chini nikakosa maamuzi.
Nikabaki katika mfadhaiko!.
“Lala hapo kitandani!” aliamuru. Nikajilaza kitanda cha futi sita kwa sita chenye shuka jeupe kabisa.
Mara taa ikazimwa. Giza likatawala. Kimya nacho kikatanda. Sauti ya mganga pekee akiunguruma kwa sauti ya chini ndiyo ilisikika. Mimi hofu tupu!
Mara kitandani tukawa wawili. Mikono ikinipapasa. Tiba gani hii! Nilishangaa lakini sikuuliza.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida nikapatwa na kiu kikali sana ghafla. Kiu kilichokausha koo langu kabisa.
“Thirsty (kiu)….” Nilinong’ona, mganga hakujibu. Nikajaribu tena kunong’ona sauti haikutoka. Lakini sikuwa katika uhitaji wa maji ya kunywa. Kuna kitu cha ziada nilikuwa nahitaji, sijui ni kitu gani sijui!! Lakini nilikuwa nahitaji.
Mikono niliendelea kunipapasa. Sasa hakuwa anaunguruma tena lakini alikuwa anahema juu juu sana. Huku napapaswa huku nahisi kiu cha ajabu.
Mara yule mganga akafika kifuani akaendelea kunishambulia. Kuja kutanabai alikuwa yu uchi! Hofu ya kubakwa ikanikumba. Nikajaribu kupiga kelele. Sauti haikutoka. Nikajaribu kumsukuma, alikuwa mzito kupita kiasi. Alikuwa na uzito kama lile gogo la usiku ule. Gogo lililonitia mimba. Kiu kikanifadhaisha na sasa sikuweza kujizuia zaidi nilitakiwa kupata kinywaji. Lakini sio maji wala soda.
Mganga akazidi kunikumbatia. Nikafanya jaribio la kumn’gata ili asitimize kitendo chake cha kunibaka. Maajabu!! Ile ladha ya chumvichumvi la jasho ikanipendeza, nikaitamani na nikazidi kumng’ata, damu! Damu ikaanza kumtoka, sikutaka hata tone moja linipite kando. Alijirusha rusha lakini sikubanduka. Hadi pale kiu kiliponiisha.
Wakati kiu kinaisha na yeye alikuwa ametulia tuli!
Nimekunywa damu ya mwanadamu!! Nilighafirika. Nikasimama wima huku nikiwa siamini kabisa kilichotokea pale ndani. Nikatapatapa katika giza mara nikabonyeza bila kutarajia kitufe. Taa ikawaka!
Macho yangu ana kwa ana na dude kubwa jeusi. Asili yake Naijeria likiwa limetulia kitandani. Shuka nyeupe sana bila hata tone la damu.
Dude lile lilikuwa uchi wa mnyama. Lilitia kinyaa kulitazama maungo yake.
Nikajifuta midomo nikaitazama. Hapakuwa na damu!! Na sikuwa na kiu tena. Kumbukumbu za kumshambulia yule mganga wa jadi zilikuwepo akilini na pia tukio la kumnyonya shingoni lilikuwa linaishi katika akili yangu. Sasa mbona hakuna damu. Mbona mashuka hayajachafuka.
Nikavaa nguo zangu huku nikiziona dalili za kufa mbele yangu.
Nikamtikisa yule daktari pale kitandani. Hakuamka. Na alidumu hivyo hadi nilipotoka. Hatua kwa hatua. Hadi nikatoka nje, hofu ikiwa inaniadhibu.
Sikusimama sana barabarani nikapata taksi.
“Nyegezi kona.”
“Nyegezi?” aliniuliza. Nikakubali.
Akawasha gari tukaondoka. Sikutaka kuzungumza lolote. Nilikuwa najiuliza ni kipi kinanitokea mfululizo kiasi hicho.
Simu yangu ikaita. Nikaitoa nikiamini ni Maria. Hakuwa yeye alikuwa Dokta Davis.
