SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Taarifa ile kila mmoja kati yangu na huyo rafiki yangu tulipokea kimshtuko. Hasahasa mimi. Nilijiuliza kwa nini? Sikupata jibu.
Maisha yakaendelea!!
Hapakuwa na mauzauza tena. Na kizuri zaidi hatimaye mama alizinduka kutoka katika usingizi ule wa kifo. Suzi akajivutia kwake kwamba ni maombi yamemwamsha, mimi sikuwa na lolote la kusema.
Mama hakuwa na kumbukumbu yoyote ile, alibaki kushangaa shangaa tu. Kwetu ilikuwa siku ya furaha sana. furaha iliyopitiliza. Sasa mama aliweza kula peke yake na hakuhitaji msaada tena. Walau furaha yangu ikarejea huku nikisahau kuhusu imani za kishirikina na kuamini mama alikuwa katika ugonjwa wa kawaida tu!!
Sasa vipi kuhusu John na ile ndoto niliyoiota? Nilijiuliza. Maana mama alikuwa amezinduka lakini John bado hakuonekana. Chuo kilishindwa kusema lolote maana mwanafunzi wa chuo kikuu anachukuliwa kama mtu mzima hakuna anayemlinda, hakuna uzio uliowekwa kumzuia asitoke, hivyo maisha ya mwanafunzi wa chuo yapo mikononi mwa msomaji mwenyewe. Chuo kitasema nini kuhusu kutoweka kwa John!! Ajabu ni kwamba hakutoweka katika mazingira yoyote yanayoelezeka bali ni ghafla tu akagundulika kuwa hayupo chuo
Nami nikaichukulia ile taarifa kama ilivyo. Kwanza upendo wangu kwa John ulikuwa umepoa sana. nilikuwa nimeanza kuhisi kuwa huyu si mtu mzuri kwangu.
****
(MIMBA YA MAAJABU)
Baada ya siku tatu. Mama akiandamana na dada yangu Suzi walirejea Makambako. Kama kawaida pesa ilikuwepo. Kwa nini sasa mama yangu asipate jambo la kukumbukwa maishani. Na Suzi naye apate la kujitambia kwa walokole wenzake. Nikawapandisha ndege. Sasa nikabaki kuishi peke yangu tena!! Sikuwa na uoga mkubwa japo sikumruhusu rafiki yangu huyu kuondoka. Tukaendelea kuishi wote.
Usiku huu ambao mama yangu alikuwa ametoweka nilikumbwa na hisia ama jambo la ajabu katika mwili wangu.
Kichwa kilikuwa kinauma, nilijaribu kumeza dawa lakini hazikunisaidia sana zaidi ya kuniweka katika majaribu ya kupitiwa na usingizi.
“Maria!! Mi nalala shosti.” Nilimwambia rafiki yangu. Aliyekuwa amejikita katika kuangalia filamu. Hivyo hakuitilia maanani sana taarifa yangu.
Mguu na njia nikakivamia kitanda nikaanza kuutafuta usingizi. Mara hizo hisia za kuumwa kichwa zikatoweka. Nikawa katika hisia nyingine zinazokera. Nikaanza kumkumbuka sana John . nikaukumbuka usiku ule mimi na yeye katika hoteli ya kifahari. Nikakumbuka pia jinsi nilivyoanza kuishi naye kama mchumba wangu. Mara nikayakumbuka mapenzi yake.
Ni hapa sasa nikaanza kuhangaika!! Nilikuwa namuhitaji John.
Nilikuwa nahitaji awe nami kitandani!! Lakini hakuwepo.
Nilitaka kujilazimisha kuamka niweze kukabiliana na hisia hizi lakini sikuweza. Nikahisi macho mazito sana!!
Mara likawa giza nene!! Kisha ndani ya sekunde kadhaa nikajihisi kama nina mikono ya ziada najipapasa. Mh!! Nikataka kufumbua macho bado yalikuwa mazito.
