RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA KUMI NA MOJA

clip_image002

SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John Pearson.
MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
John hapatikani nyumbani kwake masaa yamepita, mama yangu ana homa kali. Matukio haya yanayowiana yalinitia mashaka. Mama yangu amekufa! Niliwaza huku nikiichukia hali iliyonikumba. Sikujua ni uelekeo upi natakiwa kwenda, nilisimama chini ya mti nikaanza kuwapigia simu rafiki zake John, wote wakakiri kuonana na John lakini masaa kadhaa yaliyopita. Hakuna aliyemuona muda mfupi uliopita.
“Hakuwa na safari yoyote?” Nilimuuliza mmoja wao. Akapinga hoja hiyo. Nikazidi kuumia.
Nilirejea nyumbani kwangu nikiwa nimekata tamaa sana. sikuweza kulala wakati jina la mama likinishambulia kichwa changu.
Nilijaribu mara kwa mara kupiga simu ya John. Hali ikawa ileile.
Hatimaye nikafikia maamuzi binafsi. Nikaamua kurejea Makambako nikashuhudie tatizo gani limemsibu mama yangu.
Kama ilivyokuwa awali nikazungumza tena na kiongozi wa darasa kwa ajili ya kunitetea kwa lolote litakalotokea mimi nikiwa safarini.
Nikampatia kiasi kikubwa cha pesa ili kumshawishi zaidi. Akashawishika.
****
Ndege ndogo ya shirika la serikali ilitua katika uwanja mdogo wa ndege Iringa mjini uliojulikana kwa jina maarufu la Nduli. Nilitamani kushuka upesi upesi lakini ulikuwepo utaratibu wa kushuka. Mmoja baada ya mwingine.
Hali ile ya kupanda ndege mara kwa mara kama wengine wanavyofanya kwenye magari ilinifanya niamini kuwa pesa ndio kila kitu. Wachache wangeweza kuamini kuwa nilikuwa jijini Mwanza masaa yaliyopita kisha nikawa jijini Dar na sasa mjini Iringa. Lakini ilikuwa kweli kabisa!!!
Kitendo cha kusubiri basi kuelekea Makambako na chenyewe nilikiona ni cha kupoteza muda. Nikakodi gari aina ya Noah. Akataka kupandisha na abiria wengine nikamuonya kuwa sihitaji bughuza. Nikalipia pesa aliyohitaji!! Hakika nilikuwa na kiburi!!
“Mwendo mkali tafadhali! Lakini salama!!” nilimsihi.
Safari ikaanza. Baada ya kuwa nimemuelekeza mji niliokuwa naenda!!
Nani hakumjua mwalimu Nchimbi, hakuna ambaye hakumfahamu japo kwa jina basi alimjua na sura kabisa.
Mama alikuwa maarufu!! Umaarufu ambao sasa niliupuuzia maana haukuwa na faida zozote zile!! Umaarufu bila pesa!!!
Tukafika hatimaye nyumbani!! Hii ilikuwa baada ya dakika ishirini.
Hali ya mama ilikuwa mbaya zaidi ya homa ya kawaida aliyonielezea mdogo wangu kwenye simu. Ule muda waliokuwa wanashangaa nimefika vipi Iringa mimi niliutumia kumshangaa mama jinsi alivyokuwa anatokwa jasho huku akitetemeka. Alitokwa na vipele vya baridi na kuacha maswali kama anahisi baridi ama la! Maana wakati huo pia jasho lilimiminika.
Iringa na baridi lote lile mama anatokwa jasho na vipele vya baridi?? Ilitisha kutazama na kufikiria!!
“Mmeenda hospitali?.” Niliuliza swali langu la kwanza. Hakuna aliyenijibu. Nikawatazama nikingojea majibu.
Dada yangu mkubwa aitwaye Suzi akanijibu kuwa walikuwa na mpango huo. Nikatambua anamaanisha nini.
Upesi nikamwagiza mdogo wangu akaenda kuchukua teksi na baada ya muda kidogo mama alikuwa katika machela za akikimbizwa katika wodi ya wagonjwa mahututi. Hospitali ya Ilembula.
Madaktari walipima vipimo vyote. Kama nilivyotegemea.
Mama hakuwa na ugonjwa wowote. Lakini ajabu!! Alikuwa amezimia. Mama hakuwa akiongea. Cha kuduwaza hakuhitaji mashine za kumsaidia kupumua. Mama yangu nimpendaye kupita wanawake wote alikuwa anapumua mwenyewe.
