SITAISAHAU FACEBOOK
NA: EMMY JOHN P
SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU
Nililala katika mkeka. Ni kama nililala kwa sekunde kadhaa hatimaye pakapambazuka.
Mzee akaniamsha, akanisihi sana nihakikishe Napata jina langu halisi na hapo nitaendelea na maisha yangu vizuri.
“Jina langu ni nani?” nilijiuliza kwa sauti akanisikia.
“|Hata mimi silijui lakini ni lazima ulipate ili kuzikwepa laana za ukoo wako. Fuatilia historia yako vyema mwanzo hadi mwisho. Historia ya kweli ipo kwa mama…kamuulize mama yako. Wewe ni nani? Lakini nakukumbusha kuwa wewe sio Isabela”
Mzee alinisindikiza hadi njia ya mabasi.
“Usizungumze na mtu yeyote, kwa usalama wako na abiria wenzako.” Alifanya kunisemesha kwa sauti hafifu. Nikamsikia na kumwelewa.
Basi likapita. Nikapanda!! Mzee alinilipia nauli huku akichukua fursa ya kuzungumza na kondakta.
Safari ya kurejea Makambako. Safari ya kwenda kulitafuta jina langu. Jina lililopotea.
Kaka aliyekuwa pembeni yangu alikuwa anaongea maneno mengi sana. Lakini sikuwa namjibu chochote.
Hatimaye tukaifikia Makambako!! Nikashuka garini nikaikanyaga ardhi ya Makambako kwa huzuni sana!! Hatua kwa hatua nikaanza kuelekea nyumbani.
***
SIRI SIRINI
Mwanamke wa makamo ambaye sasa mvi zilikikaribia kichwa chake chote alikuwa anafagia uwanja. Alikuwa akiimba nyimbo anazozijua yeye huku akionekana kuzifurahia. Nilimtazama kwa makini. Nikatamani ningekuwa nimekuja kwa mazuri huenda ningemshtua kisha tukacheka wote. Lakini nilikuwa nimekuja kwa mengine magumu sana.
Huyu alikuwa ni mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi.
Nikanyemelea. Akashtuka akageuka.
“Belaaa….Belaaa mwanangu.” Akautupa ufagio, akanikimbilia, akanikumbatia kwa nguvu. Joto lake likaupenya mwili wangu ulio dfhaifu. Nikaamini kuwa nilikuwa nimemkumbuka sana. Chozi likanitoka. Nikamkumbatia kwa nguvu zaidi.
“Karibu mwanangu…mbaya wewe..yaani kimya kimya au uliongea na Suzi..wabaya sana nyie.” Alilalamika nikajilazimisha kutabasamu.
Tuliingia ndani. Tukafanya mazungumzo ya hapa na pale. Hadi tulipokatishwa na nyimbo nyingine kutoka kwa mlevi. Huyu alikuwa baba yangu mzazi. Asubuhi sana alikuwa anatokea kilabuni.
Sijui alilala huko? Nilimuuliza mama./
“Hamna sema ameamkia huko.”
“We Helena wewe…Aaah!! Suzy..ina maana haunioni uje kunipokea…si ku hizi hamsalimii watu!!” alizungumza kilevi. Macho yake hayakumwezesha kujua iwapo mimi ni Isabela.
Akapita akiacha nyuma harufu ya pombe kali. Akaingia chumbani.
Baada ya kelele za hapa na pale akasikika akikoroma!!!
Nilijikaza sana na sasa nikaamua kumueleza mama kilichonileta pale nyumbani.
“Mama hivi hili jina la Isabela ni nani alinitungia.”
“Mbona wauliza hivyo mwanangu.”
“Nipe jibu mama..ama ukoo wangu ni upi.”
“We mtoto umekuwaje lakini.”
“Nijibu mama.”
“Mbona kila kitu kipo wazi..ukoo wako ni huu wa baba yako, na jina hilo ni mimi na baba yako tulikupatia.” Alinijibu.
Niliondoka sebuleni nikaenda chumba cha wasichana nikajinyoosha. Nikapitiwa na na usingizi.
