Unknown Unknown Author
Title: PINDA AZIMA MZOZO WA GESI MTWARA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amefanikiwa kutuliza jazba za wakazi wa mkoa wa Mtwara kwa kuwaeleza kuwa kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajen...
1WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amefanikiwa kutuliza jazba za wakazi wa mkoa wa Mtwara kwa kuwaeleza kuwa kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajenngwa kijiji cha Madimba, mkoani hamo ili mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda, tofauti na madai ya wakazi hao kuwa kiwanda hicho kitajengwa jijini Dare s Salaam.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho uliofanyika leo, Veta mjini Mtwara baada ya kusikiliza madai ya wananchi hao kwa siku mbili mfululizo, Pinda alisema hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirisha kwa njia ya bomba.
“Wataalam wanasema gesi haiwezi kwa namna yeyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu…kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba, gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo” alisema Pinda na kuongeza
“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa…gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme…tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme”
Awali madai ya wakazi wa mkoa wa Mtwara yalikuwa kupinga usafirishaji wa gesi ghafi kwenda Dare s Salaam wakieleza kuwa mpango huo utafukuza uwekezaji wa viwanda mkoani humo, ambao ungechochewa na upatikanaji wa malighafi baada ya kusafishwa kwa gesi.

Pia wananchi walipinga ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi jijini Dar es Salaam wakiitaka serikali kujenga mitambo hiyo mkoani Mtwara.
“Gesi lazima isindikwe Mtwara, haitoki hadi viwanda vije…nadhani hili ni jambo jema lazima tuliwekee utaratibu …nikawauliza wataalam wangu kwani kiwanda cha kusafisha gesi kinajengwa wapi, wakanijibu Madimda…nikasema kumbe tatizo kubwa ni kutowaeleza wananchi suala la gesi vya kutosha” alisema Waziri Mkuu huku akipigiwa makofi
“Nafikiri tatizo ni sisi serikali hatukuwa na mpango mzuri wa kuwaelimisha wananchi” alifafanua Pinda
Aidha aliwataka wananchi kumsamehe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Joseph Simbakali kwa kauli alizozitoa 21 Desemba mwaka jana katika kikao cha kamati ya ushauri mkoa,(RCC) pale alipoombwa kuyapokea maandamano ya wakazi wa mkoa huo Desemba, 27, mwaka jana ambapo aliwaita wapuuzi wananchi hao na baadae wahaini.
“Binadamu kukosea lazima, lakini kubwa zaidi ni kuomba msamaha…amefanya hivyo, sasa tusahau yaliyopita tugange yajayo” alisema Pinda.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ilitanguliwa na kauli ya mkuu huyo wa mkoa kuwaomba radhi wakazi wa mkoa wa Mtwara na kwamba alipotoka kutoa kauli hiyo ambayo iliwaudhi wengi
“Kupitia hadhara hii nawaomba radhi kwa kuwakwaza , nimesikitishwa kwa kauli yangu imepokelewa kwa hisia kwamba nimewadharau” alisema Simbakalia
Waziri Mkuu katika majumuisho yake aliambatana na Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makzi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel Nchimbi.

Alitoa wito kwa wabunge wa mkoa wa Mtwara kufuta tofauti zao za kisiasa ili waweze kuharakisha maendeleo ya mkoa huo.
“Purukushani hizi ndani ya chama hazina tija, tuseme basi…wabunge hawaelewani, sasa bungeni wanakwendaje..kila mtu na lake …hebu tuseme watu kwanza mimi badae” alisema Pinda huku akishangiliwa
Pinda katika siku zake hizo mbili mkoani Mtwara alikutana na vyama vya siasa vya upinzani, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Viongozi wa dini ya kiislam na kikiristo, wafanyabishara, madiwani na wenyeviti wa mitaa pamoja na wanaharakati mbalimbali.
Akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama DK. Nchimbi alisema hali kwa sasa shwari na kwamba wizara yake imejidhatiti kwa watu na vifaa kukabilina na vurugu zozote huku akikwepa kuzungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari wanaodaiwa kuwauwa wananchi wilayani Masasi.
Dk. Nchimbi alisema katika tukio la Masasi watu wanne walifariki dunia, kinyume na taarifa ya muuguzi wa zamu hospitali ya Mkomaindo  Amina Tumbi aliyoitoa kwa waandishi wa habari siku ya tukio ambapo alisema amepokea miili ya watu Saba kabla ya siku ya pili kuripotiwa kwa kifo cha aliyekuwa majeruhi hospitali ya Ndanda.
“”Hali ni shwari, tumejipanga vya kutosha kwa watu na vifaa…Hii ni tabia mbaya haikubaliki …unapamba na polisi…itafika wakati watoto wetu watakataa kujinga na polisi…tutapambana kikamilifu misniharibie kazi mimi nina miaka 41” alisema Nchimbi
Kwa upande wake Dk. Kawambwa alisema wizara yake imeamua kuifanya Veta Mtwara kuwa kituo cha umahiri ili wahitimu wake waweze kuajiriwa katika sekta ya gesi.
Naye Profesa Tibaijuka alisema wizara yake imekamilisha mipango miji kwa mji wa Mtwara ili uweze kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kwamba wananchi wa mkoa huo wawe tayari kuendana na hali hiyo.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe alisema bandari ya Mtwara haijauzwa na kwamba inapanuliwa ili iweze kukidhi mahitaji ya baade huku akiahidi kutembela Mtwara kila baada ya miezi Mitatu ili kutoa taarifa ya maendeleo ya bandari na uwanja wa ndege kwa wananchi.
“Tulikuwa na eneo la hekta 70 tu za bandari ya Mtwara, sasa tumepanua na tunayo hekta 2994 , tumetenga hekta 110 ili tuweze kuwa na bandari huru itakayowezesha kuongezeka kwa matumizi ya bandari yetu” alisema Dk. Mwakyembe
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa vyama Tisa vya siasa mkoani Mtwara, Uledi Abdallah amesema madai ya wananchi yalikuwa mitambo ya kusafisha gesi ghafi ijengwe Mtwara na kwamba iwapo serikali imeamua kufanya hivyo madai yao yatakuwa yamekwisha.
“Kama gesi itayosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa, sisi hatuna tatizo” alisema Abdallah
Nae Mbunge wa Mtwara Mjini Asnain Murji alimpongeza Waziri Mkuu kwa hatua yake ya kuwasikiliza wananchi na kwamba mzozo huo uliodumu kwa takribani mwezi mmoja sasa umefikia tamati.

Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Mtwara mjini Saidi Kulaga alimpongeza waziri huyo kwa hatua aliyoichukua na kumuomba awaachie huru wale waliokamatwa kutokana na vurugu zilizotokea Mtwara na Masasi ili kujengwa mwanzo mpya wa mahusiano mazuri baina ya serikali na wananchi, ombi ambalo Waziri Mkuu alilipokea na kuahidi kulifanyia kazi ndani ya wiki mbili.
source: KUSINI BLOG























About Author

Advertisement

 
Top