Katibu wa Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji, Meckland Millanzi, ameiomba Mahakama ya Wilaya ya Mtwara kutenda haki, bila kushinikizwa na upande wowote ili haki itendeke dhidi ya mbunge huyo, ambaye yuko rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Millanzi alisema ameshangazwa na kitendo cha mahakama kukataa kupokea pasi ya kusafiria, ambayo ilitakiwa kuwasilishwa mahakamani hapo, ili apewe dhamana.
“Jana mahakama ilikataa kumtoa mbunge kwa sababu hakukamilisha masharti ya dhamana. Leo kibali cha kusafiria tumekiwasilisha mahakamani. Bado wamekataa kumtoa, ingawa taratibu zote tumekamilisha,” alisema Millanzi.
“Kuna baadhi ya washitakiwa, ambao wa vurugu za gesi walifikishwa jana mahakamani, na kwa bahati mbaya ndugu zao hawakukamilisha masharti ya dhamana, lakini leo wamefika mahakamani wamepatiwa kibali cha kuwaruhusu kutoka rumande, lakini sisi tumekataliwa licha ya kukamilisha taratibu zote,” alisema.
Kwa mujibu wa Millanzi, sababu zilizotelewa mahakamani hapo hazina msingi na kwamba, mahakama ni chombo kinachotenda haki na kuaminiwa na watu wengi.
“Sababu tulizoambiwa kuwa leo, hawezi kutoka eti kwa sababu za kiusalama wake. Sasa kama kesho atatolewa hali yake ya usalama itakuwaje?” alihoji Millanzi.
Murji alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara na kusomewa shitaka la kufanya uchochezi, Januari 19, mwaka huu, katika eneo la Ligula.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.