Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI: “USILIE NADIA” SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI YA MAISHA: USILIE NADIA MTUNZI: George Iron Mosenya SIMU: 0757727324 au 0655 727325 SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA Nilijua kuwa sihitaj...

clip_image003SIMULIZI YA MAISHA: USILIE NADIA
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0757727324 au 0655 727325
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
Nilijua kuwa sihitajiki tena katikia mji ule, nami niliomba mwezi mmoja niweze kuondoka wakanikubalia. Sasa wanamuita Jonas mwanaharamu!!
Gusa pengine usimguse mtoto huyu, nililaaniwa mimi na si Jonas!!
Wakati natoka mlangoni nikakutana na mama Aswile. Sikujali lolote nikaelekea katika chumba changu, nikakusanya nguo zangu huku nikiwa natetemeka, Jonas akiwa mgongoni. Nikasikia chumba kikivamiwa, ni jambo nililolitarajia. Haraka nikageuka nikakutana na mama Aswile. Alikuwa amevimba huku akiwa ameshika mwiko. Taratibu nikamshusha Jonas. Halafu nikahamishia balaa kwa mama Aswile, nilimpiga huku nikimtuhumu kuwa amelaaniwa kwa kuwafanya watoto wake wanichukie bila sababu. Nilihakikisha amenyooka.
Baada ya hapo nikabeba kilicho changu na kuingia katika mitaa ya Tukuyu nikiwa na shilingi elfu tano tu!!
Pesa niliyoipata baada ya mama Aswile kuiangusha akijaribu kukabiliana na mimi!!
Jonas mgongoni, kibegi kidogo mkononi!!
Nikaingia katika mitaa yenye baridi kali. Sina ndugu wala rafiki!!.........
Sikuwa nafahamu ni wapi natakiwa kwenda muda huo, na hapo nikaanza kuona muda ukienda kwa kasi sana. Ilikuwa asubuhi mara ikawa mchana, bado nilikuwa katika kiza kinene bila jibu sahihi.
Mida ya saa nane mchana Jonas akaanza kulia huku akiwa mgongoni.
Njaa!! Nikawaza. Nikamgeuzia kifuani na kuanza kumbembeleza lakini hakubembelezeka, nikatamani angeweza kusema nini kinamtokea nitafute njia ya kumtibia lakini hakuweza kusema na badala yake alikuwa analia tu. Nikalazimika kuingia katika banda la mama lishe, nikaomba huduma ya chakula, nikapatiwa wali na maharage. Jonas akakataa kula badala yake akaendelea kulia kwa fujo na kuwa kero kwa wateja wengine. Hapa nikalazimika kutoka naye nje huku ule wali nikiulipia bila kuula hata kidogo, ningeanza vipi kula wakati Jonas alikuwa analia? Yule mama alinifuata nje na kuniuliza nini kimemsibu mtoto, nikamweleza kuwa nilihisi ni njaa lakini ajabu hataki kula hata hicho chakula. Yule mama akampima joto kwa kutumia mikono yake na kisha akanieleza kuwa mtoto alikuwa amechemka sana nijaribu kumpeleka hospitali ama la nimpatie dawa za kutuliza maumivu.
Hilo la hospitali lilikuwa zito sana kwa sababu nilikuwa na shilingi 5000 tu, sasa ingetosha vipi gharama za hospitali tena kwa mgonjwa asiyefahamika magonjwa yake. Nikaamua kushika la pili, nikanunua dawa za kutuliza maumivu, nikazikoroga katika maji kishas tukasaidiana na yule mama kumywesha Jonas, alisumbua sana lakini alimeza.
Baada ya saa zima Jonas hakuwa akilia tena na alikuwa amejilaza katika mikono yangu. Mama wa kufikia ambaye hajui hata kesho yake na sasa ana mtoto mikononi mwake.
Ngoja ngoja, tafakari tafakari hatimaye usiku ukafika akili ikiwa imeganda tu nikishindwa kufikiri hata kidogo ni kitu gani natakiwa kufanya.
