Mtalii kutoka nchini Ujerumani anayefahamika kama Bi. Jeanne Traska (32) akiwa na muongoza wageni Athuman Juma leo majira ya saa mbili na nusu asubui wamekwama katika kilele cha Mawenzi Mlimani Kilimanjaro kwa kamba iliyonasa na kuwafanya wasiweze kushuka chini wala kwenda juu.
Bi. Jeanne na Athuman Juma walianza kupanda mlima kupitia Kampuni ya Nordic Tours tarehe 18.3.2014 kwa kutumia njia ya Rongai - Kibo –Marangu safari ambayo ingewachukua siku tano.
Hadi sasa taarifa za awali zinaonyesha kuwa Bi. Jeanne alitakiwa kwenda kileleni Kibo lakini katika mazingira yasiyofahamika alibadili uamuzi na kuelekea kilele cha Mawenzi ambacho huwa hakitumiwi na watalii isipokuwa kwa kujaza fomu maalum inayoonyesha kuwa mgeni amekubali kwa hiyari yake kupanda kilele hicho.
Shirika la Hifadhi za Taifa kwa kushirikiana na Kampuni ya Nordic Tours wanaendelea na jitihada za uokoaji kwa kutumia askari ambao wanaelekea eneo la tukio pamoja na helikopta itakayosaidia zoezi la uokoaji kwa kutegemea na hali ya hewa itakavyotulia ambapo hivi sasa kuna mawingu mazito katika eneo la mlima.
Umma utaendelea kufahamishwa maendeleo ya jitihada za uokoaji kadri zitakavyopatikana.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.