Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
RIWAYA: SITAISAHAU facebook MTUNZI: Emmy John P. SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA Maskini yule dada bila kujua kwamba ameambiwa anipatie kinga. Ak...

FACERIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
Maskini yule dada bila kujua kwamba ameambiwa anipatie kinga. Akadhani yule mbongo amemaanisha ule mkoba. Akaniomba msamaha kwa kila namna kisha kwa ukarimu kabisa akanipatia ule mkoba. Ulikuwa mzito kiasi. Nilipotaka kuondoka yule dada aliyekuwa amejikita katika kutafuta anachojua yeye, aliniita, nikageuka na kumshangaa kidogo.
“Unatakiwa kuweka sahihi.” Alinielezea kwa ukarimu.
Nikaona kama huyu binti ana nia mbaya na mimi. Nikabaki wima najiuliza iwapo niende mbele ama nirudi. Tukatazamana kwa sekunde kadhaa. Nikaona isiwe tabu. Nikarejea nikachukua kalamu niweze kuweka sahihi. Mara nikasikia fujo za mlango kufunguliwa.
Nikaomba Mungu usiwe mlango wa yule jamaa mbongo. Kisha nikasikia hatua kubwa kubwa zikitambaa.
“How long does it take to…to…..hell..” (Inachukua muda gani ku…ku…. ). Ilisikika sauti yenye kitetemeshi cha hasira. Alikuwa yule mbongo.
Sasa badala ya kuweka sahihi nikabaki kulishikashika tu lile daftari na kalamu. Mkojo ukatoka safari yangu ya mbali na sasa ulikuwa unahitaji kutoka. Nikabana miguu yangu!! Mkoba mkononi.
Ninafumaniwa Isabela mimi!!
Nikataka nikimbie!! Miguu ikawa mizito. Sikuwahi kufanya kitendo cha wizi hivyo lazima hali kama hii ingenitokea.
“Iam sorry boss..i have already given her (samahani mkuu..nimempatia tayari.)” yule dada wa mapokezi alijitetea kwa uoga.
Mara vile vishindo vikasita.
Yakafululiza matusi ya nguoni kutoka kwa yule mlevi wa kibongo.
Hapo sasa nikaangusha saini yangu.
Narudi vipi na ule mkoba sasa!! Nikajikaza nikaanza kuondoka.
Nilipogeuka nikakutana na kosa ambalo nililitegemea. Yule dada wa mapokezi alikuwa amebonyea chini tena.
Asante! Nilimshukuru kwa kitendo hicho.
Ghafla nikabadili uelekeo. Nikaelekea katika vyoo.
Upande huu, nikaambaa na korido hadi nikaufikia mlango wa kutokea. Nikamuachia tabasamu mlinzi aliyekua kwa nje na yeye akatabasamu. Tabasamuu la kizee. Kisha nikatoweka. Nikapiga hatua kwa hatua hadi nikalifikia geti kuu la kutokea. Hapa nilitakiwa kuandika jina. Nikaandika jina lililokuja kichwani mwangu lakini sio jina sahihi.
Geti likafunguliwa. Mimi na mkoba wangu. Nikatoka.
Nilipogeuka nyuma nikakutana na maneno mazuri ya kupendeza.
The Savoy Hotel
12 Buteko Avenue
Ndola
Zambia
Haya hayakuwa yananihusu. Niligeuka na kutazama mbele. Nikaanza kutokomea. Nikashtuliwa kwa kuguswa begani.
Nikageuka upesi nikaikuta amani ambayo nilikuwa naihitaji.
Samson…jemedari wa kisukuma.
Akanikumbatia kunipongeza. Lile joto lake likanikumbusha mengi. Nikapuuzia.
Oparesheni ilikuwa imekamilika.
****
Pesa zilikuwa kwa mafungu yanayolingana. Zilikuwa zinang’ara kuonyesha kwamba hazikuwa zimepitia mikono mingi.
Ilikuwa saa kumi alfajiri. Sasa nikiwa pamoja na Samson tulipita katika vijiwe ambavyo wenzetu walikuwa wanalala. Wote wakaamshwa. Hatimaye tukawa na mkutaniko wa pamoja wa kwanza tangu tuwe katika ardhi ile.
Niliwakumbusha juu ya ahadi yangu!! Sasa ilikuwa imetimia.
Hakuna aliyekuwa anafahamu thamani ya kwacha ya Zambia katika shilingi ya kitanzania. Hilo halikutupatia shida. Nikawachukua wenzangu watano wa kwanza. Nikaliendea basi linalotoka Ndolla kuelekea Mbeya mjini.
“Kwacha ngapi?” niliuliza. Akanijibu. Nikalipia nafasi za watu watano.
