RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA TANO

clip_image001RIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: EMMY JOHN Pearson

SEHEMU YA TANO
(Mwanzo wa balaa)
Asubuhi palipopambazuka, taarifa ilikuwa nyingine, taarifa ya kushtua nafsi!! Jenipher msichana aliyekuwa akiishi na huyo rafiki aliyenipigia usiku uliopita.alikuwa amefariki baada ya jitihada za madaktari kugonga mwamba kumuokoa.
Ilikuwa habari ya kusikitisha sana kwani kilikuwa kifo cha ghafla mno. Mbaya zaidi alikuwa mtoto pekee katika familia yao. Huzuni kwa baba kilio kwa mama mzazi!!!
Sikuzikumbuka tena zile sauti za usiku ule zilikuwa zinasema nini na mimi. Sauti za furaha, Sasa nikawa nawaza juu ya msiba huo!! Msiba wa ghafla!!
Msiba wa Jenipher!!
Nilipowaza jina hilo mara nikakumbuka kama vile zile sauti zilitaja jina Jenipher!! Nilijitahidi kukumbuka palikuwa na maneno gani mengine kabla ya neno hilo Jenipher lakini sikuweza kukumbuka chochote. Nikajihisi kuwa huenda ni msiba unaivuruga akili yangu na kuwaza mambo na sauti zisizokuwepo.
Lakini mara mbili? Kwa nini niwaze mara mbili sasa!! Sauti za kihehe si kihehe, kibena si kibena!! Kazi kwelikweli lakini sauti hizi zimetja jina Jenipher…
Au ni ile sauti ya rafiki aliyenipigia mimi nachanganya na hizo sauti za kibena?? Nilijiuliza na kisha kuegemea katika pointi hiyo kama jibu sahihi!!!
Mwili wa marehemu uliagwa katika viwanja vya Raila Odinga. Kila aliyehudhuria alijawa na simanzi, hasahasa kutokana na kilio cha mama mzazi wa binti yule ambaye alikuwa haishi kumlilia mwanaye huyo wa pekee aliyefanikiwa walau kufika chuo kikuu.
Tofauti na watu kuwa na majonzi niliweza kubaini sura ya mtu mmoja ilikuwa na hofu kuu. Huzuni ikiwa mbali naye.
Huyu alikuwa ni John. Sikujua kwa nini alikuwa katika hali ile. Niliyalaumu macho yangu kwa kumtazama vile huenda alikuwa sawa lakini hapana nafsi haikuridhika. Maana siku tuliyokuwanaye hakuwa na hofu kabisa na uso wake ulitabasamu tu!!!
Muda wa kuaga ulifika ilianza familia ya marehemu iliyoungana nasi pale chuoni, kisha wakafuata wanafunzi wa kike. Nilinyanyuka na kuungana na msururu mrefu uliokuwa na nia moja ya kumsindikiza marehemu na kumuaga kwa mara ya mwisho kabla hajahifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Kaburi!!
Jua kali lilikuwa likinisumbua sana na kunifanya nitokwe jasho sana, si mimi pekee niliyelalamika bali na baadhi ya wasichana waliokuwa nyuma yangu nao walilalamika. Wale waliozidisha vipodozi, jasho liliwatoka na kuondoka na vipodozi vile huku wakibaki kuwa kama vinyago, Lakini mwendokasi wa foleni haukuwa mbaya tuliamini kuwa muda si mrefu kila mmoja atakuwa amemuaga marehemu kisha kila mmoja kushika hatamu yake.
Kwa akili zangu timamu nilisikia mivumo kwa mbali sana. Sikuwa nimesinzia ili nijilaumu kwamba ni ndoto. Hapana nilikuwa najitambua kabisa. Mivumo ile ilikuwa mithili ya mkutano wa injili unaofanyika mbali kiasi na wanatumia spika kubwa kuhamasisha watu wengi waweze kusikia. Kisha sauti hizo kutwaliwa na upepo kisha kurudishwa. Sikuweza kusikia maneno yote na hata hayo niliyoyasikia yalikuwa nusunusu. Nilitaka kumuuliza aliyekuwa mbele yangu lakini bahati mbaya hatukuwa tukifahamiana. Lakini wa nyuma yangu nilikuwa namfahamu nikaamua kumuuliza kama kuna kitu anasikia.
“Eti dada we unasikia nini?.” Nilimuuliza.