Nilikuja kushtuka nikiwa na njaa kali.
Nikaliendea jiko.
Nikajihudumia vilivyokuwepo, kisha nikareje chumbani.
Majibu ya mama yalikuwa hayajaniridhisha hata kidogo.
Nitamuuliza baba pia!! Huenda kuna kitu anajua.
Kwa nini aliniita Isabela.
Nikasinzia huku nikiwa nimejiahidi hivyo kichwani mwangu.
*****
Asubuhi na mapema nilikuwa wa kwanza kuamka. Nilihitaji kumuwahi baba akiwa katika akili zake vyema kabisa.
Kabla hajalewa!!
Niliwahi na kujifanya naosha vyombo.
Hatimaye nikasikia mlango wa chumbani unafunguliwa. Baba akatoka.
“Aaah!! Bela mwanangu…lini tena umetuvamia wewe…umemaliza mitihani lakini.”
“Nimemaliza..shkamoo baba….”
`aliijibu salamu. Tukabadilishana mawazo na hatimaye kama kawaida yake akaniomba pesa.
“baba kabla ya hilo…nahitaji kukuuliza kitu.”
Alinisikiliza kwa makini, nikamueleza kile nilichomueleza mama. Baba alionekana kushtushwa na habari hiyo. Alijaribu kujiweka sawa lakini nilikuwa nimemsoma.
“Fanya hivi…nipatie hiyo pesa nikirejea tutaongea ni stori ndefu kidogo..si unataka kujua maana ya Isabela na kwanini tulikuita hivyo..nifanyie kwanza nienda kupata supu kidogo.” Alijaribu kukwepesha mada.
Niliheshimu maamuzi yake. Nikaingia ndani nikarejea na pesa kidogo nikampatia. Akatoweka.
Moyoni nilipata matumaini makubwa sana!! Niliyaamini yale maneno ya yule mzee.
Sasa mimi ni nani kama sio Isabela? Na kuna siri gani inazunguka hapa. Nilijiuliza. Wa kunijibu alikuwa ni baba.
Nilisubiri sana. Hadi pale ilipokuja taarifa kuwa baba amekutwa mtaroni. Hana jedraha lakini haijafahamika bado kama anapumua ama amekufa!!
Hii ilikuwa ni habari ya kushtua sana.
Mimi na mama tukakimbia kuelekea hospitali ambayo tulielezwa kuwa amelazwa.
Bahati mbaya zilikuwa mbio za kuwahi upepo.
Baba yangu hatukuwa naye tena!! Kifo cha utata. Hakuwa amelewa. Alikutwa na ile pesa niliyompa.
Hakika mimi sio Isabela, na kuna siri mzee wangu amekufa nayo!! Nilizungumza na nafsi yangu.
Jina langu ni nani sasa? Na kwa nini waliniita Isabela?
****
Ulikuwa msiba wa mtu maskini hata utata ungegubika vipi bado angezikwa na kusahaulika. Ndivyo ilivyokuwa kwa baba yangu.
Licha ya kifo chake kuwa na utata hapakuwa na la ziada alitakiwa kuzikwa.
Msiba huu ulivuta watu wengi kiasi kutokana na jina la mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu. Mwalimu!! Hivyo wanafunzi walijaa sana.
Historia fupi ya marehemu ilisomwa.
“….marehemu ameacha mjane na watoto wanne..mmoja wa kiume na watatu wa kike….Sebastian John, Suzan John, na Helena John.” Alimaliza kutaja majina ya watoto wa marehemu.
Sauti za kuguna zukatawala ghafla, watu wakawa wanaulizana hao watoto wanne mbona hawajatimia? Kina mama wakashindwa kumezea wakauliza palepale.
Ujumbe ukamfikia msomaji baada ya kijana mmoja kuagizwa.
Msomaji akaanza kupekua hapa na pale. Kimya kikatanda!!!
“Anaitwa Isabela John huyu hapa.” Shangazi yangu alipaza sauti akanitambulisha ili kuondoa ile sintofahamu. Nikanyoosha mkono juu. Watu wakageuka na kunitambua.
