Unknown Unknown Author
Title: RAIS: WATANZANIA WAKAMLILIE NANI?
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete Na. Paschally Mayega RAIS wangu nilifarijika sana kusoma ujumbe niliotumiwa na...

clip_image002Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete

Na. Paschally Mayega

RAIS wangu nilifarijika sana kusoma ujumbe niliotumiwa na mwanamwema Ananilea Nkya. Najisikia kusukumwa na nafasi yangu kutaka na wanawema wengine wausome na hasa kwakuwa wengi walitaka kujua yuko wapi.

Aliniandikia hivi: “Mwanamwema Paschally. Nakushukuru. Hivi sasa niko masomoni.  Nimesoma makala yako.  Kama kawaida yako, kalamu yako ni kalamu iliyojaa maelekezo ya kujenga nchi yetu. Lakini nani anasoma? Walengwa wanasoma kweli? Ninaamini wangekuwa wanasoma makala zako zote, wangepata urahisi kuongoza nchi.

“Mungu aendelee kukutunza na kukupa fikra njema za kujenga nchi yetu. Kama ulivyosema katika makala yako, hakuna kukata tamaa.  Zaidi tuendelee kumlilia Mungu wetu aitizame nchi yetu kwa jicho la tofauti maana wanasiasa wetu  sina uhakika kama wengi wanajali tena hatma ya taifa hili na wananchi wake, wanachojali zaidi maslahi yao binafsi. Ananilea Nkya.”

Ndugu rais, wako wasomaji wengi mno ambao kila mara huniuliza kutaka kujua kama viongozi wetu wanasoma haya tunayoandika. Ni vigumu kujua kwa sababu ya umbali mkubwa uliopo kati ya viongozi wetu na sisi wananchi wao.

Wako baadhi ya viongozi wema husoma na wakati mwingine huuliza, huelekeza na hata kupongeza. Kama wananchi wako wanasoma halafu wewe kiongozi wao husomi hiyo ni kwa hasara yako mwenyewe.

Sitachoka kwa maana wanasema, Muomba Mungu hachoki. Kama baba hutanisikia, Mwenyezi Mungu atanisikia.

Rais wangu, Absalom Kibanda ametoka hospitalini. Amerudi nyumbani akitokea nchi ya mbali, nchi ya wageni. Huko alipelekwa akiwa mahututi, kutibiwa. Ameugua kwa miezi mitatu huku wazazi wake na ndugu zake wa karibu wakishindwa kumuuguza kutokana na umbali mkubwa uliopo kati ya Afrika Kusini na kwao.

Ugonjwa wake haukuwa wa bahati mbaya. Ulipangwa na kutekelezwa kinyama ili kuwathibitishia wana wa nchi hii uwepo wa ushetani ndani ya nchi yao. Shetani ni roho. Aingiapo nchini hupitia katika moyo wa mwanadamu mwovu. Atakayeuliza Kibanda ni nani jua huyo ni shetani.

Kibanda alipoikanyaga tena ardhi hii iliyowatoa wazazi wake, machozi yalimtoka. Machozi yake yakawatoa na wengine machozi mengi.

Kibanda alilia na wengine nao wakalia naye. Wanamlilia nani? Baba waonyeshe watu wa Mungu wamlilie nani? Mbona hata watoto yatima katika nchi hii wana wasamaria wema wanaowahurumia. Iweje kwa maskini wa nchi hii wakose hata wa kuwatazama tu kwa jicho la huruma? Hali hii itatisha hadi lini?

Kama walivyo waogopao uwepo wa Mungu, Kibanda aliwaambia waliokuwa wanamlilia akisema; “Nawaomba kwa sasa msinililie Kibanda, ililieni nchi yenu hii ambayo kwa karibu miaka nane ya utawala wa awamu ya nne matukio kama haya yamekuwa yakiendelea kufanyika bila hatua zozote kuchukuliwa.” Huzuni ya moyo uliopondekapondeka. Wanateswa, wanaumizwa wahusika hawachukuliwi hatua zozote! Matumaini yao ya kuishi kwa amani katika nchi njema waliojaliwa na Muumba wao yamezimika. Maisha ya wananchi sasa ni mashaka matupu. Kwanini wasiutamani utawala mpya?

