Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 24
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 24 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA.....!!! “Tupo wapi? Mbona giza? Nini kinaendelea?” aliuliza Sai...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 24
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 24
ILIPOISHIA.....!!!
“Tupo wapi? Mbona giza? Nini kinaendelea?” aliuliza Saida huku akimwangalia mpenzi wake.
“Saida...ni matatizo!” alijibu Kareem.
“Matatizo? Matatizo gani?” aliuliza Saida lakini hata kabla Kareem hajajibu, mwanaume mmoja akatokea na kumtaka anyamaze vinginevyo angempiga risasi kadhaa kifuani. Saida akanyamaza. Mbele yake akakiona kifo na hakujua humo alifikaje.

ENDELEA NAYO SASA.....
Djara yalikuwa mapango makubwa nchini Misri ambayo kwa nje kabisa kulikuwa na bango lililowakataza watu kuingia ndani ya mapango hayo yaliyokuwa na wadudu wengi hatari kama nyonga, ng’e, nyoka na wadudu wengine wengi.

Pamoja na kuweka vizuizi vikubwa lakini Wazungu wengi waliokuwa wakifika nchini Misri, mbali na kutaka kuyaangalia mapiramidi hayo pia walitaka kwenda kwenye mapango ya Djara kwa ajili ya kuangalia kulikuwa na vitu gani humo.

Walitahadharishwa lakini hawakukubali, walitaka kuingia na kujionea kwa macho yao, na walipokuwa wakiingia, hawakuwa wakitoka. Walikufa? Hakukuwa na mtu aliyejua kwani kuhakikisha hilo ilikuwa ni lazima kuingia, na hakukuwa na mtu aliyetaka kuingia.

Hayo ndiyo mapango ambayo walipelekwa Kareem na Saida. Msichana huyo alikuwa kwenye hali mbaya na ndiyo kwanza alirudiwa na fahamu lakini hakukuwa na mtu aliyejali kitu chochote kile, wakamshusha kutoka kitandani na kisha kumsukuma katika mapango hayo.

“Kwa nini mnatufanyia hivi?” aliuliza Kareem huku akiwaomba watu wale wasimtupe mule.
“Kwa sababu nyie ndiyo mliosababisha yote. Ingia humo,” alisema mwanaume mmoja na kisha kumsukuma Kareem ndani ya pango lile, halafu juu wakaweka jiwe kubwa kuhakikisha kwamba watu hao hawawezi kutoka tena.

Ndani ya mapango kulikuwa na giza kubwa, hakuweza kumuona mpenzi wake alikuwa wapi, alitupwa humo lakini hakujua mahali alipokuwa, akaanza kuita kwa sauti kubwa, ilisikuwa ikisikika kama mwangwi, yaani kujirudia mara kwa mara.
“Kareem...” aliita Saida kwa sauti iliyoonyesha kuwa kwenye maumivu makali.
“Upo wapi mpenzi?”
“Nipo huku!”

Kareem akaanza kuelekea kule alipokuwa mpenzi wake, alitembea huku akipapasa, wakati mwingine alikuwa akijigonga kwenye mawe ya mapango hayo, aliumia lakini hakujali, aliendelea kuita mpaka kumfikia Saida aliyekuwa hoi.

Hakuwa na nguvu, alikuwa kwenye hali mbaya mno, hawakuweza kurudi juu kwani ili kufika huko ilikuwa ni lazima kupanda, bila ngazi, wasingeweza hivyo ilikuwa ni lazima kusonga mbele, hawajua wangeishia wapi huko ila ilikuwa ni lazima wafanye hivyo.

Walitembea huku wakiwa wameshikana mikono, hakukuwa na mwanga, walikuwa wakipapasa kila walipopiga hatua. Sauti za popo zilikuwa zikisikika, Saida aliogopa mno, alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake na wakati mwingine aliona huo kuwa mwisho wake.

“Kareem...tunakufa...” alisema Saida huku akilia.
“Hatutokufa mpenzi! Na kama tutakufa, nitafurahi kama nikifa pamoja nawe,” alisema Kareem huku wakiendelea kusonga mbele.

Yalikuwa mapango makubwa mno, walipata tabu sana, walikuwa wakijigonga huku na kule, walichomwa na mawe ya mapango hayo yaliyokuwa yamechongoka, damu ziliwatoka lakini hawakurudi nyumba, mbali na kila kitu, pia kulikuwa na joto kali lililowapa wakati mgumu.

Walitembea hivyohivyo mpaka walipofika katika sehemu ambayo walihisi kwamba kulikuwa na uwazi mkubwa, hawakujua kama sehemu hiyo ilikuwa na bwawa kubwa lililokuwa na mamba wengi ndani yake.

Waliendelea kusogea mbele mpaka walipoyakanyaga maji ya bwawa hilo, hapo ndipo wakajua kwamba walikuwa wamefika sehemu iliyokuwa na maji. Wakati wakijiuliza ni njia gani walitakiwa kupita, wakaanza kusikia vitu vikiingia ndani ya maji, hawakujua kama walikuwa mamba.