Tendo lile la watu kugeuka kuniangalia likanifanya nipatwe na aibu kidogo. Inakuwaje mimi jina langu linasahaulika?
Sikuuliza!!! Nikauchuna.
“Kwa hiyo mtoto wa nne ni Isabela John….samahani sana kwa mkanganyiko huu.” Aliomba radhi yule msomaji. Waungwana hawakulalamika.
Alipotaka kuendelea kusoma yanayoendelea katika risala hiyo akawa anatawaliwa na kigugumizi. Hali hii sasa ikaanza kuwakera watu. Lakini kabla hili halijapita akaanza kupiga chafya.
“Samahani!” akaomba radhi tena.
Haikukoma, ikaongezeka chafya ya pili, mara ya tatu ya nne, chjafya mfululizo. Akaachia lile karatasi lililoandikwa risala. Hali ikaonekana dhahiri kuwa si nzuri!!
Akajikunja kunja huku akionekana kuzitafuta pumzi zake. Mwili ukakosa muhimili akaanguka chini.
Wale waliokuwa na ghadhabu sasa ikawalazimu wakimbilie kutoa msaada. Msoma risala akatulia akiwa amejishika kifuani. Akafanana na ile maiti ya baba iliyopo katika jeneza.
Baadhi ya wanaume wakamchukua garini.
Tuliosalia tukaendelea na taratibu nyingine, hatimaye tukazika. Watu walikuwa wanajiuliza kimemsibu nini yule bwana. Hakuna hata mmoja aliyeweza kutoa majibu hata mimi pia nilikuwa katika sintofahamu.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema la mgambo likalia. Msoma risala alikuwa amepoteza maisha!!!
*****
Suala la baba kuondoka na siri kubwa aliyotakiwa kunieleza lilikuwa ni jambo lililoutafuna sana mwili wangu. Nilikuwa najiuliza bila kufikia muafaka.
Maisha yaliendelea. Chuo kilikuwa kimefungwa jijini mwanza na nilikuwa nina kumbukumbu kuwa niliomba ruhusa maalumu kabla ya mitihani haijaanza. Hivyo nilitakiwa sasa kufuatilia iwapo mtihani umekaribia ama la.
Nilitafakari nani wa kumuuliza. Nikamkumbuka Maria. Nilijilazimisha kuamini kuwa yale ya mimi kumuona katika pori nchini Zambia zilikuwa ni ndoto tu.
Nikajaribu kuvuta kumbukumbu za wapi nimewahi kuhifadhi namba yake sikupata jawabu. Hilo nalo likawa tatizo.
Nikafikia uamuzi wa kwenda katika huduma za internet café sio mbali sana kutoka nyumbani kwetu. Wakati huo sikuwa na nywele kichwani hivyo nilikuwa nimejitanda ushungi.
Nilifika kwa wakati muafaka nikapata nafasi, nikatazama yaliyonipeleka kisha nikalipia huduma ile.
Wakati nasimama niweze kutoka nikagonganisha macho yangu na mtu ambaye niliamini kuwa haikuwa mara yetu ya kwanza kuonana. Alikuwa ni msichana mnene. Nikavuta kumbukumbu lakini sikulipata jina lake.
“Mambo…” nilimsalimia, akatabasamu kisha akanijibu.
“Ujue nilidhani nakufananisha. Nilikuangalia wakati unaingia ujue nikahisi nimekufananisha.”
“Na mimi hivyo hivyo!!” nilimuunga mkono.
Tukasogea nje na kupiga stori za hapa na pale.
Wakati wa kuagana ndipo tukakumbuka kuulizana majina.
“Naitwa Isabela.”
“Mh!! Isabela!! Ulibadilisha jina ama..maana nakumbuka walikuwa wanakuita nani vilee.” Alijaribu kuvuta kumbukumbu. Mimi nikawa namtazama tu! Nilibadilishaje jina sasa mimi.
“Hata sijabadili mbona.” Nilimwelewesha. Akazidi kupinga.
Hatukufikia makubaliano, akapigiwa simu akaniaga huku akisisitiza kuwa nimemdanganya jina. Mimi sio Isabela.