Si kwamba hawakuwepo watu ambao ningeweza kuwakabili na kunipa hifadhi ya siku mbili tatu, hofu yangu ilikuwa usalama wangu katika wilaya hiyo. Hao watu niliokuwa nafahamiana nao walikuwa wakimfahamu mzee Aswile na familia yake, hivyo ilikuwa kazi nyepesi sana kuweza kuzisikia tetesi za shambulio langu dhidi ya familia ile. Na ningejuaje huenda nilikuwa natafutwa??
Ningekuwa mimi kama mimi ningejitoa muhanga lakini Jonas!! Jonas aliniumiza sana kichwa. Laiti kama ningeamua kujisalimisha huko kisha nikakamatwa, bila shaka Jonas angebaki katika familia ya mama Aswile! Familia ambayo inamuita yeye mwanaharamu. Angeishi vipi, kama wakati mtetezi wake nilipokuwa naye waliweza kumuita mwanaharamu na kumzaba vibao, je wakati ambao sipo kabisa nini kingejiri kama sio kumuua kabisa.
Hapana!! Siwezi kurudi nyuma. Nikafikia uamuzi huo. Nikasimama na kuelekea stendi ya mabasi ya pale Tukuyu, nikatafuta kona moja nikajiegesha huku Jonas akiwa salama kifuani kwangu.
Sijui hata nilikuwa nawaza nini hadi kufika pale stendi. Lakini ni sehemu pekee ambayo niliamini kuwa hapatakuwa na bughuza za hapa na pale, maana nikiwa na begi langu ningeweza kusingizia kuwa mimi ni abiria.
Baridi ilikuwa kali sana majira ya saa tatu usiku, meno ya Jonas yakawa yanagongana mdomoni, matumbo yake yakawa yanaunguruma. Nikajisemea nafsini kuwa yule mtoto yupo katika mateso makuu, alinikumbatia kwa nguvu sana lakini sijui kama alipata alichokuwa akikitafuta.
Joto!! Hakulipata joto kwani mwili wangu wote ulikuwa wa baridi pia. Nilimsikitikia sana, nikajaribu kujiuliza tena na tena ni kitu gani naweza kufanya kupambana na hali hii. Nilitazama huku na kule, kisha nikavamiwa na wazo moja kuwa iwapo nitaleta lelemama Jonas atanifia kifuani.
Wazxo la kifo likanigutusha kutoka pale chini, nikasimama wima, nikampigapiga Jonas mgongoni, akakohoa kisha akasema neno moja likaniumiza.
“Ataaka babuuu!!”
Chozi likanidondoka, nikaujua uchungu anaopitia Jonas kwa kumkosa mzee Aswile lakini nami pia nilikuwa katika uchungu mkubwa kwani laiti kama mzee Aswile angekuwepo ningekuwa natabasamu tena. Na ningekuwa nimemkumbatia Jonas huku tukiwa tumejifunika blangeti zito.
Lakini sasa nilikuwa stendi na mawazo yangu yakiwa yameganda.
Suala la kifo cha Jonas likanichangamsha na kunitia hofu kwa wakati mmoja. Na hapa nikakumbuka sehemu moja ambapo naweza kujaribu kukimbilia. Nikamkumbuka Stephano.” Nadia akasita kuzungumza kisha akanitazama na kuniuliza swali.
“Stephano…jina zuri eeeh!!” nikatikisa kichwa kukubaliana naye.
