UMOJA wa wanawake Tanzania (UWT) Katika Wilaya za Ileje na Mbozi, mkoani Mbeya wamekabidhiwa mashine mbili za kutotolea vifaranga vya kuku zenye thamani ya Sh4 milioni.Wajasiriamali wadogo wamepewa mashine hizo baada ya kujiunga katika vikundi katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji.
Msaada huo ulitolewa jana na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM), Mary Mwanjelwa katika hafla, uliyofanyika katika wilaya hizo mbili.
Katika shughuli hiyo Mwanjelwa alichangia Sh1.1 milioni na baadhi ya fedha hizo ni sehemu ya kuanzishia miradi hiyo na kila mashine ina uwezo wa kuzalisha vifaranga 100 kwa siku.
Katika mgawanyo huo Wilaya ya Ileje mbunge huyo alichangia Sh400,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi na Wilaya ya Mbozi alitoa Sh700,000 kwa ajili ya kuanzisha wa miradi hiyo ambayo imelenga kuwashirikisha wanawake katika ngazi ya kata na vijiji.Mwanjelwa alisema ametoa msaada huo ili kuwasaidia wanawake kuongeza kipato na wasiwe tegemezi.
Alisema mbali ya kutoa misaada hiyo atafanya ziara katika kila kata na vijiji vilivyopo katika halmashauri zote za jiji la Mbeya kwa ajili ya kuhamasisha wanawake kuanzisha miradi endelevu na kujiunga katika vikundi vya wanawake ili wapate misaada ya fedha.Alisema mradi huo ni hatua za awali za kuwawezesha kusimama wenyewe ikiwa ni pamoja na kuwapelekea wataalamu wa kuwafundisha mbinu ya kuzalisha vifaranga vya kuku kwa wingi.
"Wanawake wakiwezeshwa wanaweza, mradi huu ni sehemu ya majaribio na endapo mtatunza vizuri na kuzalisha vifaranga kwa wingi mtaweza kupata miradi mingine zaidi ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi miongoni,"alisema.
Pia amewataka wanachama kutoa ushirikiano wa kuwafichua viongozi wa ngazi za wilaya wasiokuwa waadilifu katika chama ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.