Nikachelewa kupokea. Ikawa imekatika.
Nikategemea atapiga tena! Hakupiga badala yake akatuma ujumbe.,
“Nakutakia usiku mwema!”
Sikumjibu.
****
Amani ikatoweka kabisa moyoni mwangu. Sikuyafurahia maisha yangu ya chuo. Sikuifurahia tena kazi niliyopewa na dokta Davis na kampuni yake.
Nikiwa nimejaribu kwa waganga na kushindwa kupata msaada wowote. Na sikuwa nikiamini sana ulokole na imani za uponyaji sasa niliamua LIWALO NA LIWE. Nitailea mimba yangu hadi nitakapojifungua.
Lakini nitakuwa na amani sana iwapo sitakuwa nachangamana na makundi ya watu. Na ili nisichangamane basi nilitakiwa kuiachia kazi niliyokuwa nimeipata. Kazi yenye kipato kizuri kabisa.
Nikatokwa na machozi nilipofikiria kuandika barua ya kuacha kazi!! Roho iliniuma sana.
“Na chozi langu likuangukie wewe uliyeniletea makwazo haya!!” nilitamka hayo wakati naweka nukta ya mwisho ya barua ile ya kumweleza Davis na kampuni yangu nia ya kuachana na kazi yao.
Sikuweza kuwaelezea kuwa nilikuwa na mimba. Niliwaambia shule imenibana sana na utendaji wangu kimasomo ulikuwa umeshuka sana.
Nikaituma kwa njia ya barua pepe kwenda kwa Dokta Davis.
Barua ikawa imefika!
Nikayasubiri majibu.
Zile milioni milioni ziliniuma sana kuziacha ziende mbali nami.
Lakini sikuwa na ujanja.
Laana na zitue kwa mbaya wangu iwapo yupo popote pele!!
****
Zilipita siku nne, kila siku nilikuwa napitia barua pepe yangu kutazama kama kuna majibu yoyote kutoka kwa Dokta Davis lakini mambo yalikuwa tofauti Davis hakupiga simu wala hakujibu ujumbe niliomtumia. Nilijiuliza je? Nimpigie simu ama niendelee kuvuta subira. Hali hiyo ya kungoja sana ikanitia mashaka, kumpigia simu pia nikasita kwa kukumbwa na maswali mengi. Kama hajaisoma ile e-mail itakuwaje? Na kama ameisoma pia nilitegemea maswali mchanganyiko ambayo yangeweza kunitia katika majaribu ya kumweleza Davis juu ya ile mimba ya kimaajabu! Jambo ambalo sikutaka kabisa litokee.
Nikaendelea kuwa kimya!
Siku zikasonga mbele. Amani finyu moyoni! Maria sasa akawa kama ndugu yangu, tuliendelea kuishi wote.
*****
Zilipokatika siku saba za kuikamilisha wiki moja, ustahimilivu ukanishinda, mateso ya nafsi yakanikita. Ujasiri ukaikimbia subira.
Nikaamua kujaribu kupeleleza, kwanini? Davis hadi sasa hajasema neno.
Sijui kwanini nilikuwa namuogopa Davis kwa kipindi hicho. Lakini sikuweza kumpigia simu.
Nifanyeje? Nilijiuliza!
Facebook! Jina hilo likanivamia kama jinamizi linalotisha lakini lenye msaada.
Kwanini naogopa? Nilijiuliza.
Ilikuwa saa moja usiku, nikiwa kitandani. Mkononi glasi ya juisi, kompyuta yangu ndogo ikiwa inamalizia hatua za kuwaka. Ilipomaliza, nikaingia katika mtandao. Tangu nitingwe na kazi niliyopewa na kampuni ya Dokta Davis na matatizo yaliyokuja baadaye nilikuwa nimeususa kabisa mtandao wa kijamii wa facebook, kwanza jina langu tayari lilikuwa kubwa pale chuoni hivyo nilikuwa napata usumbufu mtandaoni, pili sikuwa na muda kuingia kule mara kwa mara. Lakini siku hii nililazimika kuingia mtandaoni.