Wakaingia garini. Kiongozi wao akiwa Jesca
Nikarejea na kuwachukua wengine. Hawa kiongozi wao akawa Jenipher.
Kundi la nne nikalikabidhi kwa Samson.
Kisha nikabakisha kundi lililosalia mikononi mwangu.
John!! Akiwa ameambatana nami!! Nilichukua siti ya watu wawili. Nikamuweka John kisha nikambebesha mfuko fulani.
Hakuruhusiwa mtu kukaa pale.
Safari ikaanza huku maelekezo yota ya tunakutana vipi yakiwa kwa viongozi wa msafara.
Hatimaye tukaiacha Ndolla majira ya saa kumi na mbili. Safari ya kurejea Tanzania.
*****
Pesa zilibaki nyingi sana. Hivyo tuliamini kabisa hakuna kitakachoharibika. Jesca alikuwa na akiba yake, Jenipher na Samson vilevile.
(Mshikemshike )
TUNDUMA, Mbeya.
Mji ulikuwa umetulia sana. Hapakuwa na harakati za hapa na pale. Ilinishangaza sana kwa boda kama hii kuwa katika utulivu huu.
Tulikuwa tukihangaika kutafuta mahali pa kulala. Nyumba za kulala jirani na kituo cha mabasi zilikuwa zimejaa. Hivyo ilitulazimu kidogo kuzunguka. Hatukupata mahali pa kulala kwa wingi tuliokuwa nao. Sasa tuliamua kuishi maisha yetu ya Zambia. Tukaamua kulala katika stendi ya mabasi.
Baada ya kufikia uamuzi huo. Sasa mwenye kutafuta chakula aliruhusiwa lakini pa kulala tulikuwa tumeamua kabisa ni hapo hapo stendi.
Wanaume watatu waliamua kusindikizana kwenda kutafuta chakula.
Mkuu wa msafara huo Jesca aliwapatia pesa wakatoweka kwa ahadi ya kurudi upesi.
Ahadi ikavunjwa maradufu!! Hawakurudi.
Hadi tuliposinzia. Haikuwa kama yaliyomkuta Samson kule Ndola. Hawa hawakurudi kabisa.
Kesho yake. Tulipotoa taarifa polisi tulikutana na taarifa ya vifo vya watu watatu kwa kukatwa na mapanga.
Walikuwa wenzetu!! Lakini hatukukiri!! Hatukuhitaji kuwa karibu kabisa na polisi. Kwa kifupi hatukuwa tunajua hatma yetu. Hasahasa mimi ambaye nilikuwa na siri nzito.
Baada ya taarifa hizo kutapakaa. Tukajua nini kinachoendelea ndani ya mji wa Tunduma. Majambazi wa ajabu walikuwa wameuvamia mji. Hawa walikuwa na hadhi ya kuitwa majambazi wastaarabu. Walibandika matangazo kabisa kuwa kama mwanaume anatembea usiku basi awe na tahadhari aidha simu ama kiasi cha pesa shilingi. Elfu hamsini lakini bila hilo wakikutana ama zao ama zake.
Kumbe ndicho kimewasibu wenzetu!! Nilisikitika kuzipoteza roho hizi.
Asubuhi hiyo nilitaka kwenda kubadili pesa. Lakini bahati mbaya sikuwa na kitambulisho chochote. Nikaitupa kazi hiyo kwa Samson. Akazunguka mtaani kuzibadili baada ya kugundua kuwa Kwacha moja ni sawa na shilingi 0.3 ya kitanzania.
Baada ya zoezi lile kukamilika na kupata pesa ya kutosha sasa kila mmoja alitakiwa kuubeba mzigo wake mwenyewe. Aliyesema kuwa anaishi Dar alipewa nauli aondoke zake, wa Arusha naye vilevile. Na pesa ya ziada kila mmoja alipewa.
“Muutangaze ushuhuda huu bila kuipunguza wala kuongeza neno!” niliwaambia wakati tunaagana. Kila mmoja alikuwa na furaha huku wakiniona mimi kama Mungu wao. Sikujali sana!!
Safari ya Mwanza tukabaki watano. Mimi, Jesca, John, Jenipher na Samson.
****
Siku ya safari kama ilivyo kawaida nikalipia siti ya watu wawili, Jesca na Jenipher wakakaa siti moja huku Samson akikaa peke yake.
Alama ya John shingoni ilinikwaza sana. Nilitamani aweze kutuona. Lakini alikuwa anauona ulimwengu wake mwenyewe.
Safari nzima ilikuwa tulivu sana. Nilikuwa natafakari mambo mengi sana. Nilitamani kwenda Makambako kwa mama lakini niliamini haukuwa wakati sahihi.
