SAMIA – OLE WENU MNAOKWAMISHA WAWEKEZAJI NCHINI

SERIKALI itawachukulia hatua kali watumishi wake wanaozungusha wawekezaji kiasi cha kuwafanya waondoke na kunyima fursa ya wananchi kupata maendeleo kwa kutumia rasilimali zilipo nchini.
Samia Suluhu
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) kwenye maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
“Tumeshuhudia kukimbiwa na wawekezaji kadhaa kwa sababu mwekezaji anakuja anataka kuwekeza Tanzania, miaka mitatu hajapata jawabu kama ndio wekeza au toka nenda zako, anazungushwa anapigwa taasisi moja kwenda nyingine, hili lifike mwisho,” alisema.

Samia alisema serikali itakuwa makini sana kusimamia suala hilo kwa nguvu, kutokana na kwamba kumekuwa na upotevu mkubwa wa uwezeshaji katika uchumi wa nchi.

Alitaja pia kuwa tatizo la rushwa kuwa moja ya sababu inayowakimbiza baadhi ya wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini na kwamba wekezaji wanaotajwa kukimbia kuwekeza nchini wengi wao ni wanaogoma kutoa rushwa ili kupata majibu ya kama wanaruhusiwa au hawaruhusiwi kuwekeza na hufanya hivyo wanapotakiwa kuhonga.

Samia alisema azma ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda mwaka 2025 kwa kutumia rasilimali za ndani itawezekana kama watumishi waliokabidhiwa dhamana ya kukusanya mapato na kusimamia matumizi ya fedha za Serikali watazingatia maadili ya utendaji kazi na kuweka mbele maslahi ya umma.
“Viongozi wa Umma wasimamie vema watumishi walio chini yao, kuna mtindo katika baadhi ya ofisi za Serikali kufanya kazi zao bila kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya huduma kwa wateja…hili ni tatizo kubwa ndani ya Serikali yetu,” alisema.
***********

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post