*****
Nilikuwa nimejilaza na kanga niliyokuwa nimeivaa wakati naandaa chakula. Ile mikono ya ziada nikawa naisikia kabisa ikiiondoa bila idhini ya akili yangu!! Nikajilazimisha kuamka. Sikuweza. Sasa nilikuwa sina nguo mwilini.
Kisha ile hali ya kumkumbuka John ikazidi. Nikawa katika kuhitaji huduma fulani hivi ambayo ni John pekee aliweza kunitimizia.
Penzi……..
Sikuchukua muda mrefu nikapata kile ninachokitamani. Lakini lilikuwa kama gogo limeniangukia kifuani. Nikaanza kupalangana kulitoa. Pumzi zikazidi kuniishia lile gogo halikutoka kifuani kwangu.
Sijui kama zilikuwa dalili za kufa ama vipi.
Jamani nakufaaa! Nilipiga mayowe. Sijui kama sauti ilikuwa inatoka ama la! Hofu ya kifo ikanitawala.
“He!! We naye unalala uchi? Kulikoni leo?” Niliisikia sauti ikiniuliza. Nikadhani bado nina lile gogo kifuani. Nikanyanyuka kwa nguvu sana. Maria alikuwa akitazamana nami uso kwa uso. Alinishangaa nami nikamshangaa.
“Unaota wewe!”
“Kwani kuna nini?” Nilimuuliza huku nikijishangaa kweli nipo kitandani, uchi kabisa. Halikuwepo lile gogo pale kitandani.
Wasiwasi ukatanda!
“Kweli ni ndoto..ndoto mbaya.” Nilimuunga mkono Maria.
Lakini sikuwa sahihi hata kidogo kuhisi ile ilikuwa ndoto!!
****
Kweli Haikuwa ndoto kama nilivyodhani na kujiaminisha kuwa ile kanga ilitoka bahati mbaya katika mwili wangu. Kichefuchefu na kukosa hamu ya kula vikaanza kuniandama, mara niwe nataka vyakula vichachu, mara nikivipata navichukia. Ile hali ikanifanya nihisi ninakaribia kuugua ama nina ugonjwa tayari. Mtu menye pesa kama mimi kwa nini niugue niendelee kukaa ndani wakati kuna hospitali zinaweza kunihudumia vyema.
Majuma matatu baada ya hali ile nikafikia uamuzi wa kwenda hospitali.
Sikumshirikisha Maria kwa sababu nilihisi ni jambo la kawaida sana. Nikajikokota hadi hospitali. Daktari akanipokea nikamueleza kila dalili inayonifanya nijihisi aidha nina malaria ama ugonjwa mwingine wowote ule. Sikuwaza hata kwa mbali majibu aliyoyatoa daktari.
Mimba!!! Una mimba Isabela, yalikuwa majibu
Sijui kama akili iliniruka name nikaruka nikamkunja daktari ama ni mizimu ilifanya hivyo. Sijui!!
Daktari akatapatapa akanitoa na kunituliza. Huku akisisitiza kuwa ninayo mimba. Na majibu hayo yapo sahihi. Alikuwa ameghadhabika kiasi.
Maajabu haya!! Nimeipatia wapi hiyo mimba.
Mimi ni muelimishaji wa mambo ya kimapenzi na mahusiano na jinsi ya kujilinda na magonjwa ya zinaa na mimba zisizotegemewa. Sasa nina mimba ya maajabu!! Anayeelimisha ameibeba…..
Nimshirikishe Maria? Nilijiuliza. Nikasita. Maria alikuwa mropokaji sana angeweza kunisambazia habari hiyo na heshima yangu ikashuka. Sikuwa tayari kuabika mbele ya maelfu ya wanafunzi anaoniheshimu sana.
Nikimueleza mama atanilaani!! Maana alikuwa akiniamini sana, bora basi angekuwepo John ningesema ni ya kwake.
Sasa hapa namsingizia nani?
Hapana sina mimba mimi!! Nilijikataa penye ukweli.