“Sijui hata kuna nini huko mbele hata dah!! Jua kali kweli. Najisikia kizunguzungu tu hapa” Alinijibu nje kabisa ya swali nililomuuliza. Nikameza mate kulainisha koo langu, alikuwa amenikera.
Ghafla nikagundua kuwa foleni ile ilisimama, sasa nikagundua kwa nini yule binti alinijibu vile. Kumbe hakunielewa kabisa.
Kimyakimya nikamsamehe!!!
Foleni ile haikuweza kusogea mbele, nilikuwa bado katika kutafakari, kulikoni ghafla ilitawanyika. Haikuwa foleni tena bali purukushani. Kila mmoja akataka kutazama kilichopo mbele. Mwanzoni ilikuwa foleni ya wasichana lakini sasa ulikuwa mchanganyiko wa jinsia zote. Kila mmoja akijitahidi kwa kadri anavyoweza kutazama mbele kuna nini.
Nilikuwa mmoja kati ya walioparangana na kufanikiwa kuona mbele. Alikuwa ni Jesca , aidha kwa hiari ama lazima alikuwa amekumbatia ardhi isiyokumbatika. Ardhi iliyotumika kama uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu!! Alikuwa ametulia tuli kumaanisha labda amekipenda kitendo kile. Tulibaki kushangaa kwamba kuna nini kimetokea. Wasichana tukiwa katika mshtuko wanaume walijiongeza wakavua mashati yao na kuanza kumpepea Jesca. John akiwa mstari wa mbele kumtetea huyu mpenzi wake kutoka katika hali aliyokuwanayo.
Niliweka kando hasira na chuki dhidi ya binti huyo ambaye kwa maksudi alininyang’anya tonge mdomoni kwa kumchukua mpenzi wangu John kutoka katika himaya yangu.
Niliuvaa ubinadamu, huruma ikanishika. Nikajiuliza nini kinatokea?? Zile sauti za mivumo hazikusikika tena!!!
Jesca hakutingishika hata kidogo. Sasa alibebwa mzega mzega hadi akawekwa katika kivuli. Zoezi la kumpepea liliendelea kwa bidii zote.
Yule mwanadada mwingine aliyekuwa ametulia tuli katika jeneza yeye alikuwa amesahauliwa kwa muda. Cha ajabu hata mama yake mzazi naye macho yake yalikuwa yakifuatilia kwa ukaribu tukio la Jesca kuanguka.
Sio maajabu haya!!!!
Harakati za kumpepea Jesca ziliendelea hadi gari ya huduma ya kwanza ilipofika eneo lile la Malimbe, Jesca alipakizwa na gari ikaondoka kwa kasi huku ikipiga ving’ora vya kuashiria hatari ama dharula.
Nilifanya ishara ya msalaba na kumkabidhi Jesca kwa Mungu kutokana na tatizo lililomsibu. Sikujua ni tatizo gani.
Zoezi la kuaga liliendelea tena upesi upesi. Wakati huu sikumuona tena John. Bila shaka aliongozana na mpenzi wake alyekuwa amekumbwa na maswahibu.
Ile kufikiria kuwa Jesca ni mpenzi wa John. Wivu ukanipiga kikumbo nikajisikia vibaya. Nikahisi kuwa naonewa. Kisha nikaukumbuka usiku wangu wa mwisho na John. Ulikuwa usiku wa kipekee….na…na……na usiku wa kwanza kusikia sauti zile zisizokuwa na maana. Sauti za maajabu.
Sasa zinamaanisha nini? Hilo lilikuwa swali. Nje kabisa ya uwezo wangu kujibu. Lakini nani hasa wa kunijibia????
Hakuwepo!!
Baada ya taatibu zote za kuuaga mwili kufanyika. Zilifuata taratibu za kifamilia. Kuondoka na mwili wao usiokuw na uhai tena!!.
Mwili ambao ulikuwa umeagizwa kuja kusoma kwa lengo la kuisaidia familia hapo baadaye mwili huu sasa ulikuwa unarejeshwa nyumbani kwa ajili ya kuzikwa. Inauma sana.
Baada ya watu kusambaa niliwasha simu yangu kwa ajili ya kumpigia John na kumjulia hali Jesca. Lakini kabla sijapiga, iliingia simu ya Dokta Davis. Nilishtuka kwanza, maana ile kazi niliyoagizwa hata siku moja nilikuwa sijaifanya. Nikaanza kutunga uongo kisha nikapokea simu.
