• GHARAMA yake ni Dola 250,000 kila Kiwanja!
• KUANZA Desemba Klabu Bingwa Duniani huko Japan
• England kuanza Januari
IFAB leo imetoa uamuzi wa kihistoria na kupitisha kuwemo kwenye Sheria za Soka Teknolojia ya kugundua kama Mpira umevuka mstari wa Goli au la, itakayotumia Mitambo ya aina mbili ya Hawk Eye na GoalRef, ambayo imetengenezwa ili kuwasaidia Marefa kutoa uamuzi sahihi na wa haraka kama ni Goli au si Goli.
IFAHAMU IFAB:
IFAB inaundwa na Vyama vya Soka vya Visiwa vya Uingereza, yaani vile vya England, Wales, Scotland na Ireland, ambao ndio wanachukuliwa kama waanzilishi wa mchezo wa Soka, na Wawakilishi kutoka FIFA.
Mabadiliko yeyote ya Sheria za Soka lazima yapitie IFAB ambako hupitishwa ikiwa tu Kura 6 kati ya 8 zilizopo zitaunga mkono.
Mgawanyo wa Kura hizo 8 ni moja kwa kila Chama cha Soka cha England, Wales, Scotland na Ireland huku FIFA wakiwa na Kura 4.
Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke amesema FIFA itatumia Teknolojia hiyo kwenye
Mashindano ya FIFA ya Klabu Bingwa Duniani huko Japan Mwezi Desemba, Mashindano ya Kombe la Mabara Mwakani huko Brazil na Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Brazil Mwaka 2014.
Valcke ametamka kuwa FIFA itagharimia Mitambo hiyo, ambayo inagharimu Dola 250,000 kwa kila Kiwanja, na kuiacha kwenye Uwanja husika Mashindano yakimalizika.
Chama cha Soka cha England, FA, kimetamka kuwa wao wanategemea kuanza kutumia Teknolojia hiyo kuanzia Januari 2013.
FIFA na IFAB zimesisitiza kuwa Teknolojia hiyo ya kugundua kama Mpira umevuka mstari wa Goli au la, kwa kutumia Hawk Eye na GoalRef, imetengenezwa ili kuwasaidia Marefa kutoa uamuzi sahihi na wa haraka kama ni Goli au si Goli na yenyewe si ambayo itatoa maamuzi kwani Marefa watabakia ndio wenye uamuzi wa mwisho.