Hali hii ilidumu siku ya kwanza, ya pili hadi ya tatu.
Baada ya siku nne tukashauriwa kumrejesha mama nyumbani kwani hapakuwa na namna yoyote katika hospitali ile..
Hatukuwa na ujanja tukarejea na mzigo wetu, akawa anahudumiwa chakula kwa njia za mipira akiwa nyumbani. Wakati dada na mdogo wangu wakijiuliza nini kimemsibu mama, nilibaki na siri nzito sana. niliamini kabisa tatizo hili la mama linahusiana kabisa na ile ndoto. Ndoto niliyoota mimi. Ndoto ya kushangaza!! Niliumia sana moyoni lakini sikutaka kuwakatisha tamaa ndugu zangu hao. Nikajifanya kulichukulia tatizo lile kama matatizo mengine ya kawaida.
Kwa hiyo John ni mchawi!!! Nilijiuliza huku nikizidia kuumia moyoni. Kama kweli ni mchawi basi huyu napambana naye kishirikina.
Dawa ya moto ni moto!! Nilijiapiza lakini sikuweza kumshirikisha yeyote kati ya dada ama mdogo wangu Helena.
Imani zao za kilokole zilipingana na matendo haya.
Nikaamua kufanya kimya kimya!! Ilimradi kuokoa maisha ya mama. Nilimpenda sana mama yangu nisikufiche msomaji, nilikuwa katika wakati mgumu wa maisha yangu!!
Kwa mara ya kwanza nikaingia katika kibanda kidogo cha mganga wa jadi. Nje nikalisoma bango akiwa anajisifia kuwa yeye ni bingwa katika Nyanja tofauti tofauti. Maandishi makubwa yakiwa juu ya Kutibu mapenzi na kuongeza nguvu za kiume!!
Nilijielezea tatizo langu. Akasema hilo ni tatizo dogo sana. akazungumza lugha alizozijua yeye. Akafoka sana hatimaye akaanza kucheka kama tahira vile. Mwisho akanipatia dawa na maelekezo.
Nikatimiza yote aliyohitaji lakini hakuna kilichobadilika.
Siku zilizidi kusogea, na kipindi cha mitihani kikajongea zaidi kule chuoni. Nikawa katika mitihani mingi kwa wakati mmoja.
Uamuzi wa mwisho niliofikia ni kuondoka na mama akiwa mgonjwa hivyo hivyo. Pia nikaondoka na dada yangu kwa ajili ya kumuhudumia.
Nyumbani akabaki mdogo wangu pamoja na baba chapombe!!
****
Nilikuwa na pesa na zilizidi kuongezeka lakini ajabu nilikuwa nakonda sana. si ugonjwa wa mama pekee ulionifanya kuwa hivyo bali ile ndoto ya John akishirikiana na Osmani kumchukua mama yangu katika namna ya kuumiza. Walikuwa wanambuluza chini. Sasa mama yupo hoi kitandani. Ajitambui. Na yeye John hajulikani alipo.
Maajabu!!
AFE AMA UKUBALIANE NA MIMI!! Niliukumbuka ujumbe huo, niliotumiwa siku chache kabla mambo hayajaharibika. Nikaanza kujiuliza ni kitu gani kilimaanishwa. Kisha nikaikumbuka ile namba +6666666. Haraka nikakimbia chumbani, nikachukua simu nikaingiza zile namba amabzo katika mtandao nilishindwa kabisa kupata jibu kuwa ni za nchi gani, hata nilivyopiga niliamini kuwa hazitaita!!.
Ajabu!! Simu ikaita lakini haikupokelewa. Nikajaribu tena na tena hali ikabaki kuwa kama ilivyo.
Wiki moja ilipita. Nilikuwa najilazimisha kwenda chuo.
Na siku hii ya maajabu pia nilikuwa nimeenda.
Lakini hali ya pale chuoni niliona kama hainifariji kabisa. Nikaamua kurejea nyumbani majira ya mchana walau nimuone mama yangu!! Ambaye aliendekea kula kwa kutumia njia za kitaalamu.
Nilipofika getini kabla ya kugonga nilisita. Kwa mbali nilisikia vurumai ikitokea ndani. Na hakuwepo mtu zaidi ya dada yangu pale ndani.
