Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 18
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 18 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA ......!! “Pumzika kwa amani mpenzi wangu! Imeniuma sana, nimek...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 18
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 18
ILIPOISHIA ......!!
“Pumzika kwa amani mpenzi wangu! Imeniuma sana, nimekosa mtoto, mbaya zaidi nimekupoteza wewe pia...pumzika kwa amani mpenzi!” alisema Kareem huku akimkumbatia Saida kwa nguvu zote, kwake, tayari msichana huyo alionekana kuwa marehemu.

ENDELEA NAYO SASA.....Walinzi walikuwa hotelini wakihakikisha kwamba msichana Saida aliyejulikana kwa jina la Salmah Sadiq Al Muntah anapata kila huduma inayotakiwa kabla ya kuondoka kuelekea nchini Syria siku iliyofuatia.

Walikaa mapokezi huku kila mmoja akiwa makini kabisa lakini kitu cha ajabu, Saida alipotoka ndani ya hoteli hiyo, alipitia palepale walipokuwa na hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba msichana yule aliyeonekana kama mhudumu ndani ya hoteli hiyo alikuwa Saida.

Waliendelea kukaa hotelini hapo mpaka asubuhi ya siku iliyofuata ambapo baada ya kwenda katika chumba hicho na kuanza kugonga, hakukuwa na mtu yeyote ndani aliyeitikia.

Haikuwa kawaida kwani waligonga sana, walihisi kulikuwa na tatizo, hawakufikiria kama Saida alikuwa amelala, walimpa taarifa kwamba siku hiyo alikuwa na safari ya kwenda Syria na isingekuwa rahisi kulala mpaka muda huo.

Walichokifanya ni kuufungua mlango, ulikuwa wazi kabisa, walipoingia ndani, hakukuwa na mtu yeyote yule. Kitandani, hakuwepo, wakaondoka na kwenda bafuni, napo hakuwepo, hata chooni pia, Saida hakuwepo.

Harakaharaka wakawasiliana na wenzao na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea, kila mtu aliashangaa, isingekuwa rahisi namna hiyo kwa msichana huyo kutokuonekana. Kwanza walihisi kwamba alitekwa lakini walipokumbuka usiku uliopita kama kuna mtu alipita na mwanamke pale mapokezi, hakukuwa na tukio hilo.

“Sasa yupo wapi?”
“Labda alikwenda kwenye mgahawa....”

Wakaenda ndani ya mgahawa wa hoteli hiyo, napo hakuwepo. Walichanganyikiwa, wenzao waliowasiliana nao wakafika hotelini hapo, ili kuhakikisha kile walichoambiwa, wakaelekea chumbani, kama ilivyokuwa kwa wenzao, nao hawakuweza kumuona Saida.

Walichanganyikiwa, tayari gari lilikuwa nje likiwasubiri kwa ajili ya kuelekea uwanja wa ndege na kuanza safari ya kuelekea Syria ambayo wala haikuwa mbali kutoka hapo. 

Wakahisi kulikuwa na kitu, hasa kutekwa kwa msichana huyo, walichokifanya ni kuwasiliana na uongozi wa hoteli kwa ajili ya kuangalia kila kitu kilichotokea kupitia katika kamera zilizokuwa humo ndani.

Baada ya kuzungumza na uongozi huo, wakapelekwa mpaka katika chumba kilichokuwa na vijana wa IT (Information Technology) waliokuwa wakishughulika na mambo ya kompyuta na kamera za CCTV zilizokuwa humo hotelini.

Wakaanza kuonyeshea kila kitu kilichotokea usiku uliopita, walimuona mwanaume akiingia, hawakujua alikuwa nani. Mwanaume huyo akaelekea mpaka katika chumba cha Saida na kisha kugonga, msichana huyo alipofungua, wakawaona wakikumbatiana mpaka kutaka kuanguka kisha kuingia ndani.

Baada ya dakika kadhaa, mwanaume akatoka na kuelekea sehemu, hawakujua alikwenda wapi lakini baada ya muda Saida akatoka na kuelekea chooni. Wakati akiwa njiani, wakaisimamisha picha yake, wakavuta macho yake kwa lengo la kuangalia mwanamke huyo alikuwa nani.

Wakamuona akiingia ndani ya choo hicho, hakuchukua muda mrefu akatoka huku akiwa na mavazi yaliyomfanya kuonekana kama muhudumu wa hoteli hiyo. Akaelekea nje, kamera ziliendelea kumuonyesha mpaka alipoingia ndani ya gari moja na kuondoka mahali hapo.

Walichokifanya ni kuwasiliana na polisi, walitaka kujua mwanamke huyo alikuwa nani, picha ile ya macho itumwa katika kitengo cha polisi kwani walihisi mwanamke yule alikuwa mbaya.

