Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA KUMI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SITAISAHAU facebook MTUNZI: Emmy John P. MAWASILIANO: 0654 960040 SEHEMU YA KUMI. Nikamsonya!! Nikavaa kanga yangu nikafungua mlango nikatok...

clip_image002SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI.
Nikamsonya!! Nikavaa kanga yangu nikafungua mlango nikatoka.
Nikaenda hadi lilipo jokofu, nikachukua maji yaliyokuwa katika kopo dogo. Nikachukua na kikombe nikajongea sebuleni.
Hapo mama atagomba kweli!!! Nilijishauri huku nikijiamini kuwa nipo katika hali halisi!! Nyumbani kwangu ambapo mama yangu hajawahi kufika lakini hisia zikaniambia kuwa mama yangu yupo sebuleni na alikuwa anahitaji maji ya kunywa!!!
Sasa nilikuwa sebuleni. Mama hayupo.
Mwalimu Nchimbi naye kwa kununa. Hapo keshanuna huyo.
Nikataka kwenda kumuangaza nje. Lakini sikuona maana hiyo nikataka kumuita, mdomo ukawa mzito sana. Nikageuka huku na huko. Hola!! Nikageuka tena. Hakuna kitu.
Nikajisonya!! Kisha nikaguna mwenyewe kuwa ninamtafuta mtu gizani. Mama naye anakaaje gizani sasa!!
Mpuuzi kweli mimi!!! Nikasogea ukutani nikaanza kupapasa. Nikakipata kiwashio, nikabonyeza. Waaa!! Pakapendeza.
Nikageuka. Waaaa!!! Mdomo wazi, mtu anakula chakula.
Pwaaaa!! Nikaachia kikopo na glasi.
Osmani!!!
Osmani anakula chakula nilichopika mimi. Katika nyumba yangu mimi!!
“Kaa hapo sahivi jamaa si amelala au.” Aliniambia kwa sauti isiyosikika vizuri, alikuwa na pande la nyama mdomoni.
Puuuu!! Nikaanguka. Lakini fahamu zipo pamoja nami.
.Namtazama Osmani.
“John!!!! John!!!” Nilianza kuita kwa sauti ya juu sana. Osman alinitazama akacheka huku akijiziba mdomo. Nikaita tena. Hakuna John aliyetokea kunisaidia.
“Amelala wewe acha kelele.” Alinionya Osman ambaye sasa alikuwa amemaliza kula na alikuwa anakunywa maji. Nikamshangaa.
Alikuwa ananijibu bila wasiwasi wowote.
“Unajua nini Isabela. Tulia tuzungumze, mbona haya mambo madogo tu!!.” Aliendelea kuzungumza Osmani. Kidogo nikatulia sasa, akafanya tabasamu kisha akaendelea kuongea.
“Nimefuata kitu kimoja tu hapa!! Kimoja tu.”
“Nini?.” Niliweza kumuuliza sasa. Nikijilazimisha kuwa jasiri.
“Kitambulisho changu.” Alinieleza huku akiwa amenikazia macho. Sauti yake ilisikika vyema kabisa. Hakuwa katika kutania hata kidogo. Sasa alinikazia macho yake mekundu ya mviringo!!!
“Kitambulisho? Kitambulisho gani?.” Nilihoji. Bado nilikuwa chini.
“Kile nilichokupa siku ile. Pale wapi sijui. Unapajua wewe. Dah halafu hii flat screen yako umenunua wapi aisee zinauzwa bei ghali sahivi duh!! Hongera sana ” alinijibu maneno mengi!!
“Sina kitambulisho cha mtu.” Nilijibu kwa jeuri huku nikijishika kiuno!!
Kama vile jibu lile lilikuwa sawa na kumtukana aliruka akanifikia, kiganja chake kikanyooka akanitandika kofi moja. shavuni Maumivu yakapenya hadi mahali machozi yalipojihifadhi, yakatoka kwa fujo huku kilio nacho kikisindikiza.
“Sasa nadhani unaweza kuniambia. Kitambulisho kipo wapi.” Alinikaripia sasa hakuwa akitabasamu!!
“Nilikichoma moto.” Nilijibu huku kigugumizi kikinitawala na kilio cha kwikwi.
Yule bwana akakodoa macho baada ya kuisikia taarifa hiyo.