Baba si uwaonyeshe watu wako kuliko na faraja. Taifa limefunikwa na simanzi. Nchi inayegayega. Masikini hatujui kesho atakuwa nani. Ole, ole wao. Anafarijika vipi kiongozi anayeongoza masikini waliovunjika mitima yao? Kama yupo mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kuwalinda akina Kibanda na wananchi wengine, hakika huyu atakuwa na mengi ya kumjibu Mwenyezi Mungu siku yake ikifika. Uzito wa udongo utakaofukiwa juu yake utamuelemea hadi kiama.

Ndugu rais, kuishi ni bahati, lakini kufa ni lazima. Katika kipindi hiki kigumu ni vyema Kibanda na wanawema wote wanaoandika wakiwalilia maskini wa nchi hii na nchi yao, wafahamu kuwa watateswa na kuumizwa sana hata kuuawa. lakini hawatateswa wala kuuawa wote. Atabaki walau mmoja, wa kupeleka habari. Ujumbe wao hautauawa, utafika.

Wakumbuke wakati ule Mungu alipomjaribia Ayubu. Kwa wasiomjua Ayubu ni kwamba palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na uelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu na kuepukana na uovu. Siku moja akatokea mtu na kumwambia Ayubu akisema; “Ng’ombe wako walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao; wakatokea Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.”

Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine na kusema; “Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia wakaenda nao naam, wamewaua watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.”

Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine na kusema; “Wanao na binti zako walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mara tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani ukaipiga  hiyo nyumba pembe zake nne nayo ikawaangukia hao vijana nao wamekufa, na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.”

Rais wangu, tunaambiwa baada ya kuyasikia hayo, Ayubu aliinuka, akalirarua joho lake kisha akanyoa kichwa chake na kusujudia katika nchi akisema; “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile.”

Ndugu rais, waliposhambuliwa kwa makali ya upanga na kumwagiwa tindikali wanawema Saed Kubenea, Ndimara Tegambwage na wenzao wa MwanaHalisi, mimi nilikuletea habari.

Polisi walipowaua kinyama wanawema wa Ulanga waliokuwa wanafanya biashara ya madini pamoja na dereva teksi kule kwenye msitu wa Pande, mimi nilikuletea habari.

Polisi walipowaua kwa risasi wanawema watatu kule Arusha wakati wa maandamano, mimi nilikuletea habari. Polisi  walipowaua raia wema kule Ruvuma mimi nilikuletea habari.

Shabani Matutu alipopigwa risasi ya kifua na polisi na majanga yaliyowasibu waandishi wengine kule Kagera na Kigoma mimi nilikuletea habari.

Unyama wa kutisha waliofanyiwa Stephen Ulimboka na Kibanda na hitimisho la kinyama kwa mauaji ya Daud Mwangosi, mimi nimekuletea habari.

Hata yule maskini mama mjamzito aliyeuawa kwa kupigwa risasi ndani mwake kule Mtwara hivi karibuni, mimi nilikuletea habari.

Baada ya kuletewa habari Ayubu alijinyenyekesha kwa Mungu wake, akamsujudia. Baba umepata nafasi ya kumrejea Muumba wako kwa hizi habari nilizokuletea. Wanaotesa na kuua na wanaoteswa na kuuawa na sisi wengine, tulitoka katika matumbo ya mama zetu tukiwa uchi, nasi tutarudi huko vilevile. Watu wamekuwa wanyama kushinda wanyama wenyewe! Nchi ya visasi sasa inatengenezwa.

Yaliyotupasa kutenda, kwa maana ya kufikisha ujumbe, tumetenda, ujumbe tumefikisha. Tutaendelea kuyarudia haya kama sala ya asubuhi bila kuchoka hadi hapo haki itakaporejeshwa katika nchi.

