MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, leo wamethibitisha kumsaini Straika wa Uganda Emmanuel Okwi kwa Mkataba wa Miaka miwili.
Okwi anatokea Klabu ya SC Villa ya Uganda baada kurudi kwao akitokea Klabu ya Tunisia, Etoile du Sahel, ambako aliuzwa na Simba mwanzoni mwa Mwaka huu kwa Dau la Dola 300,000 ambazo zimezua utata hadi sasa.
Akiwa huko Etoile du Sahel, Okwi alicheza Mechi 1 tu na kuamua kurudi kwao Uganda baada kudai kutolipwa Mishahara yake na kurejea kuichezea SC Villa ambayo alikuwa akiichezea kabla kuhamia Simba Mwaka 2010.
Sakata la Okwi kuhamia Etolie du Sahel, pamoja na madai yake ya Mishahara, linasemekana lipo mezani kwa FIFA.
Akithibitisha Uhamisho wa Okwi, Ahmed Bin Kleb, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, alisema wamemsajili Staa huyo wa Uganda karibu Wiki moja iliyopita lakini ni leo tu ndio wamepata ITC, International Transfer Certificate, Hati ya Kimataifa ya Uhamisho, na ndio maana wameamua kutangaza rasmi ili kuondoa utata wowote kuhusu Usajili wake.
Bin Kleb amesema nia yao ni kujiimarisha ili kufanya vizuri kwenye CAF CHAMPIONZ LIGI ambako Mwakani ndio wanaiwakilisha Tanzania Bara.