Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa
Na Abdulaziz Video,Dodoma
SERIKALI imefanya uteuzi wa vyuo nane (8) vitakavyotumika kwa
majaribio (pilot) katika kufundisha mtaala wa stashahada ya elimu ya
ualimu katika shule za msingi nchini.
Akiongea na Mtandao huu kuhusiana na timu ambayo ilikuwa ikikusanya maoni ya kitaalamu kuhusu mtaala wa stashahada ya elimu ya ualimu katika shule za msingi Tanzania, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Elimu), Kassim Majaliwa, alisema vyuo vilivyoteuliwa vitano ni vya serikali, na vitatu ni vya binafsi.
Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Chuo cha Ualimu Korogwe, Chuo cha Ualimu Bustani (Kondoa), Chuo cha Ualimu Vikindu (Mkuranga), Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Dar es Salaam) na Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu ADEM (Bagamoyo).
Vyuo vingine ni Chuo cha Ualimu Capital (Dodoma), Chuo cha Ualimu
Mount Sinai Dar es Salaam na Chuo cha Ualimu Paradigms kilichopo Dar es Salaam.
“Nawaagiza wakuu wa vyuo vyote vya ualimu hapa nchini wahakikishe kuwa vyuo wanavyoviongoza na kuvisimamia vinaonyesha mabadiliko hususani katika maeneo ya ufundishaji na ujifunzaji, upimaji na tathmini na utekelezaji wa matakwa ya ubora wa elimu,” alisema Majaliwa.
Alisema utekelezaji wa mtaala huo unatazamiwa kuanza mwaka huu, mara baada ya kumalizika utoaji na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wataalamu walioteuliwa.
Aidha, Majaliwa alibainisha vigezo vilivyotumika kuteua vyuo husika
kwa majaribio, kuwa pamoja na mambo mengine, wamezingatia uwepo wa rasilimali watu na miundombinu stahiki, uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia sanjari na utayari wa uongozi wa chuo,
jumuiya nzima ya walimu na wafanyakazi,” alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mtaala huo, unaoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(Nacte) Timothy Manyaga, alisema kada ya elimu ya msingi bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Upungufu wa Walimu, hususan walimu wa Hisabati na Sayansi.
Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na uandikishaji mdogo, wa
wanafunzi katika madarasa ya elimu ya awali, na msongamano wa
wanafunzi darasani katika baadhi ya shule.
Awali, katika Elimu ya Msingi, Majaliwa alisema hadi kufikia sasa,
wizara imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kutoka 493,636 mwaka 2005 hadi 909,435 mwaka 2012,
Alisema Walimu wa Shule za Msingi pia wameongezeka kutoka 135,013 mwaka 2005 hadi 180,987 mwaka 2012.
“Pia kuimarika kwa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kutoka uwiano wa 1:56 mwaka 2005 hadi uwiano wa 1:47 mwaka 2012,” alisema Majaliwa.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.