Au mama ameshtuka!! Nilijipa imani. Lakini haikudumu kwa muda mrefu. Mlango ukafunguliwa nikamwona mwanaume anatoka ndani.
Nikataharuki!!
Ina maana Suzi ameanza kuingiza wanaume hapa ndani!! Nilikisia kwa mashaka. Kisha nikaamua kuulinda ushahidi. Nikafungua geti nikutane na yule mwanaume nimuhoji kuwa yeye ni nani katika nyumba yangu.
Tayari nilikuwa nimekasirika.
Kwa mwendo wa upesi nikaingia ndani. Hatua za harakaharaka sasa nikawa nakabiliana na yule mwanaume. Tofauti na mategemeo yangu kuwa atashtuka. Aliunyanyua uso wake akanitazama. Nilitaka kukimbia lakini mwili ukawa dhaifu. Sijui kama alikuwa anajaribu kutabasamu au alikuwa anazomea.
Uso wake ulikuwa umevimba sana na ulikuwa umechubuka. Ni kama alikuwa amekwanguliwa kwa maksudi kabisa.
Mwanaume huyu wa ajabu akasimama wima akajaribu kuongea akashindwa akanielekeza kwa vitendo kama ananizuia vile kuingia nyumbani kwangu.
Kuna nini sasa!! Nilijiuliza.
Akazidi kunisisitiza kwa vitendo nisiingie. Hakuweza kutoa sauti.
Kabla hata sijajua nimjibu vipi kwa ishara alinyanyua miguu yake akaliendea geti akatoweka.
Akaniacha nikiwa katikati ya kuingia ndani ama kurejea getini. Hali yake usoni ilinitia mashaka sana, nilihisi na mimi nikiingia nitatoka kama yeye. Uoga ukatanda!!
Bado sikujua nifanye nini. Sikukumbuka hata kumpigia simu Suzi ambaye ni dada yangu. Nikaanza kunyata kuusogelea mlango, kisha nikaghairi nikaliendea geti nikalifungua likawa wazi kabisa.
Nikaufikia mlango nikataka kuufungua, roho ikawa inasita.
Niligundua kuwa nilikuwa natetemeka sana!! nikakishusha kitasa. Mara nikasikia vishindo vikisogea kwa kasi pale mlangoni. Mawazo yangu yakaenda moja kwa moja kwa kiumbe ambacho kimemtia majeraha yule bwana niliyepishana naye. Wacha weee!! Nikatimua mbio!
Nyuma vishindo vikaendelea kunifuata kimyakimya.
Ilikuwa vyema kwamba nililiacha geti wazi. Nikapenya na kuzidi kukimbia. Sasa mdomo ulifunguka nikaanza kupiga kelele kama chizi. Huku ninazidi kukimbia!!!
Nilipoweza kugeuza shingo kutazama nyuma. Kweli kilikuwa kiumbe cha ajabu!! Kiwiliwili kile kilikuwa kimevaa nguo za dada yangu. Suzi. Lakini usoni hakuwa Suzi. Huyu naye alikuwa ameumuka uso wake. Alikuwa anatisha. Nikiwa nimejikita mawazo yangu katika kumtathimini yule kiumbe anayenikimbiza mchana kweupe mara nikajikwaa.
Yule kiumbe naye akawa ananikaribia!!!
Maajabu yule kiumbe aliponifikia na yeye hakuwa akizungumza lolote kama yule. Ishara za vidole zikawa zinanielekeza jambo fulani. Sikuelewa lolote!! Cheni yake shingoni ikanifungua akili kuwa yule alikuwa ni dada yangu!! Lakini sasa amekuwaje.
Sikupata jibu umati ukawa umetuzunguka! Kila mtu akitaka kuhoji na kufahamu nini kimetokea. Suzi aliwashangaza wengi sana. Alikuwa amevimba na hakuweza kuzungumza lolote.
Kwa ishara hizohizo sasa akaanza kuwaelekeza washangaaji wengine wakamfuata. Baadhi wakiwa na silaha mikononi. Wanawake wakiwa nyuma nyuma…..na baada ya kuifikia nyumba kila mtu akawa anaogopa kuingia ndani ya nyumba yangu. Nyumba ambayo niliizindua kwa mbwembwe za hali ya juu.
Nilifadhaika.
