Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
Na. Ahmad Mmow. KILWA
Baada ya kuthibitika kuwa barua walizopelekewa waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Rais, kuwa hazikuandikwa wala kusainiwa na viongozi wa vijiji vya Rushungi, Lihimalyao Kusini na Kata ya Lihimalyao.
Viongozi hao wamemuomba mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kupitia vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humu viwatafute na kuwakamata walioandika barua hizo ambazo zilikuwa na malalamiko ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa hayana ukweli.
Huku barua hizo zikiwa na majina, nyazifa na saini za kughushi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu huyo wa mkoa katika kijiji cha Lihimalyao Kusini. Viongozi hao licha ya kukana barua hizo zilizokuwa na malalamiko kwamba kata ya Lihimalyao na tarafa ya Pande imetelekezwa katika huduma za jamii, hali ya usalama na kutonufaika na mapato ya gesi asilia ya Songosongo.
Walimuomba mkuu huyo wa mkoa kuwatafuta, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria walioandika barua hizo zilizosababisha mkuu huyo wa mkoa, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kilwa, mkurugenzi mtendaji na wakuu wa idara wa halmashauri ya wilaya hiyo kwenda kijijini hapo kupata ukweli wa malalamiko hayo.
Viongozi hao walisema hawakuwa na sababu ya kufikisha malalamiko au kudai huduma kwa njia hiyo kwasababu wanazijua taratibu za kuiomba serikali kupeleka huduma katika maeneo yao. Nakwamba barua hizo hazikuandikwa wala hazikusainiwa na wao.
Kaimu ofisa mtendaji wa kata ya Lihimalyao, Mwanahamisi Mwarabu, ambae alitajwa nakuonesha alisaini barua ya tarehe 21.11.2016 aliyoandikiwa waziri wa TAMISEMI, alisema jina la pili lililoandikwa halikuwa lake na hata saini iliyosainiwa haikuwa yake.
Akibainisha kuwa yeye ni mtumishi wa serikali nasio mwakilishi wa wawananchi. Hivyo hawezi kuandika barua ya aina hiyo na kuitumia serikali anayofanyia kazi, tena tuhuma za uongo.
"Mkuu wa mkoa, mimi naitwa Mwanahamisi Mwarabu, lakini kwenye barua hiyo nimeitwa Mwanahamisi Selemani na hata hiyo saini sio yangu," alisema Mwanahamisi.
Kaimu ofisa mtendaji kata huyo alisema hata mwenyekiti na mtendaji wa kijiji cha Rushungi ambao wametajwa kuandika na kusaini barua ya tarehe 15.11. mwaka jana, ambayo ilikwenda kwa Rais walikataa na kusema hawakuandika wala kusaini barua hiyo.
Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Lihimalyao Kusini, Yusufu Akida alisema kunaumuhimu wa serikali kuwatafuta na kuwakamata walioandika barua hizo na kughushi saini za viongozi wa vijiji na kata hiyo. Kwamadai kuwa wao kama viongozi wanazifahamu taratibu za kufikisha na kuomba mambo mbalimbali kwa serikali yao.
Alisema kitendo hicho kinania mbaya na ovu kuhusu mahusiano mema baina ya wananchi wa kata hiyo, serikali ya wilaya na mkoa huo.
"Hatusemi hayo kwasababu ya woga au kukufurahisha wewe mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya bali tunazijua njia na taratibu zakufikisha malalamiko, sio kukurupuka tu, mkuu wa mkuu wa mkoa umewahi kuja hapa, na mkuu wa wilaya umewahi kuja kama kawaida yako unatembelea sana vijiji vya wilaya yako. Mnatoa nafasi kwa wananchi kueleza kero mbalimbali, tungekuelezeni," alisema Akida.
Mwenyekiti wa serikali wa kijiji cha Ruyaya, Hassan Amanzi, alisema kitendo kilichofanywa na watu hao sio cha kiungwana na hakikubaliki. Akiongeza kusema hawakuwa na haja ya kuwatuma watu kufikisha malalamiko hayo ambayo mengi hayana ukweli.
Akitolea mfano malalamiko kuhusu mawasiliano, alisema tatizo hilo halipo kama barua hizo zilivyosema. Kwamba hakuna mawasiliano ya uhakika ya simu na kwamba wananchi wanalazimika kupanda juu ya miti wanapopiga simu. Kwani kampuni za simu za airtel na halotel zimejenga minara ya simu katika maeneo hayo.