Nikaenda hospitali nyingine. Jibu lilikuwa MIMBA.
Akili ikahama, na nikaanza kuamini kumbe ule mtihani wa mama kupoteza fahamu ulikuwa mdogo sana. kumbe tatizo likikukumba wewe ndio utaugundua uzito wake.
Nikimbilie wapi Isabela mimi!!! Nilitaharuki.
Hisia zangu zikaenda kwenye lile gogo usiku ule. Nikajiona nimedhalilishwa kupewa mimba na gogo.
Tena ndotoni!! Chumbani kwangu.
Eeh!! Mungu nionee huruma mja wako. Nilikumbuka kumshirikisha sasa Mungu. Baada ya miezi kadhaa ya raha bila kufanya ibada.
*****
Dada yangu Suzi. Alikuwa ni mlokole lakini licha ya hayo yote alikuwa jasiri katika kutunza siri. Hili lilifahamika kwetu sote tangu tukiwa wadogo. Alitunza siri nyingi sana kifuani mwake. Siri za baba, siri za mama, zote alizibeba bila kuzitoa. Ama kwa hakika alikuwa mtu wa kipekee mwenye kifua haswa.
Nikamuona mlokole huyu ni mtu sahihi katika kumueleza linalonisibu.
Nikampigia simu tukapanga wakati tulivu kabisa wa kuzungumza.
Tukapendekeza iwe usiku. Mumewe akiwa ameingia kazini.
Usiku ukafika nikampigia simu.
Baada ya salamu za hapa na pale nikautua mzigo.
“Dada, yaliyonikuta ni makubwa mdogo wako…” nilianza kumuelezea mkasa ulivyokuwa huku nikisita kumshirikisha ukweli kuwa kuna ndoto ikiambatana na hisia ilinishika na nikahisi nafanya mapenzi ndotoni. Nilihofia ataleta ushauri wa kwenda kwa wachungaji feki kuombewa. Sikutaka kabisa kusikia mambo yake ya kilokole.
Nilipomaliza ukawa wakati wake kunishauri ama kusema lolote.
Kwa sauti tulivu tena iliyojaa unyenyekevu Suzi alianza kunieleza neno kwa neno.
Sasa nikaanza kutetemeka alipoyatamka haya. Nikaketi chini, mapigo ya moyo yakaongezeka kasi.
Nikatamani nife kwa muda. Kisha nikakumbuka kuwa nilikuwa naogopa kufa!!! Nikalipuuzia wazo hilo.
Wasiwasi ukazidi. Lakini Suzi alikuwa akiusema ukweli aliouficha moyoni kwa muda mrefu.
Suzi aliongea huku akitia msisitizo kwa aliyokuwa anayasema.
Ilikuwa ni historia ambayo sikuwahi kuisikia kamwe lakini sasa Suzi alikuwa ananifumbua macho. Uhusiano wa matukio alivyoupangilia ulinitia katika mashaka.
Wakati nampigia simu wazo langu kuu lilikuwa kuitoa ile mimba ambayo hata sikuwa na uelewa imeingia vipi katika mwili wangu. Nikamdanganya kuwa mpenzi wangu amenipachika lakini hatukuwa na mpango wa kupata mtoto katika kipindi hicho.
“Bela, Bela..usije ukathubutu kuitoa hiyo mimba!!! Usithubutu!!” alinikanya Suzi, hapo ni baada ya kunieleza kuwa kila msichana aliyethubutu kutoa mimba katika ukoo wetu alipoteza kizazi ama uhai.
Maneno hayo yaliambatana na mifano kadhaa ya ndugu zangu ambao hadi leo hii wanalilia watoto. Umri unakwenda na hakuna dalili ya mimba. Wengine wanaachika na kuolewa tena lakini hakuna mabadiliko. Wanabaki kuwa wapweke na kumshushia lawama Mungu. Kumbe kuna siri mioyoni mwao. Mimba zilizotolewa!!