“….ni heri uwe na jina baya lakini matendo yako yawe mazuri kuliko kuwa na jina baya linaloficha matendo yako….alikuwa anaitwa Mchungaji Stephano na wengi walimuita mtu wa Mungu. Alikuwa anajitolea sana kwakweli, alikuwa akihubiri basi watu wote kimya na alikuwa anagusa samba nafsi. Mara yangu ya kwanza kumfahamu nilienda na akina Monica watoto wa mzee Aswile, ujue pale nyumbani ni mimi peke yangu nilikuwa muislamu, tena muislamu jina tu maana sikuwa nakumbuka hata mwezi mtukufu ni upi, sikumbuki mara ya mwisho kukanyaga msikiti ni lini. Kwa kifupi nilikuwa muislamu wa kale, hivyo ilipotokea familia ile inaenda katika ibada nami nilijumuika nao mara moja moja ninapokuwa najisikia, sikuwahi kulazimishwa kubadili dini hata siku moja. Na pia hakuna aliyewahi kuniuliza kwanini siendi msikitini. Nilipohudhuria kongamano hili ndipo nilimfahamu mchungaji Stephano, alikuja kuisalimia familia nzima ya mzee Aswile na hapo akatambulishwa kwangu. Alikuwa mchangamfu tena mwenye utani sana, haukuwa utani wa kukera, nilipomwambia mimi ni muislam akaniambia tushindane kuomba dua, aisee yule ni zaidi ya muislamu yaani kila aya ninayoifahamu mimi na yeye anaijua. Lakini mbaya zaidi alikuwa anazijua hata nisizozifahamu mimi. Ukaribu wetu ukaanzia hapa.
“Mariam wakristo na waislamu ni watoto wa baba mmoja, usisite kuhudhuria ibada kisa wewe ni muislamu, hakuna anayeutukana uislamu katika ibada na vilevile hakuna mwenye haki ya kuutukana ukristu misikitini sisi ni watoto wa baba mmoja Mariam, usibaki nyumbani mpweke.” Mchungaji aliniambia maneo yale yakaniingia na tangu wakati ule nikawa nikipata hamu ya kusikiliza kwaya nahudhuria kanisani, na kila nilipohudhuria mchungaji Stephano alikuwa akizungumza nami.
Sikuwahi kujutia hata siku moja kuhudhuria katika ibada zao.
Kanisa lao lilikuwa maeneo ya Uyole! Na siku ya kutimiza miaka miwili tangu awe mchungaji tulipata nafasi ya kwenda kwake kusheherekea na familia yake nyumba yake ilikuwa jirani na maeneo ya Uyole. Nilipakumbuka vyema.
Jina la mchungaji huyu likawa jina sahihi kabisa kwa wakati ule, kama aliweza kunielewa vyema tangu nikiwa kwa mzee Aswile na kwa kuwa alikuwa mtu wa kujitolea basi huyu alikuwa mtu sahihi kabisa wa kumweleza matatizo yangu.
Nikaingia stendi, sasa nilikuwqa abiria kweli.
“Mbeya mjini ya mwisho, Uyole Sai, Ilomba, Mama John, Soweto……mbeya mjini ya mwisho gariii..” nilisikia sauti ya mpiga debe akiinadi gari aliyokuwa anasimamia.
Nikaingia garini nikiwa nimembeba Jonas aliyekuwa usingizini nusu na nusu macho!!
Gari likapakia kwa takribani nusu saa, na hapo likaondoka kwa mwendo wa kusuasua likiokota abiria hapa na pale.
Saa tano usiku tulikuwa Uyole, nikashuka baada ya kulipa nauli.
Sasa nikabakiwa na shilingi elfu mbili tu!
Giza lilikuwa limetanda na bado baridi iliendelea kupiga, mji ulikuwa umetulia sana. Lakini niliendelea kusonga mbele hadi nikaifikia nyumba niliyoamini kuwa aliishi mchungaji Stephano. Niligonga geti mara nyingi sana, na hatimaye nikamsikia mtu akiligusagusa.
“We nani?” sauti inayounguruma kutoka usingizini ilisema nami. Nikajitambulisha lakini hakunielewa, nikasema mimi ni muumini wa kanisa la mchungaji Stephano, hapo sasa aliweza kufungua geti.
“Unamtakia nini usiku huu.”