Rais wangu, tunapoandika historia hii tujikumbushe baadhi ya matukio yaliyojiri wakati wa sherehe za miaka 36 ya CCM kule Kigoma tarehe 5-2-2013.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliongoza timu yake kwenda Kigoma kwenye sherehe za kutimiza miaka 36 huku wakiwa wamepanda ‘abiria’ (Treni ya abiria).

Akatukumbusha Salim Ahmed Salim alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, ambapo alisafiri kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara. Barabara ile haijaisha hadi leo!

Taarifa zinaarifu kuwa wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawalindi tena mipaka ya nchi yetu kule Mtwara. Wanachofanya ni kuwadhibiti wananchi wa Mtwara wasifurukute. Wanaosema nchi yetu sehemu ya Mtwara inatawaliwa Kijeshi wanakosea wapi?

Kinana na wenzake walipanda treni, njiani wakila ugali na mboga za majani, nao wakaonekana kufanana na Watanzania wengine. Nikisema hivi ninakiri kuwa maisha wanayoishi viongozi wengi hayafanani kabisa na maisha ya wananchi wanaowaongoza. Na kwa sababu hiyo namwomba Mwenyezi Mungu, amjalie Kinana uwezo ili afanikishe ndoto yake njema ya kufuta uheshimiwa bandia waliojivika viongozi wetu. Kujiita mheshimiwa mbele ya mwajiri wako ni kukosa adabu. Hata uwe nani wewe huna adabu.

Mtu huyu alibeba udongo na kisha akabeba tofari na kujenga nyumba kwa mikono yake. Watu wa zamani wakakumbuka walivyomshuhudia mkuu wa nchi na Rais wa Jamhuri, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na jembe la mkono, akishirikiana na wanakijiji kulima shamba la kijiji. Kumbukumbu hizi njema zilikwisha potea.

Wakati wa urais wa Mwalimu Nyerere, viongozi wetu wote walikuwa ndugu zetu.

Siku hizi tumezoea kuwaona baadhi ya viongozi wetu wakipanda mti wa kumbukumbu huku wakiwa wametandikiwa zulia aghali mahali pa kupigia magoti. Kuogopa udongo wakati wewe ni mavumbi; na mavumbini utarudi ni ufala! Acheni hizo.

Rais wangu, zikaja habari kuwa uliwaomba Watanzania kuwa ukishakupita, uje ukumbukwe kama bwana maendeleo! Maendeleo na mabadiliko ni vitu viwili tofauti kabisa. Majanga haya tunayokuletea habari hayakuwapo katika awamu zilizotangulia. Kumbukumbu zake hazitakoma.

Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anakumbukwa leo na Watanzania wema na hata na Afrika na Dunia kwa upendo mkuu aliouonyesha kwa nchi yake na kwa wananchi wake.

Nyerere, wananchi wake walipolia kama hivi tunavyolia, alilia nao. Hakuonyesha dalili zozote za ukiziwi. Atakumbukwa hata na vizazi vingi vijavyo kwa ile tunu kuu aliyowatunukia Watanzania, Azimio la Arusha.

Azimio la Arusha lilijikita katika siasa ya ujamaa na kujitegemea. Nchi ilikuwa na dira na mwelekeo. Taifa likawa na itikadi iliyo wazi. Leo Watanzania hawajui wanaelekea wapi.

Edward Moringe Sokoine hawezi kusahaulika katika historia ya nchi hii. Uadilifu wake usio shaka na umahiri wake uliotukuka katika kutenda kazi, ni tunu nyingine ambayo taifa hili halitakuja kusahau. Hawa hawakuomba kuwa wakishapita waje wakumbukwe kwa hayo. Mtu haombi kukumbukwa kwa mdomo wake mwenyewe. Nchi, kama dunia ina utaratibu wake wa kumkumbuka mtu.

Yaweza kuwa ni bahati mbaya lakini huo ndiyo ukweli wa ulimwengu kuwa haya maovu tunayokuletea habari iwe, isiwe yatakufanya ukumbukwe kwa muda mrefu ujao! Wala usinyong’onyee kwa hili baba kwa kuwa Mungu ni mwema, hamnyimi mtu kila kitu. Jitihada zako binafsi katika kutaka katiba mpya watu wako wameziona. Fanikisha hili kwa haki nawe utakumbukwa kwa hili. Pamoja na rasimu kukubalika kwa asilimia kubwa lakini kuna mambo ya msingi hayajawa wazi.

