Unknown Unknown Author
Title: MATUKIO MBALIMBALI KUELEKEA MIAKA 50 YA MUUNGANO KUFANYIKA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Msemaji wa Serikali  Bw. Assah Mwambene akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Na. Aron Msigwa - MAELEZO. SERIKALI i...

clip_image001Msemaji wa Serikali  Bw. Assah Mwambene akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam.

Na. Aron Msigwa - MAELEZO.

SERIKALI imetoa wito kwa wananchi na vyombo vya habari kushiriki katika shughuli na matukio  mbalimbali ya  maadhimisho ya Sherehe za miaka 50 ya Muungano  yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 26,April 2014,  siku ya maadhimisho ya sherehe hizo.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Msemaji wa Serikali  na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni ya kipekee yanaongozwa na kauli mbiu isemayo Utanzania wetu ni Muungano Wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha  yanaambatana na matukio mbalimbali yanayozihusisha wizara na taasisi mbalimbali za Muungano.

Amesema wizara na taasisi hizo zitashirikiana na vyombo vya habari kutoa  elimu kwa wananchi  kuhusu  mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chote cha uhai wa Muungano ikiwemo umoja, amani na mshikamano.

“Sisi tumeungana miaka 50 iliyopita,huu ni muungano pekee uliobaki Afrika wa kupigiwa mfano na unaoendelea kudumu haya ni mafanikio makubwa “ amesema.

Ameeleza kuwa katika  kipindi chote cha muungano watanzania wamebaki kuwa wamoja kwa kuhakikisha kuwa Muungano unalindwa , kuenziwa na kudumishwa  na kizazi cha sasa na vile vitakavyofuata na kuongeza kuwa mwananchi anawajibu wa kuyalinda mafanikio hayo.

“Watanzania  tuna kitu cha  kusherehekea kwa sababu  miaka 50 ya Muungano kwa sababu tumebaki kuwa wamoja. Tanzania ni nchi moja ni lazima wananchi waliohusika kuunda Muungano huu tuendelee kuwakumbuka na ni sehemu ya sherehe hii”

Aidha amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana  baadhi ya watu wamekuwa wakibeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha Muungano kwa kulaumu na hata kutumia vyombo vya habari kuharibu taswira ya mafanikio hayo jambo ambalo halina msingi wala ukweli wowote kutokana na matunda  yanayoonekana sasa ya kuwafanya watanzania kuendelea kuwa wamoja.

Ameeleza kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuendelea kueleza mambo makubwa yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ndani na nje ya nchi na kufafanua kuwa Tanzania ina uzoefu mkubwa wa masuala mbalimbali katika Nyanja ya ushirikiano.

Amesema Tanzania imekuwa na ushirikiano na mataifa mbalimbali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kushirikiana na nchi nyingine jambo linaloonyesha ukomavu wa Muungano na utayari wa ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine.

“Ukiangalia sisi tuna miundombinu ya reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA inayokwenda nchi ya Zambia hii yote, miradi hii ni mikubwa iliyojengwa kwa ushirikiano  hili tu linaonyesha kuwa sisi tuna uzoefu mkubwa katika masuala ya muungano hasa kufanya kazi kwa pamoja  katika masuala haya ya Muungano”

Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa kushirikiana na mataifa jirani ikiwemo mkataba wa ujenzi wa reli uliosainiwa hivi karibuni kati ya Tanzania na Burundi.

Kuhusu  wizara na taasisi za muungano zitakazoshirikiana na vyombo vya habari kutoa taarifa kwa umma kuhusu  masuala mbalimbali kuhusu taasisi na wizara husika kuanzia mwezi huu  amesema ni pamoja na Wizara ya Kazi na Utumishi wa Umma na Ofsi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tume ya uchaguzi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Nyingine ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar,Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu.

Wizara na Taasisi nyingine ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi za Wizara ya Fedha (Muungano) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mikopo ya Nje, Benki Kuu ya Tanzania, Taasisi ya Kupambana na Fedha Haramu na Mamlaka ya Bima.

Aidha amesema kuwa kuelekea kilele cha sherehe hizo kutakuwa na fainali tamasha kubwa linalohusisha vikundi mbalimbali vya muziki na taarabu ambapo rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi atakuwa mgeni rasmi katika eneo la viwanja vya Mnazi mmoja pia kutakuwa na kongamano kuhusu Muungano wa Bara la Afrika ambalo litafanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu mstafu  Dkt. Salim Ahmed Salim.

Matukio mengine ni pamoja  na fainali  za kongamano  la wazi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  litakalofanyika Zanzibar tarehe 19 mwezi huu,Hotuba na  zoezi la utoaji wa nishani litakalofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho  Kikwete na mkesha mkubwa wa miaka 50 ya Muungano katika viwanja vya mnazi mmoja Dar es salaam na viwanja vya Mwaisla, Zanzibar.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top