Mapema leo serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali kuanzia Aprili 26 hadi 29 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba huku mvua hizo zikitarajiwa kusambaa katika mikoa ya Kilimanjaro na Mashariki mwa Manyara.
“Asiyesikia la Mkuu huvunjika guu!” usemi huu wa zamani wa wahenga umetimia mara kadhaa katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine hapa nchini baada ya kupewa tahadhari na serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Maeneo ya bondeni na yenye mkondo wa maji kama vile Jangwani, Kigogo, Bonde la Mto Msimbazi, Boko, Kawe Ukwamani na kwingineko yamekuwa ni miongoni mwa waathirika wakubwa wanaopuuzia taarifa hizi na matokeo yake wakakumbwa na majanga ya mafuriko yaliyoleta athari ya kupoteza thamani mbalimbali pamoja na vifo.