“Pole sana na kazi!!! Usijali utazoea. Naona unachoka sana hata kupiga simu inakuwa tabu. Bila shaka ulifika salama na kazi uliianza mara moja." Aliongea bila kuweka kituo Dokta Davis. Nilibaki kujichekeshachekesha, kisha nikakiri kuwa kazi inaenda vizuri sana.
“Safi sana …safi sana.” Alinisifia Dokta. Nikajisikia vibaya kwa kuwa nimemdanganya mwanaume huyu wa kipekee.
Tulizungumza mengi huku akinisihi niangalie akaunti yangu maana kuna pesa ilikuwa imetangulizwa tayari na muhasibu wa kampuni yake.
Taarifa hiyo ilikuwa furaha sana kwangu. Kiukweli nilikuwa napenda sana pesa. Sio mimi pekee, naamini kila mwanadamu anaipenda pesa!! Ila tunapishana tu kipimo cha kupenda huko!!
Nilipotoka pale eneo la viwanja vya Raila Odinga nilijivuta taratibu hadi nikazifikia ATM, nikazama ndani nikadondosha kadi yangu. Nikatazamana na akaunti yangu ikiwa imekenua, kunifurahisha mimi. Milioni tatu, laki sita na elfu sitini na sita zilikuwa zimeongezeka katika akaunti yangu. Nilitabasamu mwenyewe, huku nikichomoa kadi yangu. Sikuwa na haja na pesa kwani kwenye pochi yangu laki moja na nusu ilikuwa inasubiri matumizi yangu.
Nilipokuwa natoka katika kituo hicho cha kujichotea pesa, nilijiuliza ni kivipi watu watatambua kuwa Isabela mimi nina pesa, nilitama wanijue ili niheshimike kila kona. Nilianza kuwaza kuhusu umaarufu. Wanafunzi mia nne wa darasani kwetu pekee kunifahamu hilo niliona kama halitoshi. Nilihitaji walau nusu ya chuo waweze kunifahamu vizuri. Sikupata muda wa kufikiria kuwa sifa haziliwi wala hazinenepeshi. Bali sifa ni mzigo wa miiba!!
Mawazo yangu hayo yasiyokuwa na maana sana yaliingiliana na mlio wa simu.
“Isije ikawa taarifa mbaya…” niliwaza.
Nikaipokea simu nimsikilize shemeji yangu alikuwa akisema nini. Huyu alikuwa ni rafiki yake na John.
“Pole shemeji yangu…” Aliniambia kwa sauti iliyokata tamaa.
“Mh!! Asante..bana ndo mipango ya Mungu.” Nilimjibu.
“Haya bwana mi ndio naelekea huko kumpa kampani mshikaji.”
Kumpa kampani mshkaji?? Mshkaji gani tena hapa. Nilijiuliza. Sikupata jibu simu ikawa imekatwa.
Baada ya dakika kadhaa nilikuwa katika taksi nikielekea maeneo ya Kijiweni ambayo ndio nilikuwa naishi. Hapakuwa na foleni kama kawaida hivyo baada ya dakika chache nilifika chumbani kwangu. Njaa ilikuwa imenishika, sikudumu sana pale ndani nilivua viatu vyangu vya kufunika na kuvaa vya wazi kisha nikatoka. Kuelekea kwenye mgahawa kupata chakula.
Nikiwa katika mgahawa niligundua kuwa kuna kitu napungukiwa
katika himaya yangu. Simu!!!
Nilikuwa nimeisahau kwenye pochi yangu.
Sikutilia maanani sana kwa kuwa tayari nilikuwa najua ni wapi ipo. Nilijikita katika kusubiri chakula huku nikifanya tathmini ya hapa na pale juu ya kazi ya kipekee hiyo niliyokuwa nimepata kutoka nchi za kigeni. Ilikuwa ni kazi moja ya kipekee sana iliyokuja katika maisha yangu wakati muafaka kabisa.
Nikiwa katika kuiwaza hiyo kazi, nikakumbuka ‘umaarufu’ na wenyewe pia nilikuwa nautaka kwa namna yoyote, siwezi kuimba muziki, sijui kuigiza. Sasa nitakuwaje maarufu!!!
Pesa, pesa ndio kila kitu. Pesa zitanipa umaarufu. Nikiwa kimya hivihivi kila mtu atajilinganisha na mimi wakati mimi nipo matawi mengine kabisa. Niliwaza hayo!!! Kisha nikajisikia hasira ikinivamia kwa kufikiria kuwa kila mtu atathubutu kujilinganisha na mimi.