"Haingekuwa vibaya sana kama wangejitaja majina yao, badala ya kutumia majina ya uongozi. Walifanya hivyo baada ya kujua kunabaadhi vitu walivyosema havina ukweli," alisema Hassan.
Pamoja na kubainika kwamba barua hizo hazikuandikwa na viongozi hao. Zambi alitoa nafasi kwa wananchi kueleza kero zao na yaliyokuwa kwenye barua hizo kama yalikuwa yana ukweli. Hata hivyo wananchi walisema hayakuwa na ukweli.
Wakitolea mfano tatizo la maji. Walisema tatizo hilo linatokana na maji yaliyopo yana magadi na hayafai kutumika kwa kunywa wala kufulia nguo. Hata hivyo visima vilichimbwa na serikali na kuna tangi la maji.
Wananchi hao walisema changamoto iliyopo ni wahudumu wachache kwenye zahanati, nyumba za watumishi wa zahanati na zahanati kuhitaji ukarabati na baadhi ya wakulima kucheleweshewa malipo ya korosho walizouza.
Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai alisema wao kama viongozi wa umma hawachukii wananchi kutoa maoni wala kutumia uhuru wa kujieleza. Kwasababu ni haki yao kwa mujibu wa katiba ya nchi. Pia wanahaki ya kufikisha kwenye ngazi yoyote ya uongozi kama walivyofanya wananchi hao waliandika barua hizo.
Hata hivyo aliwataka wananchi hao kutumia haki hiyo kwania njema bila kutumia majina ya watu wengine na waeleze na kufikisha malalamiko ya kweli.
Akibainisha kwamba wananchi wanapoeleza mambo ya kweli ni msaada mkubwa kwa kiongozi mpenda maendeleo na anaejali masilahi ya watu anaowaongoza.
Kwa upande wake mkuu huyo wa mkoa ambae kabla ya kujibu ombi la viongozi hao aliwasimamisha wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya ya Kilwa, walioongozwa na mkurugenzi wao, Zabron Bugingo kujibu malalamiko yaliyokuwa kwenye barua hizo na yale yaliyoelezwa na wananchi kwenye mkutano huo. Aliwaasa wananchi kutowakatisha tamaa watumishi wa umma badala ya kuwatia moyo.
Kwani mengi yaliyosemwa kwenye barua hizo yalikuwa hayana ukweli. Nazilizopo ni changamoto ambazo nyingi zipo nchi nzima (changamoto za kitaifa) ikiwamo upungufu wa watumishi katika idara za afya, elimu na kilimo nk.
Alisema wananchi wanatakiwa kuzichukua na kuziona changamoto kama fursa ya kusonga mbele kimaendeleo. Kwasababu wanatakiwa kuibua miradi ambayo kwakushirikiana na serikali wataziondoa.
"Pamoja na viongozi wenu kuzikana barua hizo lakini wote mmeyasikia majibu ya malalamiko yaliyomo kwenye barua hizo. Kutoka kwa wakuu wa idara, serikali ilichimba visima na kujenga tanki lile pale, simu mnapiga hapa ninawaona na hakuna tishio la usalama, kuhusu watumishi imebainika mnawatumishi mnaafadhali kuliko baadhi ya maeneo mengine. Halafu wanasema wilaya hii inawalimu wa UPE tupu sijui hao walimu wametoka wapi kiasi hicho" alisema Zambi.
Kuhusu ombi la kuwatafuta, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, Zambi alisema nijambo ambalo halihitaji papara na haraka. Bali linahitaji utulivu na busara katika kulipatia majibu. Hatahivyo aliwahaidi atawapatia majibu muda mfupi ujao.
Katika barua hizo ambazo moja ilipelekwa kwa waziri wa TAMISEMI na nyingine kwa Rais. Zilikuwa na malalamiko yanayofanana. Ikiwamo kata ya Lihimalyao, tarafa ya Pande na wilaya ya Kilwa kutupwa na serikali katika kuipatia huduma za msingi na kusababisha wilaya hiyo na mji wa Kilwa kudumaa na kuondoa sifa iliyokuwa nayo kabla ya uhuru.
Madai ambayo yalijibiwa na wakuu wa idara wa halmashauri ya wilaya hiyo, moja baada ya jingine.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.