Nia kubwa ikiwa kutazama akaunti ya Dokta, ni lini mara ya mwisho kuandika kitu mtandaoni. Kama ningejua hilo ningeweza kuhusisha hofu yangu ya kwamba aidha kuna jambo baya limemkumba Davis.
Mdomo ukabaki wazi, nikapumbazwa na picha iliyokuwa katika akaunti yangu! Nikaitazama kwa makini! Haikuwa ndoto! Alikuwa yeye! Sasa ni lini ameiweka hapa? Nilijiuliza!
Nikataka kumuita Maria, nikagundua hatakuwa na la kunisaidia. Kwanza ye mwenyewe hana hulka na mtandao huu!
Nikabaki kuishangaa picha ya John! Alikuwa anatabasamu!
John alizipata wapi namba zangu za siri za akaunti yangu ya facebook? Nilijiuliza bila kupata majibu.
Mh! Au hii picha niliweka mwenyewe? Lini sasa? Nikajiuliza.
Kwa hili sikushtuka sana. Nikajipa moyo kuwa huenda niliwahi kuiweka hii picha ya John bila kujitambua kutokana na kukolea katika penzi. Penzi la John ambaye hadi wakati huu hakuwa akifahamika ni wapi alipo. Nikiwa nimeamua kumpuuzia John na hiyo picha sasa nikaamua kuendelea na kile kilichonifanya niingie mtandaoni.
Nikataka kuifungua akaunti ya Dokta Davis niweze kuikagua.
Hata kabla sijaanza kuikagua akaunti ya Dotka, nikakutana na kitu kingine cha kushangaza, hapa sasa nilijikuta naitupa laptop na kuruka mbali nayo kama nimepigwa shoti ya umeme. Ama nimeona kitu cha kushtua sana.
Ilikuwa picha nyingine, hii ilikuwa ina ujumbe juu yake 'In love with the guy!' marafiki zangu walikuwa wameishambulia kwa maoni, wengi wao wakisifia picha hiyo, huyu kwenye picha naye alikuwa anatabasamu, tofauti ya picha hizi ni kwamba John alikuwa amevaa fulana yake, lakini huyu mwingine alikuwa kifua wazi.
Kwa mtazamo wangu hii picha ilikuwa picha mbovu, isiyokuwa na mvuto. Hasa hasa kwangu ambaye hadi kumsifia mvulana amependeza lazima nichunguze vitu vingi, sasa kati ya hizo sifa huyu hakuwanayo hata moja.
Huyu hakuwa mwingine alikuwa ni yule mganga wa kinaijeria. Kamwe nisingeweza kumsahau maana nilimuona kwenye mwanga huku lile tukio la kujaribu kunibaka kisha akatulia tuli kitandani na lenyewe lilikuwa limenasa katika kichwa changu.
Tatizo!!
Bado nilikuwa wima natetemeka huku nikiiogopa ile laptop.
Nani ameingia kwenye akaunti yangu na kufanya haya?
Ujanja wa mtu muoga ni kukimbia shari. Palepale nikaitumia kanuni ile. Nikatimua mbio nikapishana na Maria alikuwa amekamata glasi iliyokuwa na juisi nikamsukuama yeye na glasi yake.
Yeye akawahi kujizuia lakini glasi ikasambaratika vipande. Nikamsikia akitoa yowe la hofu!

***ISABELA amefyonza damu ya mtu katika hali ya kustaajabisha……mauzauza yanamsababisha aombe kuacha kazi…barua haijibiwa mauzauza yanazidi……
****Sasa ni katika mtandao tena anakutana na picha ya yule mganga wa kinaijeria….HOFU…

ITAENDELEA……!!!!!

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top