UKOSEFU WA DAWA SI JUKUMU LA NHIF,NI CHANGAMOTO YA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA MFUKO..



nhifMFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema hauna jukumu la kusambaza dawa na hauwezi kuingilia majukumu ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hivyo ukavitaka vituo kutumia fedha zitokanazo na vyanzo vingine kununulia dawa ili kuziba pengo lililopo.
Umesema kuwa endapo fedha zitokanazo na Mifuko ya NHIF, CHF na fedha za papo kwa papo zitasimamiwa vyema na kutumiwa katika ununuzi wa dawa, tatizo la ukosefu wa dawa vituoni litapungua na kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Bw Emanuel Humba alieleza Wadau wa mfuko huo kuwa suala la ukosefu wa dawa vituoni lichukuliwe kama changamoto katika miaka 10 ya NHIF
"Jamani Mfuko wetu hauna jukumu la kusambaza dawa na hatuwezi kuingilia kamwe majukumu ya MSD, ila tunachowashauri ni kutumia vizuri fedha za vyanzo vingine kununulia dawa wakati kunapoonekana upungufu wa dawa kutoka MSD," alisisitiza.
Aidha HUMBA alisema kuwa mchango mkubwa unaofanywa na NHIF katika kuhakikisha huduma za matibabu zinakuwa bora ni utoaji wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ambayo itaviwezesha vituo kuboresha huduma zake ambazo zitakuwa ni kwa wananchi wote na si kwa wanachama peke yake.
mkurugenzi
Mkurugenzi mkuu NHIF,Emanuel Humba





"Lengo letu kubwa ni kuboresha huduma za afya ili hatimaye kauli mbiu yetu ya Huduma bora vijijini na afya kwa wote ionekane kwa vitendo na kulitimiza hilo ndio maana tunatoa fursa kama hizo za mikopo na kuzihimiza hospitali kuwa na maduka ya dawa ili wanachama na wananchi wasiondoke hospitali bila ya kuwa na dawa lakini viongozi hasa madiwani tusaidieni kusimamia fedha hizi zinazotokana na mifuko hii ili zitumike kuboresha na kupunguza matatizo kama ya dawa," alisema Humba
Wadau hao wakichangia mada zilizowasilishwa na viongozi wa NHIF, walisema kuwa moja ya mambo yanayokwamisha wananchi kujiunga na CHF ni ukosefu wa dawa na huduma mbovu vituoni ambapo walishauri kuwa wakati uhamasishaji ukiendelea ni vyema na matatizo hayo yakashughulikiwa ili wananchi wawe na imani zaidi.
Pamoja na kuonekana kuwepo kwa changamoto zinazokwamisha suala hilo,Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Magalula Saidi Magalula wakati akifungua mkutano huo wa wadau kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Ludovick Mwananzira, alizitaka Halmashauri kujipanga na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo lakini pia kuweka sheria itakayowalazimisha wananchi kujiunga na CHF.
DSC00450
Magalula Saidi Magalula,
"Halmashauri jipangeni, uboreshaji wa huduma ndio utakaowavutia wananchi kujiunga na Mfuko huu na kwa Mikoa ambayo imeweza kutumia vyema fedha za CHF imefanikiwa sana na tatizo la dawa hakuna...angalieni hilo na mlifanyie kazi ili wananchi wetu wawe na uhakika wa matibabu," alisema.
Mkutano huo wa Wadau wa Mfuko toka Mkoa wa Lindi ulitanguliwa na utoaji wa Msaada wa Mashuka katika wadi za Hospital ya Mkoa ( Sokoine Hosp)na kukabidhi Sare za usalama wa Madereva wa Bodaboda
Previous Post Next Post