Polisi wakaichukua picha ile na kuiweka katika kompyuta yao iliyokuwa na data za watu wote waliokuwa wakitafutwa ndani ya nchi hiyo. Wakaanza kuisaka picha halali ya mtu huyo.

Haikuwa kazi rahisi, picha zote za wahalifu zilipita lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye macho yake yalishabiiana na macho ya msichana huyo.

Walipoona wameshindwa kumpata nchini mwao, walichokifanya ni kuanza kuwatafuta wahalifu waliokuwa wakitafutwa katika nchi za Kiarabu. Kulikuwa na wahalifu, magaidi wengi kutoka sehemu mbalimbali, walitafuta na kutafuta na mwisho wa siku picha iliyoshabiiana na macho yale ilikuwa ni ya Saida, mwanamke aliyekuwa akitafutwa sana nchini Oman.

“Wapigie simu!” alisema mkuu wa kitengo cha upelelezi.
Harakaharaka simu ikapigwa mpaka Oman na kuwaambia kwamba mwanamke waliyekuwa wakimtafuta, Saida alikuwa nchini Iran na ndiye yule ambaye alijulikana kwa jina la Salmah Sadiq Al Muntah aliyeshinda shindano la kusoma aya nchini Iran.

Waliposikia, hawakuamini hata kidogo, walichokifanya wao wenyewe ni kuchukua video za msichana huyo na kufananisha na Saida, kweli, macho yaliendana, alikuwa msichana yuleyule kwani hata kompyuta iliandika MATCH 100% kwamba ilifanana kwa asilimia mia moja.

Walimsifia kwa kazi nzuri lakini ghafla, wakamchukia, msichana huyo hakutakiwa kupendwa kwani bado alionekana kuwa mtu mwenye dhambi kubwa ambaye hakutakiwa kuishi kabisa katika dunia hii.

Kwa kuwa wanajeshi wao bado walikuwa nchini humo, wakatumwa kwenda katika hoteli hiyo, wahudumu walipoulizwa, hata nao hawakuwa wakijua, ni mhudumu mmoja tu ndiye aliyekuwa akifahamu, hakutaka kujitokeza kwani hata yeye mwenyewe hakujua mavazi aliyokuwa amempa mwanaume aliyemuomba yalikuwa ya kazi gani.

Kwa sababu kulikuwa na mawasiliano na chuo kilichokuwa katika Msikiti wa Masdaq ambao ndiyo uliowachukua wanawake wale ishirini na tano, wakawasiliana nao kutaka kujua kuhusu msichana huyo, ilikuwaje mpaka awe katika kundi lao la wale wanawake waliokuwa katika maulidi ile.

Imamu wa msikiti huo alipoulizwa, akalipeleka swali kwa mwalimu wa madrasa ambaye alisema wazi kwamba hakujua kuhusu mwanamke huyo, alichukulia kitu kuwa kawaida kwa kuwa aliamini kwamba inawezekana Mungu alimtuma malaika wake kwa ajili ya kuzungumza nao.

“Sikuwa na hofu, nilihisi labda Mungu alimtuma malaika kwa ajili ya kuzungumza nasi,” alisema mwalimu wa chuo hicho.
“Kwa hiyo hukujali!”
“Kwa kweli sikujali!”
“Na wanawake waliorudi walikuwa wangapi?”
“Ishirini na tano!”
“Sasa yule mmoja alitoka wapi?”
“Ndiyo maana ninakwambia inawezekana Mungu alimtuma malaika wake kwani hata alipoingia ndani ya gari hakukuwa na mtu aliyemuona,” alisema mwalimu huyo.

Polisi wakajua kwamba kuna uwezekano mkubwa Saida akawa bado ndani ya nchi hiyo, wakaunganisha nguvu zao na kuendelea kumtafuta msichana huyo, siku zilikatika lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, walihangaika kila sehemu lakini hawakuweza kumpata Saida kitu kilichowakasirisha kila siku, yaani walisumbuliwa na msichana asiyekuwa polisi wala jasusi, ila kila walipomtafuta, waliambulia patupu.

**********************************
“Unakumbuka ubaya ulionitendea?” aliuliza Mzee Faraq wakati akizungumza kwenye simu na bilionea kutoka nchini Oman, Mzee Abdulaziz.
“Hakuna ubaya niliokutendea, yalikuwa ni mambo ya biashara tu!” alijibu Mzee Abdulaziz.
“Kwako uliona ni mambo ya biashara, ila kwangu, yalikuwa ni mambo ya ubaya. Nilikutafuta sana, ukajifanya mjanja, kila sehemu ukajificha lakini nimepata kile unachokithamini,” alisema Mzee Faraq kwa mbwembwe.
“Kitu gani?”
“Ninaye mtoto wako, Kareem.”
“Unasemaje?”
“Ninahitaji uje Misri na dola milioni hamsini na tano kwa ajili ya kumchukua mtoto wako. Ulijifanya mjanja, sasa ni muda wako kutumia kiasi cha fedha kwa ajili ya kuiokoa damu unayoipenda,” alisema mzee huyo.