“Umefanyaje?” aliniuliza, sikumjibu. Nilikua natetemeka sana, nilianza kumuogopa sana Osmani, kwanza niliwaza kile kitambulisho ni cha John iweje aseme chake? na kwanini siku ile alinipa akasema nilikidondosha? Mhh!! Ushirikina!! Nilianza kuamini kwenye imani hizo ambazo nilikuwa siziamini kabisa hapo kabla. Sauti ya mama niuliiskia kabisa mbona sasa hayupo!! Inamaana Osman ana sauti kama ya mama yangu!!!
Wanafunzi wa SAUT wanaanza kuniroga, wananionea wivu!! Nilihisi.
“ Isabella Isabella!! alinishtua John kutoka kwenye mawazo niliyokua nayo, nilipoangalia kwenye kiti alipo kaa Osmani nikapigwa na butwaa! Osman hakuwepo.
“Kheeee!! Nikashangaa, John akafikiri nimemuitikia yeye akatoka kutoka kwenye mlango wa chumbani alikosimama akanifuata. Uso wake ulikuwa umetawaliwa na uzembe wa usingizini. Bila shaka ndo kwanza alikuwa amegutuka kutoka kitandani!!.
“Vipi baby mbona upo mezani? Mi natoka zangu usingizini, nilishangaa sikuoni, chooni haukuwepo kulikoni mpenzi au njaa. Mi nilikwambia usiku ule ukajifanya mjuaji!!”? Aliniuliza John kwa sauti ya kukwaruza kwaruza huku akipikicha macho yake. Bado nilikuwa nimekaa chini palepale nilipoanguka baada ya kumshuhudia Osmani akiwa ndani ya chumba changu kisha kunizaba kofi kali usoni!!
. Nilishindwa nianze kumjibu vipi John.
Mdomo ulikuwa mzito. Pepo la usingizi lililokuwa linamkabili John lilizidi kutwaa nafasi. Akaonekana kushindwa kuvumilia. Akajivutavuta kuelekea chumbani. Mh!! Nibaki peke yangu hapana!!!
Nilikata shauri. Hata taa sikukumbuka kuzima nikatimua mbio. Nikamfuata John. Sasa nilikuwa katika wasiwasi mkubwa hii haikuwa ndoto tena!!! Yale mamb yalikuwa yametokea kiuhalisia.
Nilichokiona ni kweli kilikuwa kimetokea.
Nilifika chumbani na kumkuta John naye akimalizia kujifunika shuka. Nikaingia kwenye shuka kwa fujo. Hakuligundua hili vurumai labda kwa sababu ya usingizi mzito. Nikamkumbatia John huku nikitetemeka. Nilitamani sana kumueleza lakini maajabu mdomo ukawa mzito sana!!
Hayawi hayawi hatimaye yakawa!! Asubuhi ikafika.
John wangu akaamka wa kwanza. Kuamka kwake kukanifanya na mimi kuukatisha usingizi wangu usiokuwa na ladha kabisa.
“Hivi jana ilikuwa ndoto eeh!!.” Alianzisha mazungumzo John.
“Umeamkaje mpenzi jamani.” Nikamkatisha kwa salamu, maana hatukuwa tumesalimiana. Akanijibu kisha akaendelea kuzungumza.
“Jana si nikaota aisee. Dah!! Ndoto nyingine nazo!! Ila kuota pesa ni dalili za utajiri.” Alinieleza huku akipiga mwayo mrefu!!
“Ndoto gani tena. Nikamuuliza.”
“Eti amekuja mgeni sijui ilikuwa nyumba gani. Umezungumza naye, alipotoka eti akakuachia wewe Cheque mezani sijui milioni ngapi huko. Nilipotokea si wivu ukawa umenizidi. Nikawa mkali. Akawa kama anahairisha kukupatia. Mi nikaondoka, baadaye nikawa nachungulia mh!! Akaiweka sijui chini ya sahani ile. Ulipotoka kumsindikiza nikawahi kufunua nikakuta amekuandikia kiujumbe hata sikukielewa. Sasa nikawa nakusubiri unieleze yule ni nani. Mara kuku wako haoo wakawika kumekucha tayari!!!” Alimalizia kwa kicheko kirefu John. Nami nikaungana naye. Tukacheka.
“Una wivu we mwanaume!!.” Nilimweleza.
“Ah!! Ndoto tu hizo.” Alifunga mjadala.
Wakati John anaingia kuoga, mimi niliamka na kuanza usafi wa hapa na pale. Nikiisaili nyumba yangu. Sasa nilikuwa sebuleni. Nilipofika pale palikuwa kawaida tu!!
Hivi kumbe jana nilikuwa naota!! Nilijisemea na mimi.
