Shilingi bilioni 86 zaibwa Wizara ya Nishati/TANESCO, Gridi ya Taifa hatarini
Gazeti la The East African la Novemba 24 – 30, 2012 limetoa
taarifa kwamba jumla ya dola za kimarekani milioni 54 zimegundulika
kuibwa na watumishi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika
la TANESCO kupitia manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mtambo wa Umeme wa
IPTL. Gazeti hili limenukuu taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Tanzania (Controller and Auditor General). Taarifa hiyo
inasema kuna kikundi (racket) ambacho kazi yake kubwa ni kujifaidisha
binafsi na mpango wa umeme wa dharura kupitia manunuzi ya Mafuta mazito
ya IPTL.
Itakumbukwa
kwamba toka mwaka 2011 kumekuwa na shinikizo lililotolewa na Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba zabuni za ununuzi wa
mafuta ya kuendesha mpango wa umeme wa dharura na mchakato mzima wa
manunuzi ya mafuta haya ufanyiwe uchunguzi wa kina (forensic audit).
Katika
mkutano wa 3 wa Bunge la Kumi (April 2011) niliuliza swali Bungeni
kuhusu kashfa hii ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mtambo wa IPTL na
baadaye tarehe 16 Aprili 2011 nilimwomba Spika airuhusu Kamati ya
Nishati na Madini kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hii. Kamati ya Nishati
na Madini chini ya aliyekuwa Mwenyekiti ndugu January Makamba ililitaka
Bunge kuazimia kufanyika kwa uchunguzi kuhusu suala hili kwenye Taarifa
yake ya mwaka 2011 iliyowasilishwa Bungeni mwezi Aprili mwaka 2012.
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ndugu John Mnyika katika Hotuba yake
ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2011 alipendekeza kufanyika kwa uchunguzi
kuhusu kashfa hii pia. Juhudi zote hizo hazikuzaa matunda.
Kipindi
hicho kiwango kilichokuwa kinahojiwa kuibwa ni shilingi bilioni 15 tu.
Taarifa ya The East African kama walivyonukuu kutoka kwenye taarifa ya
CAG inaonyesha fedha zilizoibwa ni shilingi bilioni 86.
Zabuni
za kununua mafuta ya kuendesha umeme wa dharura zimekuwa zikitolewa
bila kufuata utaratibu wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya manunuzi. Hivi
sasa kila mwezi Tanzania inatumia dola milioni 70 kununua mafuta ya
kuendesha mitambo ya umeme. Fedha hizi zinatoka Hazina na sehemu ndogo
kutoka TANESCO. Wakati fedha hizi bilioni 112 zinachomwa kila mwezi
kununua mafuta mazito na dizeli ya kuendesha mitambo ya umeme, Taarifa
za kitaalamu zinaonyesha kwamba Bwawa la Mtera hivi lina kina cha maji
chini ya kiwango kinachotakiwa na uzalishaji wa umeme ni asilimia 20 tu
ya uwezo (installed capacity). Iwapo TANESCO wataendelea kutumia zaidi
maji yaliyopo Mtera, Mitambo itashindwa kazi na Gridi nzima itasimama
maana Mtera ndio nguzo kuu ya Gridi ya Taifa. Hali hii ni hatari sana
kwa uchumi na ulinzi na usalama wa Taifa. Kimsingi Gridi ya Taifa ipo
hatarini kutokana na kiwango cha Maji kilichopo Mtera hivi sasa na
kuendelea kupungua kwa kina hicho cha maji.
Wananchi wanapaswa kuelezwa kinaga ubaga nini kinaendelea katika sekta ndogo ya umeme hapa nchini;
1.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuhusu zabuni za
manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura iwekwe wazi
na ‘racket’ inayosemekana kuiba jumla ya shilingi bilioni 86 ionyeshwe
na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja na bila kuchelewa.
2.
Waziri wa Nishati na Maadini auleze umma hali yalisi ya sekta ya umeme
nchini, uzalishaji wa umeme upoje, hali ya maji katika bwawa mkakati la
Mtera na nini hatma ya mitambo ya IPTL, kesi zake na utekelezaji wa
mapendekezo ya Bunge kuwa kesi za kampuni hii zimalizwe nje ya mahakama.
Pia Taifa lielezwe Mpango wa Dharura wa umeme unakwisha lini maana muda
uliotolewa na Bunge mwezi Agosti mwaka 2011 tayari umekamilika. Waziri
aeleze hatua agni amechukua baada ya kukabidhiwa taarifa na CAG kuhusu
maafisa waandamizi wa Wizara waliohusika na wizi wa shilingi bilioni 86
za kununua mafuta ya IPTL.
3.
Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma ni kiwango gani cha fedha Hazina
imetoa kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura kati ya
Mwezi Novemba mwaka 2011 na Oktoba mwaka 2012 na kama taratibu zote za
zabuni zilifuatwa na pale ambapo hazikufuatwa ni hatua gani PPRA
wamechukua dhidi ya waliokiuka sheria ya manunuzi na kuleta hasara ya
mabilioni ya fedha kwa Serikali.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha
Dar es Salaam. Novemba 25, 2012