Tanzania inapaswa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha hakuna vifo vya wanawake na watoto wakati wa ujauzito na uzazi, alisema Salma Kikwete, mke wa rais wa Tanzania, hapo Alhamisi (tarehe 15 Machi) katika mkutano wa siku ya Utepe Mweupe ulioitishwa kushajiisha uzazi salama.Kwa sasa Tanzania ina kiwango cha juu cha watoto wanaokuwa hai katika Afrika ya Mashariki .
Vilevile alisema kwamba wanawake wengi zaidi sasa wanaamua kujifungulia hospitalini na kutumia njia za uzazi wa mpango, mambo ambayo yanawasaidia kuimarisha afya zao. "Ni dalili nzuri inayoonyesha kwamba kama tutaongeza jitihada, inawezekana kupunguza vifo kwa kiasi kikubwa au hata kuviondosha kabisa," alisema Salma Kikwete, akiongeza kuwa hilo litaiweka Tanzania katika uwezekano wa kufikia Malengo ya Kimaendeleo ya Milenia.
Salma Kikwete alizitaka familia na taasisi za kiraia kutenga sehemu ya bajeti zake kwa mama wajawazito, na pia kuitaka serikali kutekeleza ahadi zake za kuongeza wanafunzi katika vyuo vya afya.