“Ni nini hicho?” aliuliza Saida kwa sauti ya kunong’oneza.
“Sijui! Hebu tusonge mbele tutajua huko!” alisema Kareem.
“Hapana! Moyo wangu umekua mzito mpenzi! Nahisi ni kitu hatari.”
“Au popo?”
“Popo kwenye maji? Nahisi kenge au mdudu yoyote mkali,” alisema Saida huku akionekana kuwa na hofu tele.

Walichokifanya ni kupiga hatua kurudi nyuma kuyakimbia maji yale, walitaka kupita sehemu ambayo ilionekana kuwa nafuu kidogo, hivyohivyo kwa kubahatisha wakaipata njia nyembamba ambayo hawakutakiwa kutembea sawa, ilitakiwa mmoja awe nyuma na mwingine mbele.

Wakaelekea huko, joto lilikuwa likiongezeka, hawakujua walikuwa wakielekea wapi, hawakujua kama mbele yao wangeweza kupata msaada wowote ule, walichokuwa wakijua ni kwamba walikuwa wakielekea sehemu ambayo hawakuijua.

Wakati wamepiga hatua kama hatua mia moja, ghafla wakaanza kusikia kundi la popo likitoka mbele yao kuja kule walipokuwa. Walikuwa popo wengi, zaidi ya elfu moja, walikuwa wakisogea kule walipokuwa huku wakipiga kelele.

Wakajikuta wakivamiwa na popo hao na kuanza kushambuliwa. Walipiga kelele za maumivu, popo hawakuwaacha, waliendelea kuwashambulia na kila walivyokuwa wakipiga kelele na ndivyo walivyokuwa wakishambuliwa.

“Tukimbie...” alisema Kareem huku akimshika mkono Saida.

Japokuwa alikuwa na maumivu makali na mwili kukosa nguvu wakaanza kukimbia, Saida alikuwa akilia kwa maumivu makali, kushambuliwa na popo wale walihisi kama wamelowanishwa na maji tena huku wakiwa na maumivu makali, wakajua kwamba hayo hayakuwa maji bali ni damu zilizokuwa zimewatoka kutokana na majeruhi makubwa waliyokuwa nayo.

Walikimbia mpaka sehemu iliyoonekana kuwa kimya zaidi, waliwakimbia popo wale na sehemu waliyofikia wakahisi kwamba walikuwa wakikanyaga vitu chini kama mifupa.

Kareem akainama na kuanza kuvishika vitu hivyo, ilikuwa ni vifupa ya watu, watu waliokuwa wameingia ndani ya mapango hayo na hatimaye kuuawa na wadudu wakali waliokuwa humo.

“Ni nini?” aliuliza Saida.
“Ni miti.”
“Miti?”
“Ndiyo! Ni miti iliyokauka! Tusonge mbele!” alisema Kareem.
Alijua kwamba hiyo ilikuwa mifupa ya binadamu lakini hakutaka kumwambia Saida ukweli, alijua tu kwamba angekuwa na hofu zaidi hivyo ili kumuokoa na kumuondoa hofu ilikuwa ni lazima amdanganye kitu ambacho Saida alikubaliana nacho na kusonga mbele kimyakimya.

“Kareem mpenzi! Hatuta kufa humu kweli?” aliuliza Saida kwa sauti ndogo.
“Hatuwezi kufa, ni lazima tutoke salama humu.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Sijajua tutatoka vipi lakini ni lazima tutoke mpenzi!” alisema Kareem, alijua hatari iliyokuwepo, alikuwa na uhakika kwamba wasingeweza kutoka salama lakini alimwambia hivyo kwa sababu tu alitaka kumfariji.

“Kama nitakufa humu! Naomba uupeleke mwili wangu mpaka nyumbani,” alisema Saida huku akiwa amekata matumaini.
“Huwezi kufa!”
“Kareem! Najua nitakufa tu, siwezi kutoka salama.”

Walitembea kwenda mbele mpaka walipofika sehemu ambayo kulikuwa na mchanga mwingi. Wakasimama kwani kila walipokuwa wakikanyaga mahali hapo ardhi ilibonyea kitu walichohisi kwamba hiyo haikuwa sehemu salama hata kidogo.

Wakati wakiwa mahali hapo, ghafla wakaanza kusikia vitu vikitembeatembea kwenye mchanga huo. Walisimama, hawakutaka kutingishika kwani waligundua kwamba vitu hivyo vilikuwa ni nyoka na kama wangetingishika basi ni lazima wangeng’atwa.

Kila mmoja alikuwa akitetemeka, wakahisi nyoka mmoja akija na kuanza kuzunguka miguuni mwa Kareem, alivumilia, hakutingishika lakini nyoka huyo alipoanza kutembea chini ya Saida, akashtuka na kuanza kupiga kelele, hakutaka kusimama, akaanza kukimbia kusonga mbele, Kareem alipomfuata tu, sehemu ile ikadidimia na kuanza kuingia ndani. Wote wakaanza kuporomoka kuelekea chini huku wakipiga kelele za kuomba msaada.

“Puuu...puuu...” wakatua chini kwa nguvu, sehemu iliyokuwa na mawe mengi. Hapohapo wakatulia kama walivyokuwa, wakapoteza fahamu na hawakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

Je, nini kitaendelea mapangoni?
Je, wataweza kutoka salama?
Usikose Sehemu Inayofuata

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top