Au nigombee uraisi wa chuo?? Nilijiuliza. Nikakatishwa na chakula kilicholetwa mbele yangu. Hivyo sikupata nafasi ya kutafakari majibu. Lakini niliuhitaji umaarufu.
Baada ya saa zima nilirejea chumbani. Moja kwa moja katika mkoba wangu. Simu ilikuwepo. Nikaitwaa nikajilaza kitandani.
Nikatazama kama kuna mtu alinipigia.
Yeah!! John alikuwa amepiga na wengine watatu, mama pia akiwemo. Nikawapanga katika orodha nianze na yupi. Niliamini nikianza na mama hatutamaliza maongezi maana tulikuwa na mengi ya kuzungumza.
Nikaamua kuanza na John. Nilipopiga simu ikawa inatumika, nikaamua kumpigia mama nizungumze naye wakati huo nangoja John amalize kuzungumza katika simu.
Tulizungumza mengi na mama yangu mpenzi huku akiniahidi kuwa siku inayofuata atanitumia shilingi elfu ishirini za kitanzania kwa ajili ya matumizi pale chuoni.
Kidogo nicheke kwa sauti kubwa lakini nikajibana kucheka.
Pesa ninayotumia kwa nauli ya siku moja, pesa ninayoitumia kwa mlo mmoja tu wa mchana na rafiki zangu wawili, leo hii mama anataka anitumie kwa ajili ya matumizi. Kichekesho!!!
Wakati naendelea kubadilishana mawazo ya hapa na pale mama. Simu ya John nayo ilianza kuingia. Nikamdanganya mama kuwa salio limeisha nikakata simu nikamtwangia John huku nikiwa bado nakitafakari kielfu ishirini cha mama.
John hakuwa anaongea, lakini nilisikia kwa mbali vilio vya kwikwi. Kuna nini? Nilijiuliza.
“Halo, halow…John.” Niliita sikujibiwa.
Niliendelea kumsikiliza, alikuwa kimya, nikakata nikampigia rafiki yake. Yeye alipokea upesi tu!!
“Vipi upo na John?”
“Nimeachana naye muda si mrefu, amechanganyikiwa kabisa.”
“Amechanganyikiwa? Kwa nini?.” Nilimuuliza kwa wasiwasi.
“Dah!! Yaani amezinguana na madaktari huko hospitali hataki
kuamini kabisa.”
Simu hii ilizidi kunichanganya. Nikajikadiria majibu yangu, ina maana John ana Ukimwi ama? Mungu wangu nimekwisha!!! Nilihamaki. Nikikumbuka usiku ule hatukutumia kinga!!
Suala la kusikia John, kuzinguana na madaktari, amechanganyikiwa. Utata!!!
Sasa na mimi nikaanza kuhaha, kana kwamba niliyoyawaza ni sahihi.
Upesi nikanunua muda wa maongezi nikampigia tena rafiki yake John. Nikamsihi anieleze nini kimetokea.
Bila kusita akaanza kunieleza. Mwishowe nikapata jibu kamili. John hakuwa ameathirika na UKIMWI bali mshtuko. Jesca aliyeanguka wakati wa kuaga mwili wa marehemu Jenipher viwanja vya Raila Odinga na yeye amefariki.
Cha ajabu na kushtua hakuna ugonjwa wowote uliohusika katika kifo hicho. Nilifadhaika nikakaa chini, sikukumbuka hata kuaga tayari nilikuwa nimekata simu.
Mbona hivi vifo vinakuja mfululizo kiasi hiki?? Nilijiuliza na hakuwepo timamu yeyote wa kunijibu. Kila nilipokumbuka vifo hivi nilikumbuka pia na maluweluwe ya sauti zile. Sauti za maajabu!!!
Jesca naye kama ilivyokuwa kwa aliyetangulia aliagwa na wanafunzi uwanja uleule wa Raila Odinga. Halikuwa jambo la kushangaza bali lilimezwa na huzuni. Haikuwa mara ya kwanza vifo kutokea katika maisha ya chuo, lakini hiki kifo cha Jesca kilikuwa cha ghafla mno. Iliuma sana!!!
John alizimia mara mbili!!!
****

***JESCA naye amekufa huku sauti zile zikisikika…kuna nini katika sauti hizi???
***ISABELA anawaza umaarufu!! Je itawezekana kuupata???
ITAENDELEA….!!!

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post