Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva ameongoza mamia ya wakazi wa Manispaa ya Lindi kwenye mazoezi ya viungo.
Mazoezi hayo yamefanyika Leo Machi 01, 2025 katika uwanja wa ilulu Manispaa ya Lindi yakihusisha klabu za jogging, Wananchi pamoja na wadau mbalimbali.
Akiongea na wanamichezo hao mara baada ya kuhitimisha mazoezi hayo DC Mwanziva amewapongeza kwa kujitokeza kwenye mazoezi sambamba na kuendelea kuujaza uwanja wa ilulu kila siku za jumamosi.
Aidha amewaomba wananchi wa Manispaa ya Lindi kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa letu, lakini pia kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha kulipa kodi.
Nae meneja wa TRA Mkoa wa Lindi bwana Robert Mhanzi ametoa wito kwa Wananchi wa Manispaa ya Lindi kuhakikisha wanakuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kudai na kutoa risiti mara baada ya kutoa au kupata huduma, risiti ambayo itakwenda sambamba na thamani ya fedha ya bidhaa au Huduma husika.
Ikumbukwe mazoezi hayo kwa wiki hii yamedhaminiwa na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Lindi ambapo Elimu ya mlipa kodi imetolewa kwa wanamichezo hao.