Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 08
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 08 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA......!!! Hassan akainamisha kichwa kwa sekunde kadhaa. Alipokii...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 08
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 08
ILIPOISHIA......!!!
Hassan akainamisha kichwa kwa sekunde kadhaa. Alipokiinua, alikuwa na wazo jingine kabisa ambalo lilimshtua na kumshangaza kila mmoja. Hata kama lilionekana kuwa la hatari, hawakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kulitekeleza haraka iwezekanavyo.

ENDELEA NAYO SASA....
“Endesha kuingia kwenye jumba la Yasmir Al Fattar,” alisema Hassan.
“Unasemaje?” aliuliza Hussein, si yeye tu aliyeshtuka bali hata Yasmin.

“Ingiza gari humo!”
“Kuna laana!”
“Usiamini ujinga huo. Hakuna kitu kama hicho! Ili tuyaokoe maisha yetu ni lazima tuliingize gari humo,” alisema Hassan.

Hawakuwa na jinsi, hiyo ndiyo ilikuwa njia nyepesi ya kuwaepuka polisi hao waliokuwa wakiwafuata kwa kasi, alichokifanya Hussein ni kulipeleka gari katika jumba hilo. Akalibomoa geti na kuingia ndani, polisi hawakuwafuata, wakalisimamisha gari lao nje ya jumba hilo.

“Mungu wangu! Wameingia humu!” alisema polisi mmoja huku akionekana kutokuamini alichokiona.

Gari lilipoingia ndani ya jumba hilo, hapohapo likasimama, mafuta yalikuwa yamekwisha, walichokifanya ni kuteremka na kuanza kuelekea nyuma ya jumba hilo huku polisi wakiwa wamebaki upande wa mbele wakiwasiliana na polisi wenzao.

Walipofika nyuma ya jumba lile, wakachukua mawe yaliyokuwa pembeni na kuyapanga. Hawakuwa na haja ya kuingia ndani kabisa, walitaka kupita kupitia katika jumba hilo lililoogopwa na watu wote wa Oman.

Kwa muonekano wa jumba lile ilionyesha ni jinsi gani halikuwa likikaliwa na mtu. Kulikuwa na uchafu mwingi, vumbi, kuta za nyuma zilikuwa na nyufa, hali iliyokuwa humo ndani ilionyesha kabisa kwamba jumba hilo lilitelekezwa.

Hawakutaka kubaki ndani, walichokifanya ni kukimbia na kuelekea nyuma ya jumba lile kulipokuwa na ukuta, walichokifanya ni kubebana na kuuruka ukuta huo na kutokea upande wa pili ambapo kulikuwa na uwanja mkubwa uliokuwa na michanga mingi.

Hawakutaka kusimama, waliendelea kusonga mbele mpaka walipofika katika barabara kubwa iliyokuwa katika Mtaa wa Al Manhel ambapo wakapitiliza mpaka katika barabara ya lami ambapo pia kulikuwa na barabara ya vumbi iliyoelekea upande wa Kaskazini.

“Twende wapi?” aliuliza Hussein.
“Barabara ya vumbi!”

Walichokifanya, kwa sababu walijua kwamba walikuwa wakitafutwa na polisi na hata barabarani kulikuwa na watu wengine, wakawa wanatembea kwa mwendo wa kawaida, hawakutaka kushtukiwa hata kidogo.

Hakukuwa na mtu aliyemgundua Saida hata kama barabarani kulikuwa na picha zake, nikabu aliyokuwa ameivaa ilimsaidia kutokugundulika. Walikwenda kupitia mtaa huo kwa lengo la kwenda kule Al Khuwair kwa ajili ya kuonana na Kareem.

Walitembea na hiyo barabara mpaka walipofika katika Soko la Tarakabat ambapo kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakifanya manunuzi kwa ajili ya mfungo wa Ramadhan ambao ulitarajiwa kuanza siku inayofuata.

Hawakutaka kuzungumza na mtu yeyote zaidi ya kuendelea mbele ambapo kulikuwa na kituo cha mafuta cha Ya Arabya Oil ambacho ndicho kilichokuwa kikisambaza mafuta hapo Oman. Wakaenda mbele zaidi na kuchukua Barabara Kuu ya Mohammed Al Yameen ambayo ndiyo iliyokuwa ikiuganisha na barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa ikielekea katika Kiwanda cha Al Khuwair.

“Yule kule,” alisema Hussein mara baada ya kumuona Kareem akiwa pembeni ya gari lake, palepale walipomuona kipindi cha nyuma.

Wakamfuata. Kwa furaha aliyokuwa nayo Kareem, akamfuata Saida na alipomfikia, akamkumbatia. Hakuamini kama angemuona tena msichana wake aliyekuwa akimpenda.

Alimbusu japokuwa ndani ya nchi hiyo halikuwa jambo lililoruhusiwa kumbusu mwanamke kama alivyokuwa akimbusu Saida.

“Nashukuru sana kwa msaada wenu,” alisema Kareem, akaufungua mlango wa gari, akatoa bahasha ya kaki ambayo ndani yake ilikuwa na burungutu za fedha na kuwapa.

“Tunashukuru sana!” aliitikia Hassan na kuondoka mahali hapo huku wakijiona matajiri.