Nilihitaji nkujua kitu kuhusu Maria. Maana alinitokea kule porini siku ya kwanza kabisa na kamwe sikumuona tena.
Nini kilimsibu? Nilijiuliza.
Tulipita miji mbali mbali. Tukaipita Makambako, nikainama nikajifuta machozi, tukaiacha Mafinga, tukaingia Iringa mjini. Na hapa hatukusimama sana tukaendelea na safari.
Sasa gari lilisimama!! Hatukushangaa sana. Tulidhani ni kwa madhumuni ya kuchimba dawa. Lakini hatukuiona dalili hiyo.
Dereva akateremka. Akaangaza gari lake bila kuona tatizo.
Akaangaza tena. Hakuna tatizo.,
Msaidizi wake naye akashuka. Hakuna msaada!!
Wakashuka mafundi wakajaribu kugusa hapa na pale. Gari lilikuwa limezima.
Walijaribu kufanya kila wanaloweza lakini hapakuwa na matumaini. Dakika zikaanza kwenda. Masaa yakaenda. Hatimaye jioni.
Abiria wakashindwa kuvumilia. Wakatoa matusi mengi lakini haikusaidia. Gari halikuweza kuwaka.
Duh! Leo tunalala njiani!! Nilimweleza John japo hakunisikia.
John alichoweza kuona ni chakula na mengineyo lakini si watu!! Na watu halisi pia hawakuweza kumuona yeye.
Simu ilipigwa ili gari jingine liweze kuja kutuchukua. Basi lilifika likiwa na abiria wengine. Likazimishwa ili tuweze kubananishwa wote twende Dodoma. Abiria walilaani kitendo kile kwa lugha zote, huku wakilalamikia usalama wao.
“Kama hutaki basi hili hapa lala utasafiri kesho!!.” Zilikuwa kauli ngumu kutoka kwa mpigadebe. Hakuna aliyependezwa na kauli hiyo. Wakati huu sikuweza kukaa na John badala yake tulikuwa tumesimama. Ni Jesca pekee aliyepata nafasi ya kukaa. Yalikuwa mateso.
Walipofanikiwa kutubananisha kama viroba. Dereva akisifiwa na wapambe wake akaingia garini aweze kuendesha tuondoke.
Ikaanza tena kama utani, akachokonoa kwa mara ya kwanza likagoma, akajaribu mara ya pili bado hali ileile.
Akajaribu tena na tena. Injini haikuweza kuwaka. Kila mmoja akawaza lake.
Watu wakakimbilia kwenye imani za kishirikina.
Lakini huyo mshirikina ni nani? Hakuna aliyejua.
Abiria wakashuka. Kila mmoja akarejea kwenye basi alilokuwa amepanda awali. Hapakuwa na safari tena.
Usiku ukafika wanakijiji wakapika chakula na kutuuzia kwa bei mbaya sana. Hatukuwa na ujanja tukanunua.
Saa nne usiku mambo yakananza kubadilika. Hali ya hewa ilibadilika na kuwa ya kushangaza hata wanakijiji walikiri kuwa hiyo haijawahi kutokea. Badala ya baridi kali la Iringa sasa lilitanda joto.
Joto hilo ni kama lilimshtua John. John akasimama akataka kuondoka. Nikamzuia. Akawa anatumia nguvu!! Nikamzuia John, John akanitazama kwa jicho la hasira. Macho yake yakiwa mekundu sana.
John alikuwa ananiona? Nilijiuliza.
Lile joto likazidi. Abiria wakashuka garini.
Kuna kitu hapa!! Mapambano mapya!! Nikajisemea huku nikiendelea kumzuia John.
John sasa akanizidi nguvu.
Akanitoka. Akashuka chini. Nikajaribu kumkimbilia.
Huko nikamkuta akiwa anafanya jambo la ajabu. John alikuwa anajarfibu kuisukuma gari kwa kuitikisa.
Ajabu! Ikaanza kutikisika kweli. Mtikisiko ule ukawashtua wengi. Sasa vilio vikaanza kusikika. Kila mtu kuitetea nafsi yake.
Watu wakashuka upesi kwa kugombania mlango. Basi likaanguka.
Lilipoanguka John akatazama mahali. Na mimi nikageuza jicho kutazama. Yalikuwa makaburi
Makaburi yaliyo na historia ya kushangaza. Makaburi ambayo yalimtoa nishai mchina alipojaribu kupitisha umeme juu yake. Umeme ukagoma kuwaka. Akalazimika kusaluimu amri na umeme hakuupitisha juu ya makaburi yale.
Haya yalikuwa makaburi ya Kiyeyeu.
Yalikuwa yanafuka moshi wa dhahabu!!
Vita!!
ITAENDELEA ...

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top