Mzee Abdulaziz akachanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, moyo wake ulishtuka kusikia kwamba mtoto wake, Kareem alikuwa mikononi mwa mzee huyo ambaye alikuwa mtu katili, aliyependa kuua hasa pale alipoona kama akifanya hivyo basi angepata kiasi fulani cha fedha.

Alimfahamu vilivyo, hakuwa mzee wa utani hata mara moja, hakutaka kukubali, akamuomba sana msamaha kwamba amuachie mtoto wake lakini mzee huyo akagoma na kuongezea kwamba kama angejiifanya kuwataarifu polisi basi angemuua mtoto wake hata kabla hajafika nchini Misri.

“Unatakiwa kuja huku kesho. Saa sita kamili utatakiwa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Qatar Ailines utakuja huku ukiwa na fedha hizo ambazo utakuwa nazo mikononi mwako. Humo ndani ya ndege, kuna vijana wangu wawili, wao watakuwa wakikuangalia kila kitu unachokifanya ndani ya ndege. 

Utakaposhuka, kuwa makini, vijana hao watakufuata na kisha kuchukuana nao mpaka kwenye gari litakalokuwa nje likiwasubiri, mtapanda na kuja huku. Umesikia?” aliuliza mzee Faraq.
“Ndiyo! Lakini huwa sipandi ndege za umma.”
“Utatakiwa kupanda kipindi hiki! Vijana wamejiandaa na saa sita watakuwa ndani ya ndege hiyo. Usijali. Ushakatiwa tiketi yako,” alisema mzee huyo na kukubaliana na Mzee Faraq ambaye alionekana kuwa na hofu, japokuwa mbele yake aliiona hatari kubwa, hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana naye. 

Hakumwambia mkewe, siku iliyofuata, akaelekea uwanja wa ndege, akakutana na vijana hao waliompa tiketi na kisha kuingia ndani ya ndege.

Ilimuuma sana kupanda ndege za umma lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana na kila kitu kwani vinginevyo mtoto wake, Kareem angeuawa huko.

******************************
“Sir, we have to do something...” (mkuu, tunatakiwa kufanya jambo)
“What is it?” (jambo gani?) aliuliza mkuu wa majeshi nchini Marekani aliyekuwa makao makuu ya kijeshi nchini humo, Pentagon.
“We have lost B-2 Spirit in Oman,” (tumeipoteza ndege ya kijeshi ya B-2 Spirit nchini Oman) alisikika mwanaume akizungumza upande wa pili.

B-2 Spirit ilikuwa ndege kubwa ya kijeshi ambayo ilikuwa ni ya gharama kubwa kuliko ndege zote za kijeshi duniani. 

Ndege hiyo baada ya kuondoka huko kwa ajili ya kuelekea katika kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Oman kilichokuwa kilometa mia mbili kutoka katika Jiji la Muscat, ikatunguliwa na kundi la kigaidi la ISIS kwa kutumia mtambo mkubwa wa rada ambapo ndege hiyo ikashushwa mpaka chini pasipo kulipuka.

Waarabu hao wakaiangalia ndege hiyo, ilikuwa kubwa, yenye mitambo mikubwa, hakukuwa na kitu chochote walichokuwa wakikifahamu, kwa jinsi ndege ile ilivyotengenezwa, ilitumia ufundi mkubwa mno. 

Walipoona wameshindwa, wakawasiliana na Urusi na China kwa ajili ya kupeleka watu wao nchini Oman, waiangalie ndege hiyo, utaalamu uliotumika kutengenezwa ili wajue namna ya kupambana na Mmarekani kwa kutumia ndege nyingi ambazo zitatengenezwa kama ndege hiyo ya gharama duniani.

Ndani ya saa nne, wataalamu wa kijeshi wa Urusi na China wakafika nchini humo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuifungua ndege hiyo vifaa vyote na kuanza kuangalia teknolojia iliyokuwa imetumika.

Ilikuwa ngumu kugundua, walichokifanya ni kuwasiliana na nchi zao na kuwaambia kile kilichokuwa kikiendelea. Wote wakakubaliana ndege hiyo ifunguliwe na vifaa vya ndege hivyo visafirishwe na kupelekwa nchini China ambapo wangeita wataalamu zaidi wa kuichunguza ndege hiyo.

“Wazo zuri sana, ileteni China,” alisema kiongozi wa China baada ya kukubaliana na Urusi vifaa vya ndege hiyo kuelekea China. Ilitakiwa kutumwa na wataalamu kumi na mbili ambao walifika Oman kwa ajili ya kuipekua ndege hiyo.

Je, nini kiliendelea?
Je, ndege ya Marekani inahusika nini na tukio zima la kutekwa kwa Kareem na Saida?
Je, Saida atakufa?
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top