WAZIRI MKUU AONGOZA MATEMBEZI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA TET

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza matembelezi ya hisani ya kuadhimisha miaka 50 ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TET) ambapo amesisitiza uongozi wa taasisi hiyo kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwenye shule zote nchini.

Waziri Mkuu amesema anafahamu kuwa TET imedhamiria kuchapa vitabu kwa wingi ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, jambo ambalo litaleta  manufaa makubwa katika elimu na Taifa kwa ujumla. “Hivyo, kwa dhamira ya dhati kabisa, sote hatuna budi kuliunga mkono jambo hili.”

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 7, 2025) alipozungumza baada ya kumalizika kwa matembezi ya hisani katika ofisi ya TET, Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu nchini.

Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na TET kutumia matembezi ya hisani kuchangisha fedha za kuchapisha vitabu ni vema kwa uongozi wa taasisi hiyo ukaongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa kushirikisha kampuni za uchapishaji na wadau wa sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji.

 

Amesema ushiriki wa wadau katika uchapishaji wa vitabu utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu shuleni, na kufikia lengo la kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. “Vitabu ni chanzo cha maarifa na maendeleo, na ni muhimu katika kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi.”

Akizunguzmia kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema kitabu kimoja mwanafunzi mmoja, Waziri Mkuu amesema inawiana na malengo ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa watoto wa Tanzania wanapata elimu bora. “Kupitia elimu bora, Taifa linaweza kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu na kuboresha ustawi wa jamii.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba alisema maadhimisho ya miaka 50 TET pamoja na kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu. “Maadhimisho haya yanalenga kukusanya shilingi bilioni 297 kwa ajili ya kufikia azma ya kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja na ununuzi wa kompyuta za kuhifadhi vitabu.”

 

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post