Watumishi hao wanadaiwa walihusika kugawa kinyume cha taratibu viwanja katika eneo la Dampo lenye viwanja zaidi ya 20 na kiwanja cha Kilombero.
Kamati imeamua hivyo baada ya kutembelea viwanja hivyo na kupata maelezo kutoka kwa watendaji wa Jiji na kugundua mapungufu makubwa katika ofisi ya ardhi Jiji la Arusha.
Agizo la Kamati hiyo limetolewa na Mwenyekiti wake, Dk Hamisi Kigwangalla ambaye alisema licha ya kuagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi hao na kuchukulia hatua za kisheria, pia amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana kusimamisha utoaji wa vibali vya ujenzi wa viwanja hivyo.
Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nzega, aliwataja watumishi wanaodaiwa kuhusika katika utoaji wa vibali hivyo kuwa ni pamoja na Richard Ndagamuso aliyekuwa Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri. Kwa sasa Ndagamuso amehamishiwa mkoani Kagera.
Wengine ni Mrimba Magembe, Ofisa Ardhi ambaye kamati iliambiwa ameacha kazi kwa kutoa notisi ya saa 24 akiwa mkoani Shinyanga.
Yumo pia aliyetajwa kwa jina moja la Urassa, mtumishi wa Idara ya Ardhi ambaye pia ameacha kazi ndani ya saa 24, ingawa bado yuko jijini Arusha.
Rungu la Kamati hiyo ya Bunge limemwangukia pia Elly Jacob Kirenga ambaye alikuwa Ofisa Mkuu wa Mipango Miji, lakini kwa sasa amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Kirenga, juzi aliitwa kujieleza mbele ya kamati hiyo.
Dk Kigwangalla alisema kamati imeamua kuwa watumishi waliosimamishwa kazi kama wako Arusha wanapaswa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na kama wako nje ya Mkoa wanapaswa kuripoti kwa Mkurugenzi wa halmashauri ama Jiji husika.
Alisema kamati imeiamuru Serikali ya Mkoa wa Arusha kumsaka na kumfikisha mtu mmoja anayetambuliwa kwa jina la Sadik Abdallah Sadik mbele ya kamati kujieleza jinsi alivyopata baadhi ya viwanja katika dampo la Njiro.
"Huyu Sadik ameonekana sana katika hati za viwanja vya Njiro, lakini kuna utata mkubwa juu ya umiliki wake na upataji wake hivyo tunamhitaji ili kamati iweze kujiridhisha juu ya upataji wa viwanja hivyo,’’ alisema.
Kamati imesema na kuzitaka Halmashauri na Jiji kote nchini kuwa na kumbukumbu sahihi za mafaili ya viwanja tofauti na walivyoona katika Jiji la Arusha kwani utaratibu wa mafaili ya viwanja ni mbovu.
Dk Kigwangalla alisema kamati imeamuru Kamishna wa Ardhi Kanda ya Moshi na Wakurugenzi wa Jiji la Arusha kutoka mwaka 2000 hadi 2012 waripoti Dodoma mara moja mbele ya kamati hiyo kujieleza juu ya utoaji holela wa viwanja hivyo.
Alisema kamati imesema itamshauri Rais Jakaya Kikwete kufuta hati ya kiwanja cha Kilombero na kilichopo eneo la Njiro ili viwanja hivyo vitumike kwa maslahi ya wananchi tofauti na sasa.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.