POLISI jijini Dar es Salaam imewataja watu 10 waliokufa kutokana na mafuruko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, waliofariki kutokana na mafuriko hayo ni Julius Josephat (25), mkazi wa Pugu Kinyamwezi; Agatha Thomas (8), mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya High Mountain iliyopo Pugu; mtoto Josephat Jaffet mwenye umri wa mwaka na nusu, mkazi wa Buguruni; Juma Said anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40-45, mkazi wa Jangwani Mafuso na mwanaume mlemavu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35-40 ambaye maiti yake imeokotwa Mto Msimbazi, maeneo ya Gongo la Mboto.
Wengine ni Bakari Juma anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 7 hadi 10, ambaye maiti yake imekutwa eneo la Kisiwa cha Bongoyo na Richard Yohana Chipalo (30), fundi ujenzi na mkazi wa Kinyerezi ambaye alifariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kukanyaga waya wa umeme, hivyo kupigwa shoti na kufariki dunia.
Polisi imemtaja pia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Mkojan anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40 ambaye maiti yake ilikutwa eneo la Jangwani karibu na Kanisa la Milima ya Baraka; mtoto wa kiume ambaye jina lake halikufahamika, aliyekutwa Mto Msimbazi, maeneo ya Msimbazi Centre na mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 40 ambaye maiti yake ilikutwa maeneo ya Kimara Bonyokwa.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo vifo zaidi kwani wapo watu waliopotea ambao hadi sasa hawajulikani walipo, lakini wanahofiwa kufa maji.
Mbali ya kusababisha vifo hivyo, mvua hizo pia zimesababisha miundombinu ya barabara kuharibika na umeme kukatika katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakati huohuo, daraja la Mzinga, lililopo Mbagala Kongowe, Dar es Salaam limekatika juzi jioni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.