ADEN RAGE AINGIA MADENI KWA AJILI YA MISHAHARA YA WACHEZAJI WA SIMBA SC

MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage jana alitimiza ahadi ya kuwalipa haraka wachezaji wa timu hiyo mshahara wao wa mwezi uliopita baada ya fedha za awali kutumiwa isivyo.clip_image002Saa chache kabla ya Simba kuivaa KCC ya Uganda katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mjini Unguja visiwani Zanzibar, Jumatatu wiki hii, aliwataka wachezaji kucheza kwa bidii ili kubeba kombe hilo huku akiahidi kuwalipa mshahara wa mwezi uliopita haraka.

Hata hivyo, Simba ilipoteza mechi hiyo kwa bao 1-0 na kombe hilo kwenda jijini Kampala. “Leo (jana) nimelipa shilingi milioni 32 kwa ajili ya mishahara ya wachezaji kwa mwezi uliopita.

Fedha zake zilikuwa zimetumika isivyo ndani ya Simba. Niliwaahidi wachezaji kabla ya mechi ya Kombe la Mapinduzi kuwa nitawalipa haraka, na nimetimiza ahadi leo,” alisema Rage jana Dar es Salaam.

“Nimemkabidhi Mweka Hazina fedha hizo ambazo nimezikopa ili kuhakikisha wachezaji wanalipwa haki yao,” aliongeza Rage na kukataa kufafanua kwa nini awali fedha zilizopo, zilitumika isivyo.

Baadhi ya vyombo vya habari jana viliripoti kuwa Rage na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Zacharia Hans Poppe, walipigana vikumbo katika kambi ya Simba muda mfupi kabla ya mechi ya KCC.

Inadaiwa kuwa Rage alikuwa wa kwanza kufika kambini na kuzungumza na wachezaji na kuwataka kucheza kwa bidii na kutwaa kombe na kuahidi kulipa mshahara wao wa Desemba haraka.

Inaelezwa kuwa baada ya Rage kuondoka, Hans Poppe alifika na kuzungumza na wachezaji na kutoa Dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 15), akieleza kuwa ni sehemu ya mshahara huo wa Desemba.

Kamati ya Utendaji ya Simba ilitangaza kumsimamisha Mwenyekiti wao, Rage Novemba mwaka jana, katika uamuzi ambao umekosa baraka za baadhi ya wanachama wa Simba na umekataliwa na mamlaka za soka nchini likiwamo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu ulikiuka Katiba ya Simba.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post