Anti Rozi, mamdogo Sikujua, hao ni baadhi ya ndugu zangu waliokuwa wakinyanyasika katika ndoa zao kwa kuwa hawazai. Na kama na mimi ningethubutu basi ningekuwa katika mkondo huo.
Maneno hayo makali kutoka kwa bingwa wa kutunza siri yakanichoma haswaa.
Hapana!! Sipo tayari kudhalilishwa katika ndoa. Nilikiri.
Kwa maongezi yale kati yangu na dada Suzi ilimaanisha kuwa sikutakiwa kuitoa ile mimba! Mimba ya gogo! Isabela niende kuzaa gogo. Hapana!
Sasa ni kipi natakiwa kufanya hapa? Nilijiuliza bila kupata majibu. Ugumba sikuutaka na hata kuzaa na gogo n’do sikutaka kabisa kusikia.
Suzi akaniaga nikakata simu!!
Hofu kuu ilinitawala baada ya kuwa peke yangu tena. Bado nilikuwa nimeishikilia simu na nilikuwa natetemeka sana. Ni kama dunia ilikuwa imenigeukia na kunizomea baada ya kuwa imenivua nguo zote. Niliamini kuwa dunia ilikuwa inanionea. Haikuwa inanitendea haki hata kidogo. Kwa nini mimi kila siku, kwa nini wengine wanacheka, kilio kwangu tu kila siku? Mungu alikuwa ana upendeleo ama?
Nililitazama tumbo langu dogo kisha nikafumba macho na kujenga picha jinsi litakavyokuwa siku za usoni. Tumbo kubwa kabisa na kila mmoja ataliona. Aibu kubwa! Halafu pia nitachekesha kiasi fulani, nilivyokuwa cha ufupi halafu na tumbo kubwa?? Fedheha.
Kama hiyo haitoshi itafikia kipindi nitaugulia uchungu na hatimaye nitajifungua. Mtoto wa nani huyu? Nilijiuliza bila kupata jawabu sahihi. Sikutaka kujipatia jibu la gogo.
Mawazo yakaniumiza kichwa nikameza dawa za kutuliza maumivu. Nikasinzia!
Asubuhi nikashtuka kutoka usingizini. Tatizo lilelile haikuwa ndoto, nilikuwa na mimba. Nikawaza na kuwazua bado hapakupatikana jibu sahihi. Nikajaribu kupuuzia lakini suala hili liliniumiza kichwa.
Sasa nikakumbuka kuwa nilikuwa na pesa za kutosha katika akaunti yangu. Sasa kwa nini niendelee kuhangaika kiasi hiki. Ina maana pesa haiwezi kutatua tatizo hili.
Nikafikiria kugawana pesa zangu na mganga mwingine wa jadi. Lakini huyu sikutaka awe anatokea hapa Tanzania. Nilihitaji mganga
mwingine kabisa kutoka nje ya nchi.
Sikumshirikisha Maria, maana angegundua kuwa nina mimba. Hili nililiepuka sana.
Kimya kimya nikampata mganga. Alijitambulisha kuwa anatokea Naijeria. Huyu alikuwa ananifaa kutokana na umaarufu wao
Nikamfungia safari! Alikuwa amejiundia ofisi yake nje kidogo ya jiji la Mwanza, maeneo ya Shamaliwa kata ya Igoma.
Laity ungekuwa uwezo wangu ningeifanya safari ile iwe kama haijawahi kutokea maana!!!!!.......
***MAAJABU mengine makubwa kwa ISABELA…..Amebeba mimba anayohisi kuwa ni ya gogo….sasa inamtesa na kumkosesha amani…..dada SUZI anampa maneno makali ya ajabu zaidi…kuwa akithubutu kuitoa ni aidha atakufa ama la atapoteza kizazi….ISABELA hayupo tayari kwa yote mawili…….
***HATIMAYE anampata mganga kutoka NAIJERIA……anamfungia safari………..
JE MGANGA HUYU ATAMSAIDIA KWA LOLOTE………