Mwanaume mmoja aliyekuwa ameshikilia kisu tayari kwa lolote litakalokuja mbele yake aliingia ndani. Sisi tukabaki kushuhudia nini kitatokea. Suzi ambaye bado sura yake ilikuwa imeumuka alikuwa amejiweka mbali kabisa huku akionekana kutawaliwa na uoga.
“Mbona hamna kitu!!” Alizungumza yule mwanaume baada ya kutoka. Mmoja baada ya mwingine wakaanza kuingia katika nyumba yangu. Hakuna madhara waliyopata.
Suzi alikimbizwa hospitali. Baada ya siku tatu aliweza kuzungumza.
Kumbe yule mwanaume ambaye nilikutana naye siku ya tukio akiwa ameumuka usoni alikuwa ni kiongozi wa kiroho katika kanisa analolifahamu Suzi maana yeye ndiye alimleta kwa ajili ya kumfanyia maombi mama yangu mzazi.
Wakiwa katika maombi mara akaanza kiongozi wa kiroho kulalamika huku akiwa chini anagalagala hovyo. Hakuwa akinena kwa lugha lakini alikuwa akilia kwa kabila la kwao huku akimlaani paka aliyekuwa amemkaba koo huku akimshambulia.
Suzi alikuwa anashangaa tu mtu huyo akilia na kuomba msaada. Baadaye alitulia. Huo mda aliotulia tuli ndio ambao Suzi aliutumia kumsogelea. Dhahama ikahamia kwake!!
Sasa aliweza kumuona paka mkubwa rangi nyeusi!! Paka akamkwaruza kadri alivyoweza. Suzi alikimbilia chumbani lakini bado hakumkwepa paka huyu. Akakifunga chumba akidhani amemkimbia paka, mara akajikuta amejifungia chumba kimoja na yule paka mkubwa wa ajabu!! Mashambulizi yakaendelea!!
Wakati nafika na kuufungua mlango ndio wakati huo ambao paka alipotea na kumwacha Suzi ambaye alitimka mbio na kunikuta mimi nikiwa nimeanza kukimbia tayari.
Sasa alikuwa ameweza kuongea.
“Ajabu paka huyu hajamdhuru mgonjwa.” Suzi alishangaa. Nami nikashangaa zaidi. Paka hakuwa amemjeruhi mama hata kidogo!.
Simulizi hiyo ya Suzi iliniogopesha sana. nikamualika rafiki yangu Maria aishi nasi kwa muda. Wiki ya kwanza tangu afike pale. Mambo yalikuwa vizuri tu. Hapakuwa na mauzauza na michubuko katika paji la uso wa Suzi ilikuwa inafifia.
Jioni moja nilikuwa najisomea kwa maandalizi ya mitihani iliyokuwa imekaribia. Suzi ambaye hatukuwa tunasoma darasa moja alinikatisha kidogo. Akaleta maongezi yanayohusiana na imani za kishirikina juu ya kupote kwa John. Nilitega sikio nikamsikiliza kwa makini hadi akayamaliza maongezi yake.
“Ujue nini Bela hapa kuna mtu hawapendi anakufanyizieni” alizungumza huku akiwa amenikazia macho binti huyu wa kisukuma.
Kimya nikawa namsikiliza!!
“Na hapa ukilemaa wanampoteza na mama.” Alitamka maneno yaliyonishtua. Sasa hapo nikamtilia maanani. Ushauri wake wa mwisho akanisihi niende kwa mganga wa jadi kabla mama hajachukuliwa.
Kwa kuwa aliweka neno mama sikuwa na ujanja. Siku mbili baadaye nikaingia kwa mganga wa jadi kwa mara ya pili. Na yeye alikuwa na mbwembwe kama yule mganga wa Iringa.
Mara anikwangue kiganja mara anikwangue kichwani mzee huyu!! Mara aruke akitugeuzia matako, mara akatike midundo anayoijua yeye mwenyewe!!
Mimi kimyaa namsikiliza atasema nini baada ya onyesho lake hilo. Akaomba pesa akapewa.
Akatoa masharti yake!! Hayakuwa magumu sana. tukatii na kuondoka.
Alituomba turejee baada ya wiki moja. Kweli wiki ikaisha, Tuliporejea tukakuta matanga. Mganga mjanja mjanja hakuwa nasi tena duniani. Alikuwa amekufa!! Kifo cha ghafla. Siku moja baada ya sisi kuondoka pale.
Taarifa ile kila mmoja kati yangu na huyo rafiki yangu tulipokea kimshtuko. Hasahasa mimi. Nilijiuliza kwa nini? Sikupata jibu.
