Simba SC ilionyesha Ukubwa wake katika dimba la Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa ni Steven Mukwala ambaye alifunga mabao matatu (hat-trick) na kuandika historia, kwani hii ni hat-trick ya kwanza kwa mchezaji wa Simba msimu huu. Mukwala alifunga bao la kwanza dakika ya 30, akimalizia pasi nzuri kutoka kwa David Kameta 'Duchu', ambaye alifanya debut yake katika mchezo huo.
Kabla ya mapumziko, Elie Mpanzu alifanya assist yake ya tatu msimu huu, akimuwekea Mukwala bao la pili. Simba iliendelea kutawala mchezo huo hata baada ya mapumziko, na tena ni Mukwala alifunga bao la tatu akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Coastal Union baada ya shuti la Mpanzu.
Kwa sasa, Mukwala amefikisha mabao nane na kumfikia mshambuliaji mwenzake, Lionel Ateba, huku akionekana kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba.
Katika mchezo huu, wachezaji wa Simba walionyesha ari na hamu ya kushinda, na ingawa walishinda 3-0, waliweza kutengeneza nafasi nyingi zaidi ambazo zingewawezesha kupata ushindi mkubwa zaidi.
Simba sasa inafikisha alama 54, ikiwa nyuma ya watani zao Yanga, ambao wana alama 58, huku Simba ikiwa na mechi moja ya kiporo. Mchezo ujao wa Simba dhidi ya Yanga tarehe 8 Machi utakuwa muhimu katika jitihada za kurejea kileleni.