Mkuu wa wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulega amesema kuwa umefika wakati jamii ikaachana na siasa za vyama na badala yake itazame maendeleo.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha baraza la madiwani kilichowasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilaya ya Kilwa kwa mwaka 2011/2012, Ulega alisema kuwa ni vyema kuibua mambo ya ya msingi yatakayoleta maendeleo badala ya kuwa na siasa zisizo na mashiko.“Kilwa tunataka iwe na mabadiliko chanya,mabadiliko ya kimaendeleo siasa za ccm na cuf za kutishana,kuhamasishana maandamano au vurugu ama kuapizana ushughulikiana zimepitwa sasa ni wakati wa kutazama fursa mpya za Kilwa kama gesi,ufuta vitu vinavyotuletea maendeleo”alisema Ulega Katika hatua nyingine wakuu wa Idara mbalimbali wametakiwa kuacha tabia ya kuwadanganya Wakurugenzi wa halmashauri katika suala zima la mradi ya maendeleo.
Hatua hiyo imekuja baada ya ripoti ya maendeleo ya Kilwa kwa upande wa afya kueleza kuwa ukarabati wa zahanati ya Nandete,Mwengei,Hanga na Darajani mekamilikawakati vituo hivyo bado vinaendelea na hatua za awali za ujenzi. Akizungumzia kitendo hicho Diwani wa Songosongo, Hassan Swaleh, alisema kuwa wakuu wengi wa idara wamekuwa na tabia ya kuwadanganya wakurugenzi kuwa wamekamilisha miradi mingi jambo ambalo si kweli,huku akizitaka halmashauri kupunguza matumizi yasiyo na lazima ikiwemo posho zisizo na tija.
Naye Mkurugenzi Mtendaji, Adoh Mapunda alisema kuwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 halmashauri ya Kilwa imetekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 3.5 sawa na asilimia 68.2 ambazo zilitumika katika sekta ya elimu, afya, maji, barabara na ujenzi, ardhi,kilimo,uvuvi na ufugaji.