Nikaanza kutoa vyombo mezani. Tayari kwa kuviosha na ambavyo havijatumika nivirudishe mahala pake. Ni hapo ndipo nilipopatwa na mshtuko mwingine mkubwa. Chini ya sahani moja palikuwa na karatasi. Karatasi ya rangi ya kijani kibichi.
Hili jani ama karatasi? Nilijiuliza. Nikajikaza nikausogeza mkono nikalishika.
Lilikuwa karatasi!! Nikalinyanyua kwa uoga mkubwa. Bado liliendelea kuwa karatasi. Mkono wa pili nao ukajisogeza ukalipakata.
Kisha nikaligeuza.
Maandishi!!! Ya rangi nyeupe. Kiswahili sanifu, maneno machache.
AFE AMA UKUBALIANE NAMI.
Nani sasa? Nikajiuliza. Na nimewakosea nini mimi jamani eeh!! Nililaumu!!
UTAMFAHAMU HIVI KARIBUNI.. Maandishi yale yalimalizia kama yanayojibu swali langu.
Mwisho zikawekwa alama ambazo nilihisi kuwa ni namba za simu. +666666666. Simu ya wapi hii!! Nilitafakari.
Nikahisi wazimu unataka kunipanda. Akili zikasogeleana niliposikia John akiufunga mlango wa bafuni. Nikatwaa kile kikaratasi nikakificha kabatini upesi!!
Sikutaka John agundue kitu chochote. Maana kugundua kwake kungesababisha nimueleze pia juu ya kitambulisho, pia juu ya mauaji aliyoyafanya ndotoni na sasa yametokea kweli. Haukuwa wakati muafaka wa kumueleza.
Kuna jambo nilitakiwa kuliweka sawa kabla ya kuwa muwazi. Jambo hilo sikulijua lakini nikaendelea kuwa msiri!!
******
Jina langu lilizidi kukua katika chuo cha mtakatifu Augustino, wasichana wengi walitamani sana wawe kama mimi maana hakuna kitu ambacho nilikua sina katika maisha yale, takataka zote za urembo nilikua nazo, cha ajabu mimi Isabella sikuonekana kuwa karibu na msichana yeyote yule, hata rafiki yangu Happy nilimsahau, hela kitu kingine bwana nilisahau mema yote aliyonitendea Happy maana maisha yalivyokua yananipiga mtu wa kwanza kumfuata alikua yeye lakini kwa wakati ule nilimsahau kabisa
Mtu wa jirani yangu alikua John nilisahau kabisa kuwa John aliniacha kwa ajili ya umasikini wangu, sikufikiria kabisa kuwa anaweza kuwa yupo nami kisa ya pesa nilizokua nazimiliki,pesa za kutotolea jasho zaidi ya kuwaelimisha tu watu kidogo. kweli mapenzi ni upofu.
****
(UTATA)
Mama weeeeeeeeeeee!!!nilishtuka kutoka kwenye ndoto mbaya, ndoto iliyonitoa jasho jingi nililowa utafikiri nilijimwagia maji,.
Ilikuwa ndoto mbaya nyingine katika orodha ya ndoto zangu za hivi karibuni. Niliota nipo kwetu Makambako, siku hiyo tulienda kupamba ukumbi wa sherehe na mama yangu ambaye alizoeleka kama Mwalimu Nchimbi, tulimaliza saa tano usiku, hatukupata gari la kuturudisha nyumbani tukaanza kutembea kwa mguu kwa sababu mahali pale hapakuwa mbali sana na nyumbani, mara tukasikia kama mchakato fulani nyuma yetu!! tukashangaa nyuma vijana wawili wakitufuata kwa kasi. Tuliamini kuwa walikuwa vibaka. Mama akaanza kukimbia na mimi nikafuata nyuma huku tukipiga kelele za kuomba msaada, hatukupata msaada wowote tukazidi kukimbia kwa juhudi zote na sasa kila mmoja akaanza kuchoka. Na mwendo ukaanza kupungua!!
Mama akasema maneno fulani ya kukata tamaa huku akimkabidhi Mungu madaraka ya kuamua kitakachotokea kwetu. Mimi sikuwa na neno la kuongezea nikiwa nimekata tamaa niligeuka nyuma kutazama vijana hao watatuua kwa silaha gani. Badala ya kutilia maanani silaha zao kali walizobeba, macho yangu yakatua kwenye sura zao. Zilikuwa ni sura ninazozifahamu kabisa!!