“Mtoto amezidiwa nahitaji huduma yake…” nilidanganya, hapa mlinzi akatilia maanani na kunikaribisha ndani. Kwa jinsi tulivyokuwa tunatetemeka hata angekuwa nani lazima angeamini nilichokuwa nasema. Mlizi akaelekea mlangoni, akanyanyua mkonga wa simu akaanza kusikiliza nikaisikia ikiita kwa ndani maana ulikuwa ni usiku ilisikika vyema. Simu ikapokelewa wakazungumza kwa dakika kadhaa kisha akaushusha mkonga chini na kungojea.
Baada ya kama robo saa akatoka mchungaji kijana, Stephano. Nikamkimbilia na kumwangukia kifuani mimi na Jonas, akaizungusha mikono yake nikalipata lile joto la upendo.
Akanikaribisha ndani sebuleni, nikaingia huku nikiwa nalia kilio cha kwikwi, akaniuliza kulikoni. Huku akiwa ananitazama katika hali ya kutia matumaini na upendo mkuu.
Ningeweza kusita kumweleza mtu yeyote yule juu ya maisha yangu lakini si mtu ambaye anaaminiwa na maelfu kama mtu wa Mungu, na alishiriki katika kuijenga imani yangu. Na alinifanya kila jumapili niione kuwa ya thamani kwa sababu tu alikuwa akiniambia maneno mazuri, Stephano alichangia kwa kiasi kikubwa kurejesha ushirikiano kati yangu na Mungu ambaye niliwahi kusema kuwa amenisahau ama anashiriki katika kunisulubu.
Nikamweleza historia yangu ngumu kwa ufupi sana, nikamweleza jinsi nilivyofika nyumbani kwa mzee Aswile na kisha nikagusia kiundani juu ya taarifa ya tetesi aliyonipa shamba boi juu ya hisia za mama Aswile kwangu mimi kuwa nina mahusiano na mumewe. Mchungaji akaduwaa, lakini nikafikia hadi hatua ya kumweleza kuwa nahisi mama Aswile anahusika katika kumuua mumewe. Hapa akaungana nami kwa hisia hiyo, akatazama juu akawa kama anayenena kwa lugha nisizozijua. Bila shaka alikuwa kiroho zaidi. Pia nikamgusia juu ya Jonas ambaye mama Aswile alidhani ni mtoto wa mume wake, hapa nikamtaja Jesca kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu na nikamweleza mchungaji nkuwa nina tatizo la uzazi na sijawahi kuwa na mtoto. Akanipa pole!!
“Mchungaji! Mimi nimeondoka katika familia ile kwa sababu nachukiwa, na mbaya zaidi nimefanya fujo pale nyumbani. Nipo hapa kwa kitu kimoja tu…uwezo wangu kiakili umefika mwisho, sijui nini cha kufanya na nimechanganyikiwa kabisa. Naomba unisaidie kutatua jambo hili, ni wewe pekee uliyebaki katika maisha yangu, ni wewe waweza kusema neno nami nikajiona ni mwanadamu tena. Tafadhali baba mchungaji!!” nilimsihi kwa sauti ya chini. Na hapo nikayangoja majibu yake.
“Mariam!! Bwana ni mwema na humulika taa kwa watu wake na kamwe hawatajikwaa, malaika wamewazunguka na kuwalinda kwa mabawa yao. Mungu yu pamoja nawe, haujayapita hayo yote kwa uweza wako. Sijisikii vyema sana usiku huu baada ya taarifa hii, sasa nakuomba ulale, mimi ninaingia katika maombi, na nitakesha kukuombea usiku mzima na asubuhi bwana ninayemuamini atatoa majibu.” Aliniambia huku kama kawaida akirusha mikono huku na kule kisha kunena kwa lugha za kigeni.
Mwisho akanipeleka katika chumba maalumu kwa ajili ya wageni.
“Watoto na mama yao wamesafiri nimekuwa mpweke sana, angekuwepo Suzan ungelala naye humo. Lakini hayupo sasa.” Aliniambia kwa kusihi, sikujali., nikaingia chumbani, nilitamani kuoga lakini ile baridi ikanisaliti nikaghairisha na kujitupa kitandani.