Nilimsindikiza kwa macho hadi akatokomea. Nilijitazama iwapo nilifanana na mmoja kati ya ndugu zangu lakini hakuna niliyefanana naye ambaye ningeweza kumtupia lawama kuwa watu wananifananisha naye.
*****
Kile kitendo cha yule dada kuonekana kana kwamba amenifananisha kisha akakataa kuwa jina la Isabela si la kwangu nilikipuuzia na kumchukulia yule dada kuwa amepoteza kumbukumbu zake kwa kuwa miaka imepita mingi sana.
Nilivyotoka pale moja kwa moja nikaenda nyumbani kwa dada Suzi kwani tangu nirejee Makambako sikuwa nimeenda kumsalimia mume wake na familia kwa ujumla zaidi ya kukutana msibani.
Nilimkuta yupo nyumbani akiwa na familia yake jikoni wakiandaa chakula.
Alinipokea vyema tukasalimiana kisha nikataka kumsaidia kupika.
“Kuliko kunisaidia kupika ni heri unisaidie kumbeba huyu mwanao.” Alizungumza huku akijitoa mtoto aliyekuwa amembeba mgongoni. Nikampokea na kumbeba.
Ghafla mtoto akaanza kulia taratibu kisha anaongeza kilio.
“He! Haka nako lini tena kameanza kuchagua watu.” Nilimuuliza dada. Hakunijibu zaidi ya kuguna akimaanisha kuwa huenda ni jambo la kawaida.
“We dogo wewe..mama yako mdogo huyo.” Alisema akimaanisha kumweleza yule mtoto mdogo wa mwaka mmoja. Japo hakumuelewa.
Mtoto akazidi kutoa kilio.
“Hebu mchukue mwanao nadhani ana kisilani cha usingizi.”
Nilimkabidhi dada Suzi mtoto wake, cha ajabu hakunyamaza zaidi ya kuongeza kulia. Sasa Suzi akashtuka na kulichukulia uzito hili suala ambalo mwanzo ulikuwa kama mzaha fulani hivi. Alimkagua mwanae kama amechubuka mahali. Hakuna kitu!
Huenda basi ameumwa na mdudu, hata hilo pia halikuwepo!!!
Mapishi yakakoma kwa muda. Mtoto analia kwa sauti ya juu sana. Machozi yanamtoka kwa wingi mno. Hatari!!
Ilianza dakika moja na sasa zilikuwa zinatimia sitini, yaani saa zima bila kilio kukoma. Mtoto alikuwa analia sana.
Majirani wakakisikia kilio hicho kikuu wakajongea pale nyumbani kwa Suzi. Na wao pia wakashangaa.
Suzi akajaribu kumpa titi mtoto aweze kunyonya, akalikataa. Kila mmoja alijaribu kumbeba bila mafanikio.
Kimbilio lililofuata likawa hospitali.
Huko napo hapakuwa na nafuu yoyote. Madaktari walimfanyia uchunguzi na kurejea na majibu yasiyoridhisha hata kidogo. Walisema kuwa mtoto hakuwa na ugonjwa wowote ule. Hivyo hawakuwa na msaada wowote ule.
Tulirejea nyumbani. Tulipofika huku kila aliyetazama tukio hili akiwa katika mfadhaiko wa hali ya juu na kuegemeza imani zao katika mambo ya kishirikina. Ni hapa na mimi nilijishtukia na kuanza kuamini kuna jambo. Lakini jambo lenyewe ni mimi!!
Niliamini kuwa ni mimi baada ya kuyakumbuka maneno ya yule mzee kule Iringa. Aliyeniambia nisipofuatilia jina langu basi nitasababisha majanga mengi sana popote nitakapokuwa.
Usiku mzima mtoto alikuwa analia. Na kama hiyo haitoshi mara mkono wake wa kushoto ukaanza kujikunja. Suzi naye akawa analia sasa maana hakuwa na njia nyingine.
Baba wa mtoto alipigiwa simu akiwa safarini kuelekea Songea akalazimika kuhairisha safari, mama yetu alikuwa hapo nyumbani pia.