Osmani!! Alikuwa anatabasamu. John!! Yeye alikuwa amekunja sura kwa ghadhabu. John wangu!! Nilishangazwa sana na uwepo wa John katika kunikimbiza mimi na mama yangu mzazi.
Niliendelea kutulia nikitegemea maswali kutoka kwa viumbe hawa wasioonyesha huruma hata kidogo. Sikuulizwa swali.
Mara wakagawana majukumu. John akamwendea mama na Osmani akanifuata mimi. Alikuwa ameshikilia kitu mfano wa mkia, aliponifikia akanitandika nao mikononi. Maumivu yakapenya nikatokwa na yowe kubwa sana nikaanza kugalagala. Akaniacha pale akamfuata mama. Wakasaidiana na John kumnyanyua mama halafu wakaanza kukimbia naye huku wakimburuza. Mimi waliniachga palepale chini!!
Nilipiga kelele nikiwasihi wamuache mama yangu. Lakini hakuna walichobadilisha walizidi kukimbilia na kupotelea gizani. Nilipiga mayowe sana lakini hakutokea mtu wa kunisaidia. Nilipoanza kujigalagaza kwa kukata tamaa ndipo nikakutana na ardhi ya ajabu, ardhi inayonesanesa. He!! Ardhi ya wapi hii inanesa kiasi hiki?
Nilijiuliza huku nikijilazimisha kufumbua macho yangu, macho yalikuwa mazito sana kufumbuka. Nikajilazimisha hadi yakafumbuka.
Nikakutana na giza nene, nikaanza kupapasa huku na huko, nikakutana na vitu vingine viwili vinabonyea nilipojilazimisha zaidi kuvitazama ndipo nikakutana na mito miwili katika kitanda changu. Na ile ardhi ndio hiki kitanda changu cha sita kwa sita. Ndoto!!!
Nikawasha taa lakini nikahisi maumivu makali katika mikono yangu, Kheee! nikashtuka kukuta mikono yangu imevimba na ina alama ya kama michirizi hivi, hofu ikanitanda mhh!! ina maana ilikua ya kweli ama? Kama ni kweli kwa hiyo John amempeleka wapi mama yangu?
Wamempeleka wapi mwalimu Nchimbi!! Nikaendelea kutahamaki. Hali hii sasa ilikuwa ya hatari kupita zote.
Gusa popote katika maisha yangu ila chunga usimguse mama yangu. Nichezee uwezavyo, ninyanyase uwezavyo lakini kamwe usiyafanye haya kwa mama huyu aliyenibeba tumboni kwa miezi tisa. Kwa gharama yoyote lazima ujutie ama la nijute mimi.
Kama hii ni kweli John lazima anieleze ni wapi wamempeleka!!
Nilijiapiza. Sitajali kama hii ni ndot ama sio ndoto!! Mama yangu!!! Mama mama kabisa!!!
Upesi nikapapasa na kuipata simu yangu ya mkononi. Bila kujalisha ulikuwa usiku wa saa ngapi ilikuwa lazima nimpigie mama niweze kujua nini kinatokea huko walipo , nikajaribu kumpigia hapatikani!! Nikaogopa kukubaliana na ukweli huo. Kwamba na ndoto ile ilikuwa sahihi kama zilizopita na kuondoka na uhai wa wanadamu.
Mungu wangu mama hapatikani ana nini jamani? nilijiuliza hivyo huku nikisahau kuwa huo ulikua usiku na inawezekana akawa amezima simu.
Ilikua kama saa tisa za usiku..nikampigia baba naye akawa hapatikani, kwa baba sikuwa na wasiwasi niliamini huenda amelala vilabuni.
Nilijiuliza maswali mengi huku nikijiuliza kwanini mambo yale yananitokea mimi, ni wapi nimekosea.
Niliumiza kichwa sana hatimaye usingizi ukanitwaa. Na kuwaza kukakoma!!!
Bila kujua hatma ya mama!!!
Nilishtuka baadaye kutoka usingizini baada ya simu yangu kuita kwa mda mrefu, kuangalia jina ni la mdogo wangu, usingizi wote ukaniisha nikakumbuka ile ndoto ya usiku, hofu ikanitanda nikawaza au mdogo wangu alikua ananipigia kunipa habari za msiba wa mama? mara simu ikakatika.
Nikampigia mdogo wangu!!! Nijue kulikoni, wakati huo natetemeka mwili mzima. Jasho likinitoka. Sikutaka kuamini hii ndoto.
Kwa hili nilichanganyikiwa kuliko vipindi vyote nilivyowahi kuchanganyikiwa!!
