Baadhi ya Wakazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam wakiitikia wito wa Rais John Pombe Magufuli wa kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania Bara unafanyika kila mwaka tarehe 9 Desemba kwa kufanya usafi katika maaeneo yao.
Mafundi Pikipiki katika Kata ya Kitunda jijini Dar es Salaam wakizoa takataka ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kufanya usafi katika maeneo yao ikiwa ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.
Na Benedict Liwenga, Dar es Salaam
Wakazi wa Kata ya Kitunda Kati Jijini Dar es Salaam wameitikia wito wa kufanya usafi katika maeneo yao ikiwa ni siku ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania inayofanyika kila mwaka tarehe 9 Desemba.
Akiongea na Lindiyetu.com leo kwa niaba ya wakazi wa eneo lake, Mjumbe wa Nyumba Kumi Bi. Zahara Idrissa ameeleza kuwa kauli ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli la kuwataka Watanzania wote nchini kuadhimisha Sherehe za Siku ya Uhuru kwa kufanya usafi katika maeneo yao ni suala muhimu kwakuwa linasaidia katika kuepukana na magonjwa ya milipuko ukiwemo ugonjwa wa Kipundipindu ambao umeshika kasi nchini.
Bi. Idrissa amesema kuwa kwa kufanya usafi katika maeneo ya makazi kutawafanya watu wengi kujitambua na kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo ili kuepukana na magonjwa hatari, hivyo wao wameamua kuitikia wito huo kwa dhati na kushirikiana kwa bidiii kuifanya kazi hiyo.
Ameongeza kuwa, suala la kufanya usafi katika makazi nchini kote liwe endelevu kwani haitakuwa na maana kufanya hivyo siku moja tu ya Uhuru kama kumpendezesha Rais.
‘’Hili suala la usafi ni zuri sana na linaboresha mazingira yetu na linawafanya watu wajielewe kwa kuishi katika mazingira yaliyosafi na salama ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa hasa ya milipuko, lakini kuna watu wengine wanakuwa wabishi wa kufanya usafi hivyo hatunabudi kuwahimiza watu wa namna hii’’, alisema Bi. Idrissa.
Aidha, ametoa ushauri kwa Serikali ya Awamu ya Tano ya kutaka suala la usafi liwe la mara kwa mara ikiwezekana kila siku za Jumamosi watu wawe wanafanya usafi na kwa kufanya hivyo magonjwa kama vile Kipindupindu na malaria vitatoweka.
Mkazi wa Kivule Bwana Yusuph Mateka ambaye ni Fundi pikipiki katika eneo la Kitunda Shule anafafanua kuwa, suala la kufanya usafi ni jambo zuri lakini changamoto iliyopo ni magari ya kuzoa taka yamekuwa hakuna katika maeneo yao hali ambayo inawafanya wafanya usafi kulundika taka eneo moja bila kuzipeleka kunakohusika.
‘’Kwa kifupi hali iliyoko ya uchafu jijini Dar es Salaa imekithiri lakini kama zoezi hili la ufanyaji wa usafi litakuwa enedelevu basi litasaidia kuondokana na maradhi hasa ya kipindupindu, hivyo mimi nampa pongezi sana Mhe. Magufuli kwa wazo hili zuri alilotuletea sisi Watanzania".
Watanzania leo wanashiriki katika kufanya usafi kwenye maeneo yao ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara ambayo kwa mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamua itumike kwa kufanya usafi nchini kote ili kuepukana na magonjwa ya kipindupindu yatokanayo na uchafu.