Wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani sasa wataanza kupimwa virusi vya Ukimwi nyumba hadi nyumba.
Akizungumza Mratibu wa kudhibiti Ukimwi wilayani humo, Kusena Job, alisema kuwa njia hiyo itasaidia watu wengi kujitambua afya zao.
Hata hivyo alisema zoezi hilo litakuwa la hiyari kwa kumshauri mlengwa. "Tuna mpango wa kuhamasisha upimaji wa Ukimwi kwa kupita nyumba hadi nyumba hii itasaidia kila mmoja kujitambua afya yake," alisema.
Aliongeza kuwa ipo changamoto ya baadhi ya watu hasa kinababa, kutokuwa na mwamko wa kujitokeza kupima, ikilinganishwa na kinamama ambao wamekuwa wepesi katika kuitikia hilo.
Alisema kuwa, akinamama hata wanapokuwa wajawazito wanapoanza kliniki, wamekuwa wepesi kukubali kupima na kujitambua.
Mratibu huyo alisema kuwa katika wilaya hiyo kuna vituo nane vinavyotoa huduma ya unasihi na utoaji wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi ikiwemo hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Alivitaja vituo vingine vinavyotoa huduma hiyo kuwa ni, kituo cha Chalinze, Lugoba, Miono, Mbwewe, Ubena na Msata.
Alisema kuwa kuna mpango wa kuongeza vituo vingine viwili, Yombo na Kibindu.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.