Simu ikaita. Mara ya kwanza haikupokelewa!!!
Nikazidi kutetemeka!!!
Mara ya pili simu ikapokelewa.
“Dada..shkamoo.”
Alinisalimia. Sikuweza kumjibu. Nikamuulizia mama. Akasita kunijibu. Nikamsikia akihema juu juu. Wasiwasi wangu ukazidi.
“We Helena!!” nilimuita katika simu.
“Abee!!” aliniitikia.
“Si nimekuuliza kama mama ni mzima.”
“Ndio Ni mzima. Ila ana homa.”
“Naweza kuongea naye sasa hivi?.” Nilimuuliza hakujibu swali lile akazalisha mengine. Nikaanza kuiamini ndoto yangu!!!
“Niambie mama ana nini?” sasa nilimkaripia.
“Mama ana homa kali amelala!!.”
Nikakata simu. Nikasimama wima. Hofu kuu!!
Nifanye nini sasa!! Nilijiuliza. Kisha nikaamua kwa ujasiri kumtafuta John, tayari ilikuwa alfajiri. Nikabonyeza namba zake. Nikawa nasikiliza huku nikitawaliwa na uoga.
Simu yake haikuwa hewani. Wasiwasi ukazidi.
Ina maana John ndio ameenda Makambako kwa mwalimu Nchimbi!! John ni mshirikina ama??
Nilijiuliza. Sikupata jawabu. Hakuwepo wa kunijibu vilevile.
Ilikuwa lazima nifanye kitu. Hapakuwa na muda wa kujilaza tena!!!
Nikaufunga mlango nikatoweka!!
Teksi niliyochukua ikanifikisha nyumbani kwa John. Nilikuwa nimeamua kuitoa siri yote ilimradi kuokoa maisha ya mama. Nilijiuliza John atanifikiriaje kwa haya mashairi ambayo naenda kumuimbia. Litakalokuwa na liwe!! Nilijitia imani.
Kama nilivyopiga simu ya John bila kupokelewa ndivyo ilivyokuwa katika mlango wake. Mlango haukufunguliwa na yeyote. Nilibaki katika mshangao hadi alipofika jirani yake na kunitaarifu kuwa hata yeye hajui
John alipoenda, ni masaa kadhaa yalikuwa yamepita.
Nilikubaliana naye. Nikatoweka, moyoni nikiwa nazidi kuifuga hofu.
John hapatikani nyumbani kwake masaa yamepita, mama yangu ana homa kali hawezi kuongea kwenye simu, nimetoka kuota ndoto mbaya John na Osman wanamkwapua mama yangu. Matukio haya yanayowiana yalinitia mashaka. Mama yangu amekufa! Niliwaza huku nikiichukia hali iliyonikumba. Sikujua ni uelekeo upi natakiwa kwenda, nilisimama chini ya mti nikaanza kuwapigia simu rafiki zake John, wote wakakiri kuonana na John lakini masaa kadhaa yaliyopita. Hakuna aliyemuona muda mfupi uliopita.
“Hakuwa na safari yoyote?” Nilimuuliza mmoja wao. Akapinga hoja hiyo. Nikazidi kuumia.
Nilirejea nyumbani kwangu nikiwa nimekata tamaa sana. sikuweza kulala wakati jina la mama likinishambulia kichwa changu.
Nilijaribu mara kwa mara kupiga simu ya John. Hali ikawa ileile.
Hatimaye nikafikia maamuzi binafsi. Nikaamua kurejea Makambako nikashuhudie tatizo gani limemsibu mama yangu.
Nilipoiwaza safari hii nikaukumbuka na ule ujumbe wa ‘AFE AMA UKUBALIANE NAMI’……walimaanisha mama yangu ama?? Sasa nikubaliane na kitu gani jamani mimi!!!!
Kama ilivyokuwa awali nikazungumza tena na kiongozi wa darasa kwa ajili ya kunitetea kwa lolote litakalotokea mimi nikiwa safarini.
Nikampatia kiasi kikubwa cha pesa ili kumshawishi zaidi. Akashawishika.
****

****ISABELA anaapa kuwa iwapo ni kweli alichokiona ndotoni, basi aliyefanya vile lazima ajutie…….nini kitajiri???
***OSMAN ni nani na ametokea wapi??
**Dokta Davis naye………anashughulika na nini??
**John ame[potelea wapi?? Je ni kweli anahusika katika kukwapua mama yake!!
ITAENDELEA ……..!!!

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top