KLABU
ya Manchester United sasa imekaa mkao wa kula baada ya Wesley Sneijder
kuambiwa hawezi kucheza Inter Milan tena hadi akubali kupunguziwa
mshahara wake wa pauni 200,000 kwa wiki.
Kiungo
huyo Mholanzi, amegoma kupunguziwa mshahara Inter na Mkurugenzi wa
klabu hiyo, Marco Branca amesema hatahusishwa kwenye mipango ya klabu
hiyo akubali kupunguziwa mshahara.
Sneijder,
ambaye aliiongoza Inter chini ya kocha Jose Mourinho kutwaa taji la
Ligi ya Mabingwa na ya nyumbani mwaka 2010, alikuwa anatakiwa na klabu
kadhaa ikiwemo Man United, lakini Sir Alex Ferguson aliamua kuachana
naye kutokana na mshahara mkubwa alioutaka.
Lakini sasa kuna uwezekano Mholanzi huyo akatua United January.
Mchezaji
huyo mwenye umri wa miaka 28, alisaini mkataba mpya wa miaka mitano
wenye mshahara huo mnono wa pauni 200,000 kwa wiki mwaka 2010, lakini
Inter hivi sasa iko katika mpango wa kupunguza bajeti yake na matokeo
yake ni pamoja na kumuuzaa kipa Julio Cesar kwenda QPR msimu huu.
Branca ametoa taarifa kuhusu Sneijder, ambaye ametemwa kwenye kikosi kinachomenyana na Parma leo, katika tovuti ya klabu hiyo.