Blangeti zito likamfunika Jonas, sasa alitabasamu kidogo, kisha akapotea usingizini. Nami nikawa katika kusinzia. Lakini si hoi kama Jonas, baada ya muda kidogo nikiwa sijasinzia bado nikasikia sauti ikiniita, alikuwa ni mchungaji. Nikajifanya sisikii vyema, akaita tena bado sikuitika. Sijui kwanini sikutaka kuitika, labda ni msongamano wa mawazo kuwa mchungaji ameingiwa tamaa za kimwili ama vipi. Hatimaye akaondoka. Nami nikasinzia kweli.
Nilikuja kushtuka usingizini Jonas alikuwa analia, kilio chake kilitaka kufanana na kile cha usiku ule kisha asubuhi mzee Aswile akafariki. Nilitaka kupuuzia baada ya Jonas kusinzia tena kwani kilio kile hakikudumu. Lakini nikakumbuka kuwa mimi ni Nadia niliyelaaniwa, Nadia mwenye mwonekano wa mwanadamu lakini nikiishi kama kivuli, Nadia mwenye hofu wakati wote. Nadia asiyeaminika, Nadia asiyetakiwa kumwamini mtu.
Nikasimama na kuufungua mlango kisha nikajongea katika sebule, nikijifanya naenda kutafuta maji ya kunywa katika friji. Nikaisikia sauti ikiunguruma kwa chini chini, bila shaka katika simu. Nikaganda katika friji na sasa nikaweza kusikia maneno baadhi, lakini muongeaji akaendelea kujisahau na mwisho akawa anazungumza kwa sauti ya juu.
“Ameshasinzia nimeenda chumbani alipo nimemuita haitiki, amechoka kwakweli. Sasa sika wewe kitu cha msingi kama unafahamiana na bodaboda yeyote yule akupeleke kituoni asubuhi, si umeshachukua RB….wewe wape hela ya mafuta mje na difenda yao mtamkuta hapa…..
….wewe usijali kuhusu hilo, nitakifunga kile chumba mtamkuta kama alivyo. Tena jitahidi sana maana mambo aliyoniambia ni balaa, wewe naye ujifunze kuwa na siri mbona anajua mambo mengi hivyo, je angeenda kwa mtumishi mwingine unadhani tungeonekanaje mpenzi wangu.
……sio kama nakulaumu mamangu, mi nakwambia ukweli mpenzi. Haya hayo yaishe maana hukawii kukasirika. Wewe asubuhi sana uje umchukue halafu mimi nitamalizana na mkuu wa upelelezi afanye tunayotaka. Mbaya sana huyu binti, na niliwahi kukwambia kabisa haya mambo ya kufuga viumbe usiowafahamu ipo siku utafuga majini………(kimya akisikiliza upande wa pili)
…..kuhusu mtoto usijali hata cha msingi huyu paka kwanza. Alfajiri nakifunga chumba mtawakuta wote. Alijifanya mjuaji sana kukupigeni na kukimbia hii Mbeya yetu asingeweza, wewe nilikwambia ukajifanya kukata tamaa…..wewe saa kumi na mbili fika hapa…”
Nilibaki kama sanamu nimeganda pale katika friji. Alikuwa ni mchungaji Stephano, mtu pekee niliyekuwa namwamini kuwa atanisaidia katika tatizo hili linalonikabili, sasa anazungumza na mama Aswile, yaani mama Aswile na mchungaji kumbe ni wapenzi. Mungu wangu!! Nilipagawa, mbaya zaidi alikuwa amesisitiza kuwa asubuhi polisi wanakuja kunishika, na kuhusu Jonas watajua cha kumfanya. Nilitetemeka sana, nikaondoka kwa kunyata nikaelekea chumbani, Jonas alikuwa anapepesa macho huku na kule, na yeye alikuwa ametoka usingizini tena. Ukutani kulikuwa na saa, ilikuwa ni saa nane na dakika hamsini hivi. Sikutakiwa kulala tena, lakini ningetoka vipi katika nyumba ile.