Wananchi wana matarajio yao na hisia zao ambavyo katiba mpya haina budi kuonyesha kuwa inajali. Nchi ilikuwa na siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo baada ya kutupwa rasmi na rasimu tuliyoletewa hakuna kilichowekwa badala yake. Kuna ubepari, kuna ukoloni mambo leo, haijulikani nchi imeelekezwa wapi.

Lengo kuu la katiba kwa maslahi ya taifa lazima litajwe. Bila hivyo Watanzania watafanana na mifugo iliyo ndani ya lori ambalo halijulikani linakwenda wapi.

Rais wangu, eneo lingine linaloweza kumfanya mtu akumbukwe kwa wema ni kusahihisha yaliyojiri Kigoma. Uwepo wa Makamu Mwenyekiti Phillip Mangula na Katibu mkuu wake Kinana katika sherehe za miaka 36 kuliziongezea maana zaidi sherehe zile.

Hawa wawili wanaelewa vizuri sana kuwa kuifanya CCM izaliwe tarehe 5, Februari, haikuwa ajali, kulipangwa kwa makusudi. Waasisi wa CCM hawakuikurupukia tarehe hiyo.

Tarehe 5, Februari 1967 kama ilivyokuwa tarehe 9, Desemba 1961 ndiyo siku ulipotangazwa ukombozi na uhuru wa kweli wa maskini wa nchi hii.

Siku lilipotangazwa rasmi Azimio la Arusha. Mangula na  Kinana wanaujua vizuri uzito wa siku hii. Watu waliimba wakisema; “Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, tuishangilie na kuifurahia.”

Kuifanya CCM kuzaliwa siku hiyo ikiwa ni miaka kumi imepita tangu kutangazwa Azimio la Arusha kulikuwa na maana moja tu, kwamba CCM ni zao la Azimio la Arusha. Kwamba maono, dira na matarajio ya Azimio la Arusha ndiyo yangekuwa ya CCM. Ni bahati mbaya kuwa hiyo haikuwa.

Hivyo kuitukuza CCM bila hata kulitaja tu Azimio la Arusha kama ilivyotokea Kigoma kungeweza kufananishwa na uhaini. Ni ishara ya kuwavika tena minyororo wananchi, minyororo ileile waliokuwa wamekwishavuliwa na Azimio la Arusha!

Azimio la Arusha ndiyo lilikuwa tegemeo na kinga ya Watanzania maskini dhidi ya viongozi wao walafi. Likadhibiti pengo kati ya walionacho na wasionacho, na hivyo kuijenga jamii yenye undugu wa kweli, uelewano na mshikamano. Leo limevunjwa wananchi hawana wa kumlilia. Watanzania wanaishi kwa staili ya wanyama wa mwituni. Kila mtu anakula kulingana na urefu wa makucha yake!

Ije mvua, lije jua Mangula na Kinana wanapaswa kukubaliana na ukweli kuwa chama chao kina deni kubwa kwa wananchi wa nchi hii. Deni hilo ni Azimio la Arusha. Kama wanamkubali Mwalimu Nyerere kuwa ni baba wa taifa hili, basi kile chema baba alichowatengenezea watu wake halafu chama chao kikabomoa, wanapaswa kukirudishia. Waache waje wabomoe watu baki. Bila kufanya hivyo hawa wataikwepaje laana ya mzazi wao? Kuyapuuza maandiko haya  ni kuitafuta hukumu ya bure. Nao watafanana na wale watu kule kwetu wanaitwa ‘wakoma chifwile’ yaani watu wanaoua kilichokwishajifia! Mamlaka waliYopewa hayakutokana na kazi ya mikono yao, bali kwake aliyewapeleka baada ya kuyaona mateso ya waja wake!

SOURCE: FREEMEDIA

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top