Maisha yakaendelea!!
Hapakuwa na mauzauza tena. Na kizuri zaidi hatimaye mama alizinduka kutoka katika usingizi ule wa kifo. Suzi akajivutia sifa kwake kwamba ni maombi yamemwamsha, mimi sikuwa na lolote la kusema. Nilitaka kumwazia mganga kuwa ndiye aliyetusaidia lakini lakini mbona amekufa tayari!!!
Sintofahamu!!
Mama hakuwa na kumbukumbu yoyote ile, alibaki kushangaa shangaa tu. Kwetu ilikuwa siku ya furaha sana. furaha iliyopitiliza. Sasa mama aliweza kula peke yake na hakuhitaji msaada tena. Walau furaha yangu ikarejea huku nikisahau kuhusu imani za kishirikina na kuamini mama alikuwa katika ugonjwa wa kawaida tu!!
Sasa vipi kuhusu John na ile ndoto niliyoiota? Nilijiuliza. Maana mama alikuwa amezinduka lakini John bado hakuonekana. Chuo kilishindwa kusema lolote maana mwanafunzi wa chuo kikuu anachukuliwa kama mtu mzima hakuna anayemlinda, hakuna uzio uliowekwa kumzuia asitoke, hivyo maisha ya mwanafunzi wa chuo yapo mikononi mwa msomaji mwenyewe. Chuo kitasema nini kuhusu kutoweka kwa John!! Ajabu ni kwamba hakutoweka katika mazingira yoyote yanayoelezeka bali ni ghafla tu akagundulika kuwa hayupo chuo
Nami nikaichukulia ile taarifa kama ilivyo. Kwanza upendo wangu kwa John ulikuwa umepoa sana. nilikuwa nimeanza kuhisi kuwa huyu si mtu mzuri kwangu.
****
Baada ya siku tatu. Mama akiandamana na dada yangu Suzi walirejea Makambako. Kama kawaida pesa ilikuwepo. Kwa nini sasa mama yangu asipate jambo la kukumbukwa maishani. Na Suzi naye apate la kujitambia kwa walokole wenzake. Nikawapandisha ndege. Sasa nikabaki kuishi peke yangu tena!! Sikuwa na uoga mkubwa japo sikumruhusu rafiki yangu huyu kuondoka. Tukaendelea kuishi wote.
Usiku huu ambao mama yangu alikuwa ametoweka nilikumbwa na hisia ama jambo la ajabu katika mwili wangu.
Kichwa kilikuwa kinauma, nilijaribu kumeza dawa lakini hazikunisaidia sana zaidi ya kuniweka katika majaribu ya kupitiwa na usingizi.
“Maria!! Mi nalala shosti.” Nilimwambia rafiki yangu. Yeye alikuwa amejikita katika kuangalia filamu. Hivyo hakuitilia maanani sana taarifa yangu.
Mguu na njia nikakivamia kitanda nikaanza kuutafuta usingizi. Mara hizo hisia za kuumwa kichwa zikatoweka. Nikawa katika hisia nyingine zinazokera. Nikaanza kumkumbuka sana John . nikaukumbuka usiku ule mimi na yeye katika hoteli ya kifahari. Nikakumbuka pia jinsi nilivyoanza kuishi naye kama mchumba wangu. Mara nikayakumbuka mapenzi yake.
Ni hapa sasa nikaanza kuhangaika!! Nilikuwa namuhitaji John.
Nilikuwa nahitaji awe nami kitandani!! Sio tu kuwa kitandani nilihitaji afanye kitu katika mwili wangu!!! Lakini hakuwepo.
Nilitaka kujilazimisha kuamka niweze kukabiliana na hisia hizi lakini sikuweza. Nikahisi macho mazito sana!!
Mara likawa giza nene!! Kisha ndani ya sekunde kadhaa nikajihisi kama nina mikono ya ziada najipapasa. Mh!! Nikataka kufumbua macho bado yalikuwa mazito. Lakini nilikuwa napapaswa jamani!!! Nani sasa ananipapasa!!
Mara kitu kizito kifuani!! Macho siwezi kufumbua na mpapaso unaendelea
*****

**Nini kinamtokea ISABELA usingizini….hisia hizi zinatoka wapi?? Na nani atazituliza???  Kaazi kwelikweli……….

ITAENDELEA KESHO!!!

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post