Kareem na Saida wakaingia ndani ya gari, kitu alichokuwa akikifikiria mwanaume huyo kilikuwa ni kuondoka kueleka katika bandari ya Sultan Qapoos ambayo ilikuwa kama kilometa kumi na mbili kutoka hapo walipokuwa.

Tayari alikwishafanya mawasiliano na rafiki yake mwingine, Yusuf Al Sadiq ambaye alimuahidi kwamba angekamilisha safari ya mpenzi wake kuelekea Dubai. Akamwambia Saida mpango wake kwamba ilikuwa ni lazima aondoke kuelekea huko kwani kwa Oman, kwa kipindi hicho haikuwa salama kabisa kwa maisha yake.

“Niende peke yangu?” aliuliza Saida.
“Ndiyo! Sitoweza kwenda nawe...” alijibu Kareem.
“Kwa nini?”

“Kwa sababu natakiwa kurudi nyumbani. Tukio lililotokea ni kubwa sana, kama polisi watakuja nyumbani na kunikosa, moja kwa moja watajua kwamba mimi ndiye nilihusika katika kukutorosha. Ni lazima nirudi ila na mimi nitakuja Dubai kesho kuonana nawe,” alisema Kareem.

Nikifika Dubai, nitaelekea wapi?”
“Kuna mtu atakuja kukuchukua!”
“Nani?”
“Ndugu yangu!”
“Una uhakika na huyo ndugu yako? Asije naye akaniuza!”
“Hakuna kitu kama hicho!”

Wakati wakizungumza hayo tayari walianza safari ya kuelekea katika bandari hiyo. Mwendo waliotumia ulikuwa ni wa kawaida tu. Hawakutaka kutumia barabara kubwa kwa kuhisi kwamba huko ni lazima kungekuwa na ulinzi mkubwa na kila mtu angekuwa makini barabarani.

Walipita katika barabara za mitaani, kutokana na gari alilokuwa akilitumia kuwa la kifahari, hawakupata usumbufu wowote kutoka kwa askari wa barabarani ambao waliamini kwamba mtu aliyekuwa akitumia gari hilo alikuwa tajiri mkubwa.

Walikwenda mpaka walipofika katika makutano ya barabara mbili kubwa, Barabara ya Al Ghubrah na Dohat Al Adab, wakaunganisha mbele mpaka walipofika katika Hospitali ya Taifa ya Al Hayat ambapo hapo wakachukua Barabara ya Al Marafah, walisonga mbele zaidi.

Kwa sababu walitaka kutumia barabara zisizokuwa na ulinzi mkubwa, iliwabidi kuzunguka sana kiasi kwamba Said alichoka na kila alipomwambia kama walikaribia, alijiwa kwamba safari ilikuwa ndefu.

Dakika hamsini baadaye ndipo wakaingia Barabara ya 18th November ambayo iliwapeleka mpaka katika Shule ya Bangladesh Muscat ambapo wakaingia katika Barabara ya mwisho ya Sultan Qaboos ambayo iliwapeleka mpaka katika bandari hiyo.

Walipofika, Kareem akachukua simu yake na kumpigia rafiki yake Yusuf Al Sadiq ambaye ndiye alimuahidi kwamba angemsaidia kumsafirisha Saida kimaficho mpaka Dubai. Akaanza kuzungumza naye kwenye simu, walipokubaliana, wote wawili wakateremka na kuanza kulifuata geti kubwa jeusi na kuingia ndani.

“Umefanya vizuri kuja,” alisema Yusuf Al Sadiq huku akiachia tabasamu pana.
“Kwa nini?”
“Kuna meli yangu inaelekea Dubai kupeleka mzigo leo hii. Tutamsafirisha humo,” alisema Yusuf Al Sadiq.

Hakuwa na jinsi, japokuwa wakati mwingine alihisi kama rafiki yake huyo angemsaliti kama alivyosalitiwa mwanzo lakini akakubaliana naye na hivyo kumvuta Saida pembeni na kuanza kuzungumza naye.

Muda wote Saida alionekana kuwa na huzuni, hakuwa na uhakika kama angefika salama huko Dubai, alimwangalia mpenzi wake huku macho yake yakionyesha hofu kubwa.

“Najua unahofu lakini naomba tuwe na nafasi ya kumuamini Yusuf Al Sadiq. Hatuna jinsi mpenzi,” alisema Kareem.
“Sawa. Haina shida. Kama umemuamini, sina budi kumuamini pia,” alisema Saida.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, alichokifanya Kareem ni kuondoka na kurudi nyumbani huku akimuacha Saida mikononi mwa Yusuf Al Sadiq. Wakati akiwa njiani, ghafla akaanza kusikia ving’ora vya magari manne ya polisi likielekea kule alipotoka.

“Mmh!” alijikuta akiguna, wakati huo, geti la kuingia katika bandari hiyo likafunguliwa. Akahisi kuna tatizo, hakutaka kuondoka, alichokifanya ni kuligeuza gari lake na kuanza kurudi hukohuko. Alichohisi ni kwamba hata rafiki yake, Yusuf Al Sadiq alikuwa amemsaliti kama alivyomsaliti Al Khalid.

Je, nini kitaendelea? Usichoke Tukutane Kesho Saa Moja Kamili Asubuhi

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top