Unknown Unknown Author
Title: PRESS RELEASE - UFUNGUZI WA MSIMU WA MAUZO YA KOROSHO GHAFI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
BODI YA KOROSHO TANZANIA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI (PRESS RELEASE) UFUNGUZI RASMI WA SOKO LA KOROSHO NA BEI MWONGOZO YA ZAO LA K...
BODI YA KOROSHO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS RELEASE)
UFUNGUZI RASMI WA SOKO LA KOROSHO NA BEI MWONGOZO YA ZAO LA KOROSHO MSIMU WA 2014/2015

1.0 UTANGULIZI
Wadau wa Tasnia ya Korosho walifanya mkutano wao Mkuu wa Mwaka 2014 kuanzia tarehe 09 - 10 Agosti, 2014 mjini Masasi. Pamoja na mambo mengine Wadau walijadili na kukubaliana bei mwongozo ya kuuzia/kununulia zao la korosho kwa msimu wa 2014/2015. Aidha, walikubaliana kuhusu utaratibu utakaotumika katika mauzo ya korosho katika msimu husika. Nachukua fursa hii kutangaza bei na utaratibu ambao umekubaliwa kama ilivyoagizwa na wadau wenyewe.

2.0 BEI MWONGOZO YA KOROSHO MSIMU WA 2014/2015
Wadau wamekubaliana kwamba bei mwongozo kwa kilo moja ya korosho ghafi daraja la kwanza (Standard Grade) itakuwa shilingi 1,000/= na kilo moja ya korosho za daraja la pili (Under Grade) itakuwa shilingi 800/=. Bei hii ni ya mwongozo tu kwani bei halisi itapatikana sokoni. Bei ya soko inaweza kubadilika kutegemeana na nguvu za soko (mahitaji na ugavi).

3.0 UFUNGUZI RASMI WA MSIMU WA 2014/2015
Msimu wa 2014/2015 utafunguliwa rasmi tarehe 20 Agosti, 2014. Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wadau wote wanaohusika na uuzaji/ununuzi wa zao la korosho kukamilisha maandalizi ya msimu kabla ya tarehe ya ufunguzi rasmi. Wadau hao ni pamoja na wakulima, Vyama vya Msingi vya Ushirika, Vyama Vikuu vya Ushirika, watunza maghala, wasafirishaji, mabenki na wengine wote ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine. Msimu huu unafunguliwa mapema ili kuitumia vizuri fursa tuliyonayo ya kuvuna mapema zao la korosho ukilinganisha na nchi nyingine zinazolima korosho duniani. Hivyo vyama vikuu vya ushirika na wale wote wanaosimamia usambazaji wa magunia wanatakiwa kupeleka magunia maeneo ambayo korosho zimeanza kuvunwa ili vyama vya msingi vianze kukusanya korosho na kupeleka kwenye maghala kwa ajili ya mauzo.

4.0 UTARATIBU WA MAUZO
Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho umekubaliana na kusisitiza kwamba kila mdau azingatie taratibu zinazoongoza ununuzi/uuzaji wa zao la korosho. Utaratibu wa mauzo ni kama ifuatavyo:-
(i) Mfumo wa Stakabadhi Ghalani utaendelea kutumika na mauzo ya korosho yatafanywa kwa zabuni.
(ii) Sanduku la zabuni litatunzwa katika ofisi husika za vyama vikuu vya ushirika.
(iii) Zabuni zitapokelewa siku moja kabla ya siku ya mnada kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni na mnada utafanyika siku inayofuata saa 4:00 asubuhi.
(iv) Zabuni zote zitatakiwa kuchapwa kwa kompyuta au mashine kwa kutumia karatasi yenye nembo ya kampuni.
(v) Zabuni zote zitatakiwa kufungwa kwa lakiri (‘seal’).
(vi) Minada itafanywa na kamati ya mauzo itakayojumuisha wadau mbalimbali na kusimamiwa na Bodi ya Korosho Tanzania.
(vii) Ufunguzi wa zabuni utashuhudiwa na wawakilishi wa wakulima na wanunuzi waliowasilisha zabuni hizo.
(viii) Baada ya kushuhudia ufunguzi wa zabuni, wanunuzi watatakiwa kuondoka ili mjadala wa kuwapata wanunuzi ufanyike, na
(ix) Baada ya kuwapata wanunuzi, Bodi ya Korosho Tanzania kupitia vyombo vya habari itatangaza bei na kiasi cha korosho kitakachonunuliwa kwenye mnada. Taarifa za kina kuhusiana na matokeo ya mnada zitabandikwa katika mbao za matangazo zilizopo katika ofisi za vyama vya ushirika husika.

5.0 UTOAJI WA LESENI
Katika miaka ya hivi karibuni, leseni za biashara zilikuwa zinatolewa bila malipo. Kwa mujibu wa Sheria ya fedha Na. 5 ya mwaka 2011 kuanzia msimu huu leseni za ununuzi wa korosho zitatolewa kwa kulipia ada ya leseni ambapo wanunuzi wa ndani watalipia shilingi 750,000/= kwa mwaka na wanunuzi wa nje watalipia Dola 500 za Marekani kwa mwaka.
Hivi sasa wanunuzi wanakaribishwa kuja kukata leseni kwa ajili ya msimu wa 2014/2015 katika ofisi za Bodi ya Korosho Tanzania.

6.0 HITIMISHO
Ni matarajio yetu kwamba wadau wote watatekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuhakikisha kwamba kila mmoja ananufaika na biashara hii ya korosho.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
MWENYEKITI WA BODI
AGOSTI, 2014

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top