Nadia mimi nilikuwa nimetupiwa pepo la kusalitiwa na kukataliwa, hata kiongozi wa kiroho alikuwa amenisaliti!!!! Hakika niliumia sana, na hapa nikajiona nisiyekuwa na ujanja tena.
Majira ya saa kumi na moja chumba kile kilifungwa kwa nje.
Saa kumi na mbili kama nilivyoyasikia mazungumzo kwenye simu ndo muda ambao askari walitakiwa kufika pale kunikamata. Jonas abaki na kufanywa wanavyotaka.
Milango ya jela nikaiona ikifunguka na Nadia mimi nikitakiwa kuingia. Nikaona akina Desmund wakitabasamu huku mzee Matata na wenzake wakinicheka, Bryan alikuwa akinizomea na familia yangu nzima ikipiga makofi, hata mama yangu akiwa mmoja wao katika orodha.
Nitafanya nini nikwepe mtego huu, kumwamini mtumishi wa kiroho kumeniponza. Muda nao ukazidi kusogea dakika kwa dakika………..mwandishi umewahi kuusikia moyo wako ukiwa wa moto huku ukidunda pigo moja baada ya jingine kwa kasi isiyohesabika. Basi nilikuwa namna ile. Sikuona dalili yoyote ya kujiokoa kutoka pale. Mlango mkuu wa kutokea nje ulikuwa umefungwa na mbaya zaidi mlinzi atakuwa amezuiwa asiniruhusu kutoka nje……..nilimwomba Mungu ile laana iishie kwangu lakini sasa alikuwa kwa mara nyingine amenihukumu na kunipa kisogo, Jonas alikuwa anaishi katika laana yangu, Jonas alsiyejua hili wala lile anahangaika nami..Jonas…Jonaa….asiyeweza hata kusema neno lolote la ubaya kwa mtu anahukumiwa na wanaojitambua, walimuita mwanaharamu sasa watamuua.” akasita kuzungumza, kilio cha kwikwi kilikuwa kimelikamata koo lake. Akalia kwa kujibana bana lakini hakuweza. Alikuwa anatetemeka sana.
Nikamchukua shingo yake na kumlaza begani mwangu, akaendelea kulia.
“USILIE NADIA….machozi yako bado yana thamani sana usiyaruhusu yamwagike zaidi ya hapa Nadia, nilikuahidi tangu siku ya kwanza kuwa sitakusaliti kamwe na nitakupigania upate unachokitafuta. Niamini, na nilikwambia tukifika Dar utajua nini namaanisha….” Nilimsisitiza lakini bado alilia kwa uchungu sana.
Nikamlaza kitandanbi kwangu, nikamfunika na shuka langu, mimi nikakaa katika kochi, Nadia akiwa analia pekee katika shuka.
Katika makochi mimi nikazidi kuchanganyikiwa.
Nadia alikamatwa ama alifanikiwa kuwashawishi wakamwachia?
Kama alikamatwa ilikuwaje akaachiwa huru wakati alikuwa na siri nzito kifuani mwake?
Na Jonas mwisho wake ulikuwa upi?
Vipi kuhusu Desmund?
Vipi mkewe Desmund?? Vipi mama mzazi wa Desmund na yule mzee Matata naye vipi?
Jesca hajulikanai alipo, na yeye hatima yake vipi?
Hakika maswali yalikuwa mengi kuliko majibu…nikatamani Nadia ajue jinsi gani maswali yale yananiumiza kichwa anyanyuke na kuendelea kunijibu. Lakini Nadia hakuwa anajua hilo….akasinzia pale kitandani.
**Haya NADIA katika wakati mwingine mgumu sana wa maisha yake, sasa hayupo pekee bali yupo na mtoto Jonas….nini kitajiri??

KUMBUKA: Simulizi ya NADIA inaelezea matatizo yanayowakumba wanadamu wengi sana, usijiulize Nadia alikuwa mwanadamu wa aina gani bali jifunze kitu kwa kila mkasa anaopiASANTENI.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top