Suzi alikuwa Amelia sana na alikuwa amewaacha walokole wenzake wakimwombea kwa namna zote mtoto yule. Lakini hali iliendelea kuwa tete.
Mtoto huyu akifa itakuwa juu yangu!! Niliwaza na kufikia maamuzi.
Dada Suzi alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kunisaidia katika hili. Maana tayari tulikuwa tunamtambua kuwa alikuwa mwanamke wa kipekee aliyeweza kuhifadhi siri nzito nzito.
Huenda hata siri aliyokufa nayo baba nayo angeweza kuwa nayo!! Nikarusha karata yangu.
Nikamfuata dada Suzi nje alipokuwa amekaa chini ya mti akilia kwa juhudi zote.
“Da Suzi.” Nilimuita, akageuka akanitazama na macho yake mekundu yaliyovimba kutokana na kulia kwa muda mrefu.
“Nahitaji kuzungumza nawe dada.”
Alinitazama tena bila kusema lolote.
“Kuna jambo nahisi….”
“Nini?”
“Naweza kuwa najua chanzo cha tatizo hili.”
Suzi akageuka mzima mzima akanitazama kwa umakini kabisa akisubiri niseme neno.
Sikuwa na haja ya kumueleza kuwa ile ninayotaka kumwambia ni siri, nilikuwa namuamini sana.
“Suzi…” nilianza kumuelezea kwa kirefu na mapana juu ya maisha niliyopitia, nikamueleza juu ya ile mimba ya maajabu ambayo mwisho wake ulikuja baada ya kukatwa ilea lama ya 666 katika makalio yangu, nilimueleza pia juu ya Dokta Davis na pesa zake haramu, ndoto za maajabu zote pia nilimuelezea.
Dada Suzi alinisikiliza vyema sana nilipokuwa namueleza juu ya makaburi ya Kiyeyeu huko Iringa na jinsi nilivyokutana na babu nisiyemfahamu aliyenieleza kuwa jina la Isabela sio jina langu. Natakiwa kulitafuta jina langu.
Alishangazwa na kukwama kwa basi letu hadi pale niliposhuka mimi, kifo cha mwanaume aliyekuwa anasoma risala ya marehemu baba pia alishangaa nilivyomweleza kuwa yawezekana ni moja ya majanga niliyoyasababisha.
“Hata baba alikuwa ameniahidi kunieleza jambo fulani lakini ajabu kabla hajaweza kunieleza ametutoka. Nahisi ni yaleyale. Najua dada yangu hauamini mambo haya lakini niamini mdogo wako.”
Nilimsisitiza na ili kumfanya aamini tuliingia ndani nikamfunulia kovu langu. Hapo sasa aliweza kuniamini.
“Kwa hiyo mwanangu anaweza kufa pia.” Aliniuliza kwa wasiwasi.
“Sijui nisemeje lakini kiukweli naogopa sana…” nilimjibu.
“Sasa Bela mimi nafanyaje hapa katika hili.”
“Dada kama unaweza kujua lolote lile kuhusiana na mimi tafadhali nieleze tumuokoe mtoto. Hana makosa hata kidogo.” Nilimsihi Suzi. Kilio cha mtoto kilikuwa juu kama kilivyoanza na alikuwa anazidi kujikunja mkono.
Suzi alinitazama usoni kama anayesoma kitu fulani kwangu.
“Bela…yapo baadhi ninayoyajua….nitakueleza, sio kwa imani za kishirikina hapana!! Nakueleza kwa kuwa ni lazima uyajue. Kama mwenyezi Mungu amenipa pigo hili ili nikueleze siri hii basi nakueleza. Lakini jitahidi kuwa na moyo mgumu.” Nilianza kutetemeka kwa maneno hayo ya dada, hakika nilikuwa namuheshimu kwa kuwa na siri nzito nzito.
ITAENDELEA....
About Author
JE, UNA HABARI, PICHA, TANGAZO, MAKALA NA USHAURI? USISITE KUWASILIANA NASI SIMU / WHATSAPP NAMBA 0625535420.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.