
Pichani ni mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombare
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru ametamka ya kwamba Chama Cha Mapinduzi(CCM) kamwe hakiwezi kuepuka makundi ya urais kupitia chama hicho wakati kikielekea katika hatua za ukingoni za kulipata jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya urais katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa hata miaka ya nyuma yalikuwepo.Kauli ya mwanasiasa huyo inakuja wakati kamati kuu ya chama hicho ikikutana mjini Dodoma kuandaa ajenda za mkutano wa halmashauri kuu ya CCM huku ajenda ya jina la nani atakayekipa ushindi mwaka huu katika nafasi ya urais ikitajwa kutawala katika mkutano huo.
Mwanasiasa huyo alitoa kauli hiyo juzi wakati akihojiwa katika kipindi cha uzalendo kinachorushwa na luninga ya ITV wakati akizungumzia makundi ya urais ndani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu.
Akihojiwa katika kipindi hicho alisema kuwa CCM hakiwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila ya kuwa na makundi kwa kuwa makundi hayo yalianza tangu mwaka 1995 hadi sasa.
“Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi wa kidemokrasia bila ya kuwa na makundi,mwaka 1995 kila mgombea alikuwa na kundi lake na mwaka 2005 tulikuwa na makundi hata mwaka huu unayo makundi”alisema Mwiru
Alisema kuwa katika mfumo wa kidemokrasia ndani ya chama unaruhusu makundi kwa kuwa kila mgombea anakuwa na kundi lake ambalo linamjenga na kutoa ushawishi katika harakati mbalimbali.
Alisema kuwa kuna tofauti kubwa kati ya makundi ya urais ya mwaka 1995 na ya mwaka 2015 kwani miaka hiyo makundi yalikuwa ni ya kawaida tu tofauti na sasa ambapo baadhi ya wanachama wamekuwa na mitizamo hasi .
Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa mbali na makundi hayo mwisho wa siku ni lazima apatikane mgombea mmoja ambaye atakubalika nje ya CCM.
“Mwisho wake ni lazima apatikane mmoja kupitia vikao vya CCM na anayekubalika na wengi ndani ya CCM ndiye atakayekubalika nje ya CCM hiyo ndiyo demokrasia”alisisitiza Mwiru
>>(Habari na jamiiblog